Siku Aliyolia Mtume (Rehma na Amani Zimshukie)

Kutoka kwa Ibn Masoud (ra) amesema: Mtume Rehema na Amani za Mwenyezi Mungu zimshukie aliniambia: “Hebu nisomee Quran”. Nikamwambia: ‘Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu nikusomee na kwako ndio imeteremshwa? Akasema Mtume (saw): “Hakika mimi napenda niisikie kwa mtu mwengine”.

Ibn Masoud Akasema; Nikamsomea surat Nisai hadi kufikia aya hii:

فَكَيْفَ إِذَا جِئْنَا مِن كُلِّ أُمَّةٍ بِشَهِيدٍ وَجِئْنَا بِكَ عَلَىٰ هَٰؤُلاۤءِ شَهِيداً

Basi itakuwaje tutakapoleta shahidi katika kila umma na tutakuleta wewe (Nabii Muhammad) uwe shahidi juu ya huu umma wako. [An-Nisaa: 41]

Hapa Mtume (saw) akamwambia Ibn Masoud: “Tosha” Mara nikimgeukia nikaona akitiririkwa na machozi usoni mwake.

Kikawaida kwa mwenye kuisoma Quran na kuzingatia maana yake basi moyo wake hulainika kwa kujawa na Khofu ya Mola wake. Kitendo cha Mtume (saw) kumtaka swahaba wake Ibn Masoud (ra) amsomee Quran, kinaelezewa na wanavyuoni kwamba wakati mwengine Quran humuathiri mtu zaidi pale anapo isikiliza kwa mwenzake. Twaona jinsi gani Mtume (saw) alivyo shindwa kuhimili kilio alipo isikiliza aya hii ishara ya kuwa Quran sio kitabu tu cha kusomwa tu bali inatakikana kuwe na athari na mazingatio makubwa kila tunapo isoma.

Katika fitina kubwa wamagharibi waliofaulu  kufitini Waislamu ni kuondosha ndani ya mabongo yao ufahamu halisi wa Quran. Huyu hapa waziri wa zamani wa Uingereza Disrael akisema kwamba;

Njia pekee ya kuwamaliza Waislamu ni kutoa ufahamu wa Kitabu hiki (Quran) ndani ya mabongo yao.

Kwa kifupi akiashiria kuwa mafunzo yaliyomo ndani ya Quran yachukuliwe kama nadharia na falsafa tu zisizowezekana katika maisha ya kila siku. Na naam hapa ndio tumefikia, misikiti imejaa tele misahafu huku watu wakiweka halaka za tafsiri ambazo huishia kuambizana tu pasina kufanyia kazi.

Ni muhimu kuzingatia kilio cha bwana Mtume (saw) hasa kwenye maana ya aya hiyo ya Surat An- Nisai. Bila shaka aya inataja siku nzito ya Qiyama ambayo miongoni mwa hali zake ngumu ni kama ilivyo tajwa kwenye aya iliofuata baadaa ya hiyo iliomliza bwana Mtume (saw) yaani ya nambari 42 Mola akisema:

يَوْمَئِذٍ يَوَدُّ ٱلَّذِينَ كَفَرُواْ وَعَصَوُاْ ٱلرَّسُولَ لَوْ تُسَوَّىٰ بِهِمُ ٱلأَرْضُ وَلاَ يَكْتُمُونَ ٱلَّلَ حَدِيثاً

Siku hiyo walio kufuru na wakamuasi Mtume watatamani ardhi isawazishwe juu yao. Wala hawataweza kumficha Mwenyezi Mungu neno lolote. [An-Nisaa: 42]

