Tatizo Afrika Ya Kusini Ni Zaidi Ya ‘Zuma’
بسم الله الرحمن الرحيم
Juni 29 Mahkama ya Kikatiba ya Afrika Kusini ilimhukumu aliyewahi kuwa Raisi wa Afrika ya Kusini Jacob Zuma (79) kwenda jela kwa miezi 15 kwa kupuuza mahkama hiyo iliyomtaka atoe utetezi wa tuhuma za rushwa zinazomkabili kwa Tume ya Zondo (The Zondo Commission), tume inayoongozwa na Naibu Jaji Mkuu Raymond Zondo, iliyopewa jukumu na serikali ya nchi hiyo kuchunguza madai ya ufisadi na rushwa yanayomkabili Jacob Zuma kwa kipindi chote cha miaka 9 ya uraisi wake.
Zuma alisitasita kujisalimisha kwa polisi ambao walipaswa kumtia nguvuni, pia akatumia haki ya kimahkama kupinga maamuzi ya mahkama. Hata hivyo, hukmu ikabakia kama ilivyo na ikawa kwake lazima kutumikia kifungo kama ilivyoamuliwa na mahkama, na kufanya kuwa raisi wa mwanzo katika Afrika ya Kusini kufungwa jela.
Hali hiyo iliwafanya wafuasi wa Zuma na watu wengi kupinga kifungo hicho na kuanza kampeni kabambe ya kupigania kuachiwa Zuma huru. Kampeni iliyoanza kumi la mwanzo la mwezi huu wa Julai ikiambatana na mandamano, vurugu na machafuko makubwa yaliyosambaa kila mahala kama moto katika nyasi kavu, kiasi cha kugharimu uhai wa watu zaidi ya 300, majeruhi wengi, mahabusu na kupelekea jeshi la nchi hiyo kuingilia kati.
Japo kwa juu juu tutaona sababu ya vurugu za mara hii ni tofauti na vurugu nyingi zilizotangulia hususan zile dhidi ya wahamiaji wa kigeni ndani ya miaka ya 1994, 1995, 2008 na 2015 ambapo zililenga zaidi wahamiaji na wageni kwa kutenda uvamizi wa silaha, kuwaua, uvunjaji wa nyumba zao, kuwafukuza na kuwatoa kwenye makaazi yao, kuvitaka vyombo vya dola viwarejeshwe makwao nk. Lakini katika msingi wake ni sawa.
Vurugu za safari hii zilizoasisiwa na wafuasi wa Zuma zimeanza kwa sababu za juu juu za kuonesha kutoridhishwa kwao na maamuzi ya kimahkama na vyombo vyao vya kusimamia haki pia kuwa na hisia kuwa kuna mkono wa kisiasa katika kuchafua jina na haiba ya Jacob Zuma.
Kwa upande wa serikali msimamo wake juu ya ghasia hizi umedhihirishwa na Raisi Cyril Ramaphosa ambae tangu kuzuka vurugu hizo ameshahutubia raia kupitia runinga mara tatu, ambapo serikali yake inaona kwamba machafuko hayo nchini humo ni hujma yenye lengo la kudhoofisha mamlaka ya katiba, kuharibu uchumi, kuondosha uthabiti wa kijamii na kudhoofisha utawala wa kidemokrasia.
Vurugu hizi na machafuko haya yenye kuambatana na kuzuiya barabara nyeti za kibiashara, kupiga moto viwanda na vitega uchumi vikubwa, kuharibu mali na wizi ulioruka mipaka hazionekani kuwa ni suala la kupigania uhuru wa Zuma tu, bali qadhia ya Zuma ni kama imedandiwa kuwakilisha machungu mengi ya wananchi hususan katika hali ya kisisa na kiuchumi.
Afrika ya Kusini licha ya kutajwa kuwa miongoni mwa vinara bora wa demokrasia, nchi ya pili kuwa na uchumi wa juu barani Afrika, ikiwa na miundo mbinu bora, nidhamu mwanana iliyoboreshwa ya masuala ya kifedha na kuwepo uzalishaji wa hali ya juu wa maadini na viwandani, lakini nusu ya raia wake wanaishi chini ya mstari wa umaskini, na ukosefu wa ajira umetapakaa kiasi cha Raisi Ramaphosa kuwahi kusema kuwa ni “mgogoro mkubwa na wa hatari”. Hivi sasa ukosefu wa ajira ni 32% kwa miezi mitatu iliyopita ndani ya mwaka huu.
Profesa Mcebisi Ndletyana ambae pia ni mchambuzi wa kisiasa nchini humo ameliambia shirika la Habari la Al-Jazeera kwamba nchi hiyo ni miongoni mwa nchi zenye hali mbaya sana katika kukosa usawa baina ya raia wake, jamii inajihisi kama imetelekezwa na serikali na wana hivyo wana ghadhabu.
Uchumi ya kibepari imeisukumiza Afrika ya Kusini kama zilivyo nchi nyengine changa katika shimo kubwa la maangamizi ya ufukara na umaskini licha ya rasilmali nyingi zilizopo, kukosekana uwiano wa kiuchumi baina ya wenye nacho na wasiokuwa nacho. (maskini na matajiri), na kubwa na la hatari zaidi ni kuzalisha ghadhabu na kuchanganyikiwa kwa raia, na kusubiri tu fursa yoyote kupunguza chuki na ghadhabu zao.
Maoni hayajaruhusiwa.