Donald Rumsfeld Na Maadui Wenzake Wataondoka Lakini Umma Wa Kiislamu Utabakia

بسم الله الرحمن الرحيم

Amesema Mtume saw katika Hadithi aliyoipokea Abu Qatada bin Rabi Al-Answari
“Muumini anapokufa hupata ahueni ya mitihani ya dunia na huondoka kwa neema ya Mola, wakati mtu muovu anapokufa huacha ahueni kwa wanadamu, miti ardhi na wanyama. (Bukhari – Hadith no. 6512)
Aliyekuwa Waziri wa Ulinzi wa Marekani wakati wa utawala wa Rais George W Bush bwana Donald Henry Rumsfeld (88) alifariki dunia mwishoni mwa mwezi wa Juni nchini Marekani, na muda wa shughuli ya maziko yake na mahala ikafanywa kuwa siri kubwa ila kwa wachache katika wanafamilia.
Donald Rumsfeld aliyehudumu nafasi ya uwaziri wa ulinzi kwa maraisi wawili tofauti, wakati wa Raisi Gerald Ford 1975 – 1977, akiwa waziri wa ulinzi mwenye umri mdogo na pia alihudumu kwa nafasi hiyo hiyo kwa takriban miaka sita wakati wa raisi George W. Bush 2001 – 2006, akiongoza mikakati ya Marekani katika vita vya Iraq na Afghanistan
Rumsfeld ndiye aliyekuwa mshauri mkuu wa Rais Bush wakati wa kampeni ovu ya kupambana na Uislamu na Waislamu kwa guo la ugaidi mnamo mwaka 2001. Wakati wake aliiongoza Marekani na Washirika wake wa NATO kuivamia Afghanistan kwa madai kuwa uongozi wa Taliban wakati huo ulipinga kumsalimisha Osama bin Laden ambaye Marekani ilimtuhumu kuhusika moja kwa moja katika shambulio la Septemba 11 mwaka 2001.
Taliban ilikataa kumsalimisha kwa sababu Marekani ilishindwa kutoa ushahidi wa kutosha dhidi yake. Baadae Marekani ikaivamia Afghanistan kinguvu kwa propaganda kuwa nchi hiyo inahifadhi magaidi.
Pia ndani ya muda mfupi Rumsfeld aliutangazia ulimwengu kuwa utawala wa Iraq chini ya Rais Saddam Hussein unamiliki silaha za maangamizi ambazo zinahatarisha usalama wa eneo zima la Mashariki ya Kati na ulimwengu kwa ujumla.
Natija ya propaganda ovu dhidi ya Iraq kuwa inamiliki silaha za maangamizi iliipa uhalali Marekani kuivamia Iraq licha ya hatua hiyo kupingwa vikali na Umoja wa Mataifa chini ya Katibu Mkuu wa wakati huo bwana Kofi Annan.
Ndani ya mwaka 2003 Marekani ikaivamia Iraq kwa madai ya kusaka silaha za maangamizi, silaha ambazo mpaka leo Marekani imeshindwa kuionesha dunia.
Katika kipindi cha uvamizi wa Marekani nchini Iraq chini ya Waziri Rumsfeld kumeshuhudiwa maafa makubwa kama mauaji ya halaiki na mateso yaliyofanywa na wanajeshi wa Marekani nchini humo katika kipindi chote cha uvamizi. Bila ya kusahau uporaji wa mali kama vile dhahabu, mafuta nk.
Aidha, chini ya usimamizi wa bwana Rumsfeld kulitendeka dhulma nyingi dhidi ya Waislamu wa Iraq na Afghanistani kiasi cha yeye kushutumiwa vikali na mashirika ya kutetea haki za binadamu kama vile Amnesty International, Human Right Watch kwa kutoa idhini ya kuteswa na kudhalilishwa kwa wafungwa ndani ya Iraq katika gereza maarufu la Abu Ghuraib.
Taarifa iliyotolewa na Shirika la Habari la CBS mnamo tarehe 5/5/2004 ilisema kuwa wafungwa wengi wa kiume katika gereza la Abu Ghuraib walibakwa walilawitiwa na wengine kupigwa shoti za umeme na maafisa wa ujasusi wa Marekani ambao walipewa idhini na Idara ya Pentagon chini ya Rumsfeld kutenda unyama huo.
Tukio hilo lilizidisha fedheha kwa Marekani kote duniani na mfumo wake wa urasilimali / ubepari ambao Marekani wakati ule ilidai imekwenda kuwakomboa watu wa Iraq na Afghanistan.
Katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Aljazeera mkuu wa chuo kikuu cha Colombia na aliyewahi kuhudumu katika serikali ya Marekani bwana Jameel Jaffer alisema kuwa Rumsfeld atakumbukwa kwa kutoa amri ya kuteswa, kudhalilishwa kwa wafungwa waliokuwa wakishikiliwa kwenye gereza la Guantanamo na magereza mengine ya siri nchini Afghanistan na Iraq.
Rumsfeld amepoteza roho nyingi kwa dhulma, ameacha watoto mayatima na wajane wengi na kufilisi ndani ya Iraq na Afghanistan. Hayo ni kumbukumbu mbaya ovu inayoakisi uhalisia wa mfumo dhalimu wa kibepari ambao toka zama za ukoloni mkongwe umekuwa ndio chanzo cha kuandaa watu waovu ambao wameleta maafa katika dunia hii kama mauaji, uporaji rasilmali kwa nchi changa, na kuzifanya nchi hizo kama mashamba yao, na raia wao kama watumwa wao.
Hiyo ndio athari aliyoiacha Rumsfeld baada ya kifo chake. Ameacha makovu ya kudumu kwa watu wa Iraq na Afghanistan, ameacha mwendelezo wa mateso kwa Waislamu hasa vita dhidi ya ugaidi ambavyo vimegharimu na vinagharimu maisha ya Waislamu duniani kote na kuupaka matope Uislamu.
Kwa upande mwingine Rumsfeld ameuacha Uislamu na mwamko wake ni wenye nguvu zaidi na zaidi, huku idadi ya wanaosilimu na kuudadisi Uislamu kuongezeka.
Aidha, kifo chake kimeambatana na fedheha ya karibuni ambapo tarehe 6 Julai 2021 dola yao ya Marekani iliondoka nchini Afghanistan baada ya kupoteza rasilimali vitu na watu katika vita vilivyodumu kwa takriban miaka 20. Shirika la Al-jazeera liliripoti tukio hilo la aibu na fedheha la kuondoka wanajeshi wa Marekani kwenye kambi yao ya Bagram, kwa kuzima umeme na kuondoka kimyakimya usiku pasina taarifa.
إِنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا يُنْفِقُونَ أَمْوَالَهُمْ لِيَصُدُّوا عَنْ سَبِيلِ اللَّهِ فَسَيُنفِقُونَهَا ثُمَّ تَكُونُ عَلَيْهِمْ حَسْرَةً ثُمَّ يُغْلَبُونَ وَالَّذِينَ كَفَرُوا إِلَى جَهَنَّمَ يُحْشَرُونَ (الأنفال: 36).
“Hakika wale waliokufu hutumia mali zao ili kuzuilia njia ya Mwenyezi Mungu, basi watatumia, kisha itakuwa juu yao hasara, kisha watashindwa. Na wale waliokufuru watakusanywa kwenye Jahannam” (TMQ 10: 36)
Ust. Issa Nasibu
Risala ya Wiki No. 110
23 Dhu al-Hijjah 1442 Hijri / 02 Agosti 2021 Miladi

Maoni hayajaruhusiwa.