Tukiachilia mbali huruma ya Mtume (saw) kwa umma wake twaweza tukasema kilichompelekea kuangua kilio ni ushuhuda wake mbele ya Mwenyezi Mungu (swt) kwa Ummah wake na uliotangulia. Na hii ni kama ilivyo pokewa kuwa siku ya Qiyama Kila nabii atakuja akiwa na mtu mmoja na nabii mwengine awe na watu wawili bali na Zaidi ya hao. Watu wake waitwe mbele yake waulizwe: ‘Je, huyu nabii wenu aliwafikishia ujumbe?’ Watu waseme, ‘La’. Kisha yule nabii aulizwe: ‘Je, uliwafikishia ujumbe hawa watu?’ Nabii aseme; ‘Ndio’. Kisha aambiwe, ‘ni nani shahidi wako?’ aseme, ‘Muhammad na Umma wake’. Mtume (saw) na Umma wake waulizwe: ‘Je, aliwafikishia nabii huyu watu wake ujumbe?’ Waseme: ‘Ndio’. Kisha uulizwe, ‘nyinyi mlijuaje?’ Waseme: ‘Alitujiliia Mtume (saw) akatueleza kwamba mitume iliwafikishia watu wao ujumbe’.

Tukitaamali zaidi tutakuta maswali msingi hapa: – Je, kweli Mtume (saw) alifikisha Uislamu kama mfumo kamili kwa umma wake? Jawabu ya haraka na iso na shaka ni; ndiyo, Sasa swali ni Je, sisi Waislamu kweli tumeuchukua Uislamu kimfumo kamili na kama nuru aliyo kuja nayo (saw) ama tumetabani mfumo mwengine uso na mashiko na wahyi wa Mwenyezi Mungu (swt). Jawabu ni kuwa  Waislamu leo hatuko chini ya Nuru

aliyo kuja nayo Mtume wetu (saw). Siasa zetu, uchumi na nidhamu ya kijamii zote hizo tunazipeleka kwa  mujibu wa ukafiri wa Kirasilimali.

Wengi wetu tumeingizwa khofu  tukiogopa lawama ya wasemao  kuwa Uislamu ni mfumo muovu bali  usojimudu karne hii! Bali la kutia  uchungu zaidi ni kuwakatisha tamaa  wachache miongoni mwetu na  kuwakejeli kila wanao kumbwa na  vitimbi vya madhalimu kwenye kazi  tukufu ya kuukomboa ulimwengu  upya kupitia kusimamisha Uislamu  ndani ya serikali yake ya Khilafah.  Je, hali itakuwaje siku hiyo ikiwa hivi sasa Uislamu tumeugeuza juu chini?

Na hapa ni tujitambue sisi kama  Waislamu kuwa mbele yetu ipo kazi  ya kushikamana na Uislamu kama  alivyo tuachia Mtume wetu (saw).  Tuzingatie kuwa kama atakavyo

kuwa shahidi Mtume wetu (saw) pia  nasi ni mashahidi kwa watu wengine.  Na hii ni kama Mwenyezi Mungu  (swt) alivyosema:

وَكَذَلِكَ جَعَلْنَاكُمْ أُمَّةً وَسَطاً لِّتَكُونُواْ شُهَدَآءَ عَلَى ٱلنَّاسِ وَيَكُونَ ٱلرَّسُولُ عَلَيْكُمْ شَهِيداً

Na vivyo hivyo tumekufanyeni muwe Umma wa wasitani (adilifu),  ili muwe mashahidi juu ya watu,  na Mtume awe ni shahidi juu yenu.

[Al-Baqarah: 143]

Kwenye ayah ni kwamba sisi ndio Umma bora kwani tupo kwenye mfumo wa kweli na wenye uadilifu na ndio maana sisi ni mashahidi kwa Umma nyengine kwa sababu tuko

kwenye uadilifu. Na kama inavyo julikana katika sharuti za ushuhuda huwa ni uadilifu. Kwa namna hii  basi bila shaka tumekalifishwa na  MwenyeziMungu (swt) kuwafikishia  watu suluhisho ya matatizo yao  yote yakiwemo ya kisiasa, uchumi  na kijamii. Tusipo fanya hivyo  tutakuwa tumehatarisha maisha  yetu hapa duniani na kesho Mtume (saw) ataeleza bayana kuwa sisi  tulikengeuka ujumbe wake tukaishi  kinyume na Uislamu aliokuja nao yeye (saw).

Shabani Mwalimu

Mwakilishi kwa Vyombo vya Habari

Hizb ut Tahrir Kenya

Inatoka Jarida la Uqab: 13

https://hizb.or.tz/2018/02/01/uqab-13/

Maoni hayajaruhusiwa.