Umoja wa matwali’i na kufanya bidii kutafuta mwezi mwandamo wa Ramadhan

 بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ

Swali:

Ndugu yangu mkarimu:

Assalamu Alaykum Warahmatullah Wabarakatuh

Kulingana na barua yako ya tarehe 24/06/2018 inayohusu kufanya bidii ya kutafuta mwezi mwandamo wa Ramadhani wa mwaka huu, ningependa kuelezea yafuatayo:

Tofauti ya nyakati iliyopo hapa na Palestina na California ni masaa kumi, yaani wakati wa kuuona mwezi mwandamo California, itakuwa hapa kuchomoza kwa alfajiri kumeshapita  kwa masaa matatu, jambo linalo maanisha kumalizika kwa usiku kiukamilifu bila ya kuthibitika kuuona mwezi mwandamo katika usiku huo, ambapo itakua sahihi kula kwetu mchana katika siku ile ya Jumatano. Eneo letu (Palestina) halishirikiani na California katika sehemu yoyote ile ya usiku, wakati ambapo huo usiku ndio mahali (wakati) wa kuuona mwezi mwandamo.

Na kumalizika usiku kikamilifu bila ya kuthibitika kuonekanwa kwa mwezi mwandamo, ijapokuwa itakuwa umeshazaliwa kunatufanya sisi tuwe katika hukmu ya waliogubikwa anga lao na mawingu (man ghumma ‘alayhim), na itakua kula kwetu mchana na msimamo wetu wa hukmu shar’i ni sahihi. Ama kufunga siku moja ya Shawal kwa nia ya kulipa siku ya Jumatano hii humaanisha kulipa siku ya shaka (yaumush-shakk)  ambayo haifai kufunga siku hiyo kabisa.

Angalizo muhimu: Maeneo yaliyopo karibu kwenye pande mbili za Msafiri wa Tarehe wa Kimataifa (International Date Line) yanaungana katika matwali’i  kwa mujibu wa mwezi (qamari) kwahiyo hushirikiana katika kuanza mwezi wa qamari (mwandamo) ijapokuwa kuna tofauti ya nyakati baina yao ambayo ni masaa 24. Kwahiyo mazingatio ni katika kuanza kwa mwezi wa qamari (mwandamo), sio kwa kile kinachoitwa siku hizi ‘Kwa mujibu wa makadirio ya kilimwengu’, bali ni kwa kuuona.

Haya ndio niliyonayo, na Allah Mtukufu ni Mjuzi zaidi.

Wassalamu Alaykum Warahmatullah Wabarakatuh.

 

Jawabu:

Waalaykum Salaam Warahamatullah Wabarakatuh

Nimeisoma barua yako, inadhihirika kwamba mkanganyiko ulionao ni katika maudhui mwezi mwandamo wa Ramadhani…

Ndugu yangu, kuna nukta lazima zijulikanwe kiukamilifu katika maudhui hii:

1-Hakika Mtume (SAW) anasema:

«صُومُوا لِرُؤْيَتِهِ وَأَفْطِرُوا لِرُؤْيَتِهِ»

“Fungeni kwa kuuona na fungeni kwa kuuona”, hii ni amri ya jumla kwa ajili ya Waislamu (khitwaab ‘aam lilmuslimiin)  ambayo ina maana mwezi mwandamo utakapoonekanwa katika mahali popote pale basi ni juu ya Waislamu katika sehemu zote wajifunge nayo (amri/khitwab) hiyo … Nukta hii ni muhimu kuielewa… Narejea, ni muhimu kuielewa…

Na kwa hiyo, fahamu yoyote au istinmbaat au tafsiri ya kwamba Waislamu si wajibu juu yao kufunga na kufungua kwa pamoja hiyo ni fahamu yenye kasoro inayopingana na kilichotabaniwa. Kwahivyo, uliyoyafikia wewe katika barua yako ya kwamba watu wa California ni faradhi juu yao kufunga siku ile na watu wa Palestina si faradhi juu yao (kufunga siku ile) ni kwamba yanapingana na fahamu ya hadithi iliyotabaniwa ya umoja wa kufunga na kufungua.

2-Hakika yaliyomo kwenye barua yako ya hisabu ya tofauti baina ya Palestina na California si kina katika utafiti. Unasema hivi: (Tofauti ya nyakati iliyopo hapa na Palestina na California ni masaa kumi, yaani wakati wa kuuona mwezi mwandamo California, itakuwa hapa kuchomoza kwa alfajiri kumeshapita  kwa masaa matatu, jambo linalo maanisha kumalizika kwa usiku kiukamilifu bila ya kuthibitika kuuona mwezi mwandamo katika usiku huo, ambapo itakua sahihi kula kwetu mchana katika siku ile ya Jumatano. Eneo letu (Palestina) halishirikiani na California katika sehemu yoyote ile ya usiku, wakati ambapo huo usiku ndio mahali (wakati) wa kuuona mwezi mwandamo.

Na kumalizika usiku kikamilifu bila ya kuthibitika kuonekanwa kwa mwezi mwandamo, ijapokuwa itakuwa umeshazaliwa kunatufanya sisi tuwe katika hukmu ya waliogubikwa anga lao na mawingu (man ghumma ‘alayhim), na itakua kula kwetu mchana na msimamo wetu wa hukmu shar’i ni sahihi. Ama kufunga siku moja ya Shawal kwa nia ya kulipa siku ya Jumanne hii humaanisha kulipa siku ya shaka (yaumush-shakk)  ambayo haifai kufunga siku hiyo kabisa). Hisabu haiku hivyo:

a-Ndio, tofauti baina ya Palestina na wao (California) ni kiasi cha masaa kumi, Palestina ipo kwenye Latitudo 35 Mashariki, na California ipo kwenye Latitudo 120 Magharibi, yaani tofauti baina yao ni (23+120=155) na kila mstari wa Latitudo ni kiasi dakika 4, kwahiyo tofauti itakuwa kiasi cha masaa kumi, lakini kuelekea mbele sio kwa kurudi nyuma. Kwahiyo nyakati kwetu ziko mbele ya California na haziko nyuma. Jua likitua huko, yaani umeshaanza usiku wa Alkhamisi kwao na iwe saa kumi na mbili za jioni (18), kwetu usiku huu wa Alkhamisi utakuwa unakurubia kumalizika, yaani wakati wetu utakuwa (18+10=28), yaani kiasi cha saa kumi za alfajiri ya siku ya Ijumaa, yaani kiasi cha karibu na adhana ya alfajiri…, na si kama ulivyohesabu kwa kurudi nyuma, ukafanya masaa kumi kwa kurudi nyuma, ukasema wakati kwetu utakuwa (18-10) yaani saa mbili za asubuhi! Hivyo itakuwa saa mbili za asubuhi za siku yoyote katika Palestina katika California itakuwa kiasi cha saa nne za usiku za siku hiyo, kwahiyo usiku wa siku huutangulia mchana wake… Kwahivyo, jua la siku katika Palestina huchomoza kabla ya kuchomoza katika mji wa California katika siku ile… Na huzama jua katika Palestina kabla ya kuzama kwao California. Kwa mfano, wakati linapokuchwa jua kwao kiasi cha saa kumi na mbili “18” za jioni ya siku ya Jumane, yaani usiku wa Jumatano, kwetu itakuwa karibu na alfajiri, yaani saa kumi (10) za alfajiri ya siku ya Jumatano. Kwahiyo, lenye nguvu ni kwamba kuna ushirikiano katika sehemu ya usiku hata ikiwa ushirikiano huu ni mdogo wa kiasi gani.

b-Pamoja na hayo, hebu tujaalie kwamba maeneo hayo mawili hayashirikiani katika sehemu ya usiku, basi funga yao na kufungua kwao huwa moja. Ufafanuzi wa hilo ni kama ifuatavyo:

