Suala La Ushahidi Katika Uislamu Ni Thabiti Na Rahisi
بسم الله الرحمن الرحيم
Mfumo wa mahakama wa Kiislamu umelipa suala la ushahidi uzito mkubwa tofauti na mifumo mingine yote ya kikafiri hususani ubepari unaotawala leo ulimwengu.
Uislamu umeweka aina nne tu za ushahidi wa kisheria ambazo ni kukiri, kula kiapo (yamiin) ushuhuda wa mtu na maandishi.
Ushahidi wa kukiri (Iqrar/confession).
Hii ni aina ya ushahidi ambapo mtu hukiri mwenyewe kuwa amefanya maasia fulani, na hivyo anahitaji adhabu ili iwe ni kafara kwake kutokamana na adhabu za akhera.
Amesimulia Zaid Bin Khalid na Abu Huraira Allah awawie radhi kuwa: alisema Mtume (s.a.w). “…nenda kwa mke wa fulani, kama atakiri basi mpigeni mawe’’.
Pia katika hadithi iliyopokewa na Abu Huraira: alikuja mtu kutoka kabila la Bani Aslam wakati Mtume SAAW akiwa msikitini akasema: ‘Ewe Mjumbe wa Allah nimefanya zinaa’
Baada ya kukiri bwana yule mara nne na kuthibitisha kwamba ana akili timamu. Mtume SAAW akaamrisha apitishiwe hukmu ya rajm (kupigwa mawe mpaka afariki )
Kukiri huku ni tofauti na kukiri katika sheria za kibepari ambapo mtu hupewa mateso na vitisho kutoka kwa askari mpaka akakiri kosa hata kama hajalifanya ili aepukane na mateso. Pia askari hutumia mwanya huu kuwabambikia kesi watu kwa chuki, rushwa, nk. na kuwalazimisha kukiri makosa na kuwatishia kama wakikana mahakamani.
Hii ni kwa sababu sheria nyingi zimetoa mwanya wa kukiri mtu akiwa polisi kuwa ni ushahidi katika mahakama licha ya kuwa mtu hupaswa kukiri au kukataa kosa mahakamani pekee. Mfano sheria ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwenendo wa Jinai (Kf.48, Sheria ya Mwenendo wa Jinai)
- Ushahidi wa kiapo (yamiin/oath)
Aina hii ya ushahidi hutumika pale ambapo mshtakiwa hatakubali kukiri makosa, hivyo hulazimika kula kiapo cha kuthibitisha uadilifu wake. Hapa tunajifunza pia Uislamu umelenga kuhifadhi hali za watu wote, yaani hata mshtakiwa hupewa nafasi kubwa ili tu asidhulumiwe, tofauti na ukafiri ambapo tuhuma hufanywa kana kwamba ndiyo makosa kamili.
Amepokea Ibu Majah katika Sunnah yake kutoka kwa Ibnu Abass kuwa anasema Mtume (s.a.w) :
“Kama watu watahukumiwa juu ya madai yao, madai ya damu na pesa, kiapo kitakuwa kwa mtuhumiwa’’
Na amepokea Ad – Daaraqutni kutoka kwa Ata kutoka kwa Abu Huraira kutoka kwa Mtume (s.a.w) kuwa; “ushahidi lazima utolewe na mlalamikaji, atakaekataa lazima atoe kiapo, isipokuwa katika kesi za Al – Qasama”
Na katika Hadith nyingine amesimulia Amr Bin Shuaib, kutoka kwa baba yake, kutoka kwa babu yake, kuwa Mtume wa Allah (s.a.w) amesema; “ushahidi lazima utolewe na mlalamikaji na akikataa mshitakiwa, basi lazima atoe kiapo isipokuwa katika Al Qasamah’’.
Aina hii ya ushahidi ipo katika Uislamu tu na hakuna mfumo wowote mwingine. Hii ni kwa sababu Uislamu umefungamanisha nidhamu zake zote na Muumba, Allah Al Hakim.
- Ushahidi wa mtu
Hapa huwa ni ushahidi wa mtu aliyeshuhudia tukio. Uislamu ukaweka uwepo wa watu zaidi ya mmoja ili kupata uhakika wa jambo. Anasema Allah kuwa:
وَاسْتَشْهِدُوا شَهِيدَيْنِ مِنْ رِجَالِكُمْ فَإِنْ لَمْ يَكُونَا رَجُلَيْنِ فَرَجُلٌ وَامْرَأَتَانِ مِمَّنْ تَرْضَوْنَ مِنْ الشُّهَدَاءِ
“Na washuhudie wanaume wawili katika watu wenu (kama mashahidi), kama hakuna wanaume wawili, basi leteni mwanaume mmoja na wanawake wawili miongoni mwa mnaowaridhia katika mashahidi’
(TMQ Al –Baqarah: 282)
Na pia Uislamu ukatilia mkazo kuhusu mashahidi hao kuwa ni lazima wawe ni waadilifu. Hii ni tofauti kabisa na sheria za kidemokrasia ambapo mtu yeyote anaweza kuwa shahidi, na hakuna idadi iliyowekwa ya mashahidi.
Sheria ya Ushahidi namba 9 ya 2016 ya Zanzibar (Sheria ya Ushahidi) iliyoanza kufanya kazi rasmi mnamo tarehe 18 Januari 2017 ni mfano mzuri katika hili.
Ushahidi wa maandishi
Amesema Allah;
وَلاَ تَسْأَمُوا أَنْ تَكْتُبُوهُ صَغِيرًا أَوْ كَبِيرًا إِلَى أَجَلِهِ ذَلِكُمْ أَقْسَطُ عِنْدَ اللَّهِ وَأَقْوَمُ لِلشَّهَادَةِ وَأَدْنَى أَلاَّ تَرْتَابُوا إِلاَّ أَنْ تَكُونَ تِجَارَةً حَاضِرَةً تُدِيرُونَهَا بَيْنَكُمْ فَلَيْسَ عَلَيْكُمْ جُنَاحٌ أَلاَّ تَكْتُبُوهَا وَأَشْهِدُوا إِذَا تَبَايَعْتُمْ وَلاَ يُضَارَّ
“Wala msipuuzie kuandika, liwe dogo au kikubwa katika makubaliano, hilo ni bora mbele ya Allah na ushahidi wenye nguvu katika kuondoa mashaka kati yenu, isipokuwa katika mapatano ya haraka (ya kawaida) baina yenu, katika hayo hakuna lawama kwenu kama msipoandikishana”
(TMQ Al Baqarah: 282).
Tunaona mpaka hapo jinsi suala la ushahidi lilivyo nyeti katika Uislamu, amma katika ukafiri na demokrasia yake ushahidi si kitu muhimu kwani mtu yeyote hata ambaye ni mrongo huweza kutoa ushahidi, na hata hivyo mfumo wa kimahakama huwa si huru kutoa maamuzi sahihi.
Mfano mzuri tunaona kila mwaka kuwa licha ya kuwa ushahidi umetolewa na watu wamehukumiwa na mahakama lakini maraisi na viongozi mbalimbali wakuu wa nchi huweza kuwaachia huru wahalifu kwa jina la msamaha. Hufanyika haya nchini Tanzania hususan katika maadhimisho ya siku ya “uhuru” nchini Kenya na nchi tofauti tofauti.
Said Bitomwa
Risala ya Wiki No. 81
22 Dhu al-Qi’dah 1441 / 13 Julai 2020 Miladi
https://hizb.or.tz/
https://www.facebook.com/Hizb-ut-Tahrir
#KomeshaUkandamizajiWaKisheriaNaUtekaji
#StopOppressiveLawsAndAbduction
Maoni hayajaruhusiwa.