Tamko la Hizb ut Tahrir Tanzania Kufuatia Kuachiwa Huru Kwa Baadhi ya Watuhumiwa wa Ugaidi (Uamsho)

بسم الله الرحمن الرحيم

Ukumbi wa Hotel ya Travertine, Magomeni- Dar es Salaam
IJumaa – Juni 18, 2021
Ndugu Wanahabari,
Juzi Jumatano Juni 16, 2021 waliokuwa mahabusu wa ‘ugaidi’ wa Jumuiya ya Uamsho walianza kuachiwa huru baada ya kukaa mahabusu kwa miaka 7. Hatua hiyo ilijiri baada ya mashtaka yao kufutwa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) Sylvester Mwakitalu kwa kukosa mashiko, hivyo Afisi yake imeonelea hakuna haja ya kuendelea na kesi zao.
Ndugu Wanahabari,
Sisi Hizb ut Tahrir Tanzania tukiwa wadau ambao daima tumekuwa tukisimama kidete kupigania haki na kupinga dhulma mbali mbali ikiwemo hii dhidi ya mahabusu hata katika mazingira magumu, pia tukiwa wahanga wa dhulma hiyo kama tutakavyotaja mbele, awali ya yote tuchukue fursa hii kuwapongeza na kuwafariji mahabusu wa Uamsho walioachiwa huru kwa kuungana tena na familia zao, ndugu na marafiki. Aidha, tunatambua hatua hii muhimu ya vyombo vya kusimamia haki kuanza kusikiliza vilio vya wahanga. Pia tunawapongeza na kuwashukuru sana sana jopo la wanasheria kwa muhanga, kazi kubwa na nzito ya kuwatetea mahabusu mpaka kesi kufikia ukingoni. Bila ya kusahau kuzishukuru kwa dhati kabisa baadhi ya jumuiya za Kiislamu kama Shura ya Maimamu na viongozi wake hususan Sheikh Issa Ponda, baadhi ya vyama vya upinzani na viongozi wake, taasisi za kutetea haki za binadamu, baadhi ya masheikh, maustadh, wanaharakati na wapenda haki, baadhi ya vyombo vya habari na kila aliyesimama kidete katika qadhia hii.
Ndugu Wanahabari,
Baada ya hayo, sisi Hizb ut Tahrir Tanzania kwa qadhia ya kuachiwa huru Uamsho tunapenda kutoa tamko lifuatalo:
1. Udhaifu katika usimamizi wa haki na matumizi mabaya ya Afisi za Umma
Kufutwa kwa mashtaka haya ya ugaidi ya Uamsho na Mkurugenzi wa Mashtaka, baada ya kukosekana ushahidi thabiti kwa miaka 7 ni dalili ya wazi ya kuwepo udhaifu mkubwa katika suala la usimamizi wa haki. Japo kuwa mashtaka ya ugaidi hayana dhamana, lakini Afisi hiyo ilikuwa na mamlaka ya kuyafuta mashtaka hayo mapema kwa kukosa mashiko, lakini haikufanya hivyo, na badala yake mamlaka ya Afisi hiyo ya Umma yakatumika kwa namna inayoonesha uwepo wa dhamira na nia isiyokuwa njema.
2. Kuwepo hali ya dhulma, kupinda haki na uonevu
Baada ya Uamsho kukaa mahabusu kwa miaka 7 kwa tuhuma za ugaidi, hatima ya mashtaka hayo imetupa sura na shaka halali ya kuwepo utamaduni wa dhulma na uonevu ikiwemo kesi za kubambikiza kwa wasio na hatia kupitia mgongo wa sheria ya ugaidi, kama pia inavyolalamikiwa kwa hilo sheria ya uhujumu uchumi, na kama pia jambo hilo linavyothibitika kwa kauli ya raisi Mama Samia Suluhu karibuni kwamba amewaagiza Takukuru kufuta kesi 147 za kubambikiza. Kuna kila sababu ya kuona hata mashtaka mengine mengi ya ugaidi kando na Uamsho yamekuwa yakitumika kwa dhamira ya uonevu, dhulma, chuki nk.
3. Uhuru wa Uamsho uwe mwanzo wa kutendewa haki mahabusu wengi waliobakia.
Kufutwa mashtaka ya Uamsho ni hatua muhimu ya kutia moyo, lakini huo uwe mwanzo tu wa safari ndefu kwa taasisi za kusimamia haki kwa kwenda mbali zaidi, kwa kuwa kuna mahabusu wengi wa mashtaka kama hayo ya ugaidi, kwa mfano ndani ya Dar es Salaam pekee kabla ya kuachiwa Uamsho kulikuwa na mahabusu wa aina hiyo 140, Arusha hawapungui 60, bila ya kutaja mikoa mingine kama Tanga na ndani ya Mtwara ambako wanaharakati wetu watatu wa Hizb ut Tahrir Tanzania, Ustadh Ramadhani Moshi Kakoso , Omar Salum Bumbo na Waziri Mkaliaganda wamekuwa mahabusu kwa mashtaka kama hayo ya ‘ugaidi’ kwa karibu miaka 4 sasa. Mahabusu wote hao wanateseka katika mazingira duni kwa miaka mingi kwa mgongo wa sheria ya ugaidi, kesi zao hazisikilizwi na kila siku kisingizio wanachopewa ni kile kile maarufu cha kutokamilika ushahidi.
Katika hilo sisi Hizb ut Tahrir Tanzania tunaendelea tena kusisitiza msimamo wetu kwa taasisi za kusimamia haki kama uliokuwa katika kampeni yetu ya Juni 2020
kwamba: ‘mahabusu wote katika mikoa mbali mbali waachiwe huru, wapewe dhamana au kesi zao zisikilizwe kwa haraka’.
Katika hilo tunavitaka vyombo vyote vya kusimamia haki vijizatiti katika majukumu yao hayo kwa weledi, uaminifu na haki kama alivyosema Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) Sylvester Mwakitalu karibuni katika vyombo vya habari.
4. Kutofaa Sheria ya Ugaidi
Sheria ya ugaidi imelalamikiwa tangu kuasisiwa kwake, na hilo limeendelea kwa muda mrefu kutoka kwa Waislamu na wasiokuwa Waislamu. Sheria hii ni ya kigeni ya mabeberu, kibaguzi inayolenga kuwakamata na kuwatuhumu kundi fulani ndani ya jamii yaani Waislamu, na inapingana na misingi mingi ya haki ikiwemo kumnyima mtuhumiwa dhamana, kumnyima fidia baada ya kumuweka mahabusu kwa miaka mingi nk.
Matumizi ya sheria hiyo yanaharibu mahusiano mema ya kijamii, kwa kuwa inaleta sura ya wazi kwamba imelenga kuwaonea Waislamu. Kubwa zaidi sheria hii inatoa mwanya kwa watendaji waovu kudhulumu na kuleta uonevu na kutumika vibaya.
Katika kuepusha madhara zaidi ya sheria hiyo tunataka sheria hiyo ifutwe kabisa ili kujenga jamii yenye utengamano, mshikamano isiyo na chuki.
5. Ugaidi ni propaganda ya magharibi
Kwa kumalizia, lazima iwe wazi kwamba Uislamu sio dini ya ugaidi na wala haijawahi kuwa hivyo. Tarumbeta la vita vya ugaidi ni chuki ya madola ya magharibi dhidi ya Uislamu na Waislamu na kupaka matope Uislamu baada ya kuanguka ukomunisti, na kushindwa kuutetea mfumo wao wa ubepari kwa hoja, wakilazimisha nchi changa kijanja zishiriki katika ajenda hiyo. Aidha, ni ajenda inayotumika na madola hayo hususan Marekani kupata uhalali wa kuvamia nchi mbali mbali na kuingilia masuala yao ya ulinzi na usalama, kuharibu mahusiano baina ya raia wao, kuzuwa vurumai ili kunyonya rasilmali za nchi nk.
Sisi Hizb ut Tahrir tunaolingania Uislamu kwa njia ya mvutano wa kifikra tunatoa mwito kwa waadilifu kutoburuzwa na propaganda za magharibi kwa jina la ugaidi, bali watafiti Uislamu kupitia vyanzo vyake sahihi.
Masoud Msellem
Mwakilishi kwa Vyombo vya Habari
Hizb ut Tahrir Tanzania
0778 870609
Baadhi ya Vyombo vya Habari vilivyoripoti:
1. AQ ONLINE TV
https://youtu.be/kL3np_Xwo0s
2. MASJID MTORO ONLINE TV
https://www.youtube.com/watch?v=iO9JUxhL7IQ
3. MWANAHALISI TV
https://www.youtube.com/watch?v=Yp4sh8nk5eo

Maoni hayajaruhusiwa.