-Tujaalie kuna maeneo matatu a, b, na c. na kwamba a linashirikiana na b katika sehemu ya usiku kwahiyo litafunga na kufungua pamoja nalo… b linashirikiana na c katika sehemu ya usiku na kufunga na kufungua pamoja nalo… Hiyo ina maana kwamba a ina wajibu  wa kufunga na kufungua pamoja na c. Ni sawa ikiwa a linashirikiana na c katika sehemu ya usiku au halishirikiani. Lililo wajibu kwamba a na c wanafunga na kufungua pamoja, hiyo ni kwasababu a linashirikiana na b katika sehemu ya usiku kwahiyo hufunga na kufungua pamoja. Na b na c yanashirikiana katika sehemu ya usiku kwahiyo wanafunga na kufungua pamoja  kama tulivyotaja punde hivi. Na kwamba hali hii ni kama yalivyo maeneo yote ya dunia. Kwahiyo, matumizi ya hadithi Fungeni kwa kuuona na fungueni kwa kuuona ni jumla (‘aam) kwa maeneo yote ya dunia.

3-Kwahivyo, hata ikiwa Palestina haikushiriikiana na California katika sehemu ya usiku, ikiwa sahihi hivyo kama ilivyoelezwa kwenye barua yako, basi itakuwa lipo eneo baina yao (Palestina na California) mfano katika Afrika linashirikiana na California katika sehemu ya usiku na pia linashirikiana na Palestina katika sehemu ya usiku kwahiyo, litafunga na kufungua pamoja na California na wakati huohuo linafunga na kufungua pamoja na Palestina…  Na itakuwa Palestina na California wanafunga pamoja. Kwahiyo, maeneo yote ya dunia watafunga na kufungua pamoja. Na ndivyo inavyofanya kazi hadithi ya Mtume (SAW) kuwa ni wajibu kwa Waislamu kufunga na kufungua kwa pamoja.

4-Ama tukichukulia kama ulivyodhania kuwa kushirikiana sehemu katika usiku  ni lazima iwe baina ya California na Palestina ili wafunge na kufungua kwa pamoja, na kuwa hayashirikiani (maeneo haya) katika sehemu ya usiku kwa mujibu wa maelezo yako yaliyomo katika barua yako, hii humaanisha kutofanyia kazi maana ya hadithi ya Mtume (SAW) ya kwamba kufunga na kufungua ni wajibu iwe kwa pamoja kwa Waislamu wote. Na kwa hali ilivyo, hili linapingana na lile tulilolitabani na kulilingania kwalo la umoja wa Waislamu katika kufunga kwao na kufungua kwao. Na kwa hakika tulitoa nashrat  (toleo) juu ya jambo hili katika tarehe  25 Shabani, 1415H/ 14 Dcember, 1998.

5-Ama kauli yako ya kwamba usiku unaanza Palestina na jua ndio linachomoza huko California kwahiyo vipi funga itakuwa. Hili sio jambo zito, kwa mfano sisi tunauona mwezi mwandamo baada ya kuchwa jua siku ya Jumatano, na Alkhamisi tunafunga, na wakati wa California itakuwa mchana wa Alkhamisi, kwahiyo linapozama jua la Jumatano kwao ni sawa, kama wameuona mwezi mwandamo au hawakuuona, kuuona kwetu sisi mwezi mwandamo huwalazimisha wao kufunga Alkhamisi… Na ama ikiwa hatukuuona sisi kwetu baada ya kuzama jua Jumatano na wao baada ya kuzama jua Jumatano kwao wameuona, lakini taarifa zikatufikia mchana wa Alkhamisi, kwahivyo tutalipa siku hiyo. Na hili litafanya kazi mwanzo wa mwezi na mwisho wake, yaani usiku wa Eid…

Na hakika limetokea hili wakati wa Mtume (SAW), kama ilivyoelezwa katika hadithi ambayo ameitoa Ahmad katika musnad wake kutoka kwa Abi Umair bin Anas, amenieleza jamaa yangu wa upande wa ami yangu katika Ansar miongoni mwa Masahaba wa Mtume (SAW) amesema:

«غُمَّ عَلَيْنَا هِلَالُ شَوَّالٍ فَأَصْبَحْنَا صِيَاماً فَجَاءَ رَكْبٌ مِنْ آخِرِ النَّهَارِ فَشَهِدُوا عِنْدَ رَسُولِ اللَّهِ صلى الله عليه وسـلم أَنَّهُمْ رَأَوْا الْهِلَالَ بِالْأَمْسِ فَأَمَرَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسـلم (أَنْ يُفْطِرُوا مِنْ يَوْمِهِمْ وَأَنْ يَخْرُجُوا لِعِيدِهِمْ مِنْ الْغَدِ)»،

“Mawingu yalitufanya tusiuone mwezi mwandamo wa Shawal, tukaamka tumefunga, wakaja wapanda wanyama mwisho wa mchana wakashuhudia mbele ya Mtume (SAW) kuwa wao wameuona mwezi mwandamo jana, kwahiyo Mtume (SAW) akaamrisha (kuwa wafungue siku yao ile na kuwa kesho watoke kwa ajili ya Eid yao)”. Kwahivyo, Mtume (SAW) aliwaamrisha wafungue katika siku ambayo waliihesabu kuwa ni Ramadhani kwasababu ya kuonekanwa mwezi mwandamo wa Shawal na wasiokua wao katika sehemu sio Madina Munawara. Lile kundi la wapanda wanyama liliuona mwezi mwandamo kabla ya kufika Madina na watu wa Madina hawakujua kuuona kwao huku, na wakaamka asubuhi wamefunga. Lakini walipoelewa kwamba Waislamu wengine wasio kuwa wao wameuona mwezi mwandamo, ndipo Mtume (SAW) akawaamrisha kufungua siku ile… Ama siku hizi, vyombo vya habari vilivyojaa katika nchi zote vinaweza kunukuu habari za kuonekanwa mwezi mwandamo kwa dunia nzima ndani ya sekunde chache  tu na kuwalazimu Waislamu kufunga au kufungua kwa kusikia taarifa ya kuthibitika kuonekanwa mwezi mwandamo katika sehemu yoyote ile ya dunia…

Kwahiyo, jambo hili sio zito, bali ni jepesi kwa mwenye kuwepesishiwa na Allah, na hasa kwa kuwa mawasiliano siku hizi yamekuwa kama kupepesa kwa jicho.

6-Ama siku ya shaka (yaumush-shak), sio kama ulivyoeleza wewe, bali ni mwezi (tarehe) thelathini Shaban, siku ambayo haijakufikia habari ya Muislamu yeyote ya kuuona mwezi mwandamo katika sehemu yoyote duniani. Siku hii ndio haifai kufunga. Na ikikufikia habari kwamba kuna mtu (Muislamu) ameuona mwezi mwandamo na hali yakuwa wewe umeshakula kwasababu ulikuwa unadhania hiyo kuwa ni siku ya shaka (yaumush-shak), kwahiyo, ikikufikia habari ndani ya mchana wa siku hiyo kwamba mtu mmoja (Muislamu) ameuona mwezi mwandamo, hapo itakuwa siku hiyo sio siku ya shaka (yaumush-shak) bali itakulazimu kuilipa.

Kwa ufupi, ni kuwa hadithi ya Mtume (SAW) ya:

(صوموا لرؤيته…)

 “Fungeni kwa kuuona…” inakusanya dunia nzima, na kauli yoyote kinyume na hii huwa ni ya makosa au ina kasoro. Na Allah ndie Mjuzi zaidi na Mwenye Hekima zaidi.

Na mwisho kabisa, je si bora zaidi ewe mtekelezaji wa kheri (Nafeth) ungeuliza kwa kutaka kubainishiwa badala ya kuuliza hali yakuwa umeshachukua msimamo? Sivyo hivyo?

Ndugu yenu Atta bin Khalil Abu Rashtah

22, Shaban 1440H

28, April 2019

Maoni hayajaruhusiwa.