Sheikh Othman Matata Nae Arejea Kwa Mola Wake
بسم الله الرحمن الرحيم
Kwa huzuni na masikitiko makubwa tumepokea taarifa ya kufariki dunia Sheikh Othman Matata. Marehemu ni mhadhiri bingwa katika mada za ‘Mlingano wa dini, mchambuzi mkubwa wa Sayansi ya Quran na mtaalamu wa fasihi ya Kingereza, ambapo umashuhuri wake sio Tanzania pekee, bali ni wenye kuenea.
Kifo cha Sheikh Matata kilichotokea usiku wa kuamkia leo ni pigo na pengo jengine kubwa mno katika uwanja wa elimu ya Kiislamu na da’awa, sio tu Tanzania, bali Afrika Mashariki na ulimwengu mzima wa Kiislamu, kwa kuwa marehemu alikuwa miongoni mwa wahadhiri wakubwa, muhodari, mfasaha na mwenye uwezo mkubwa wa kujenga hoja, khasa kwa wale wenye kujaribu kutilia mashaka Quran Tukufu.
Marehemu amewahi kuwa katika jopo wa wahadhiri wakongwe nchini toka kipindi cha akina Ngariba na Kawemba, wakiongozwa na Almarhum Sheikh Qassim bin Juma kwenye mihadhara ya viwanja vya Mnazi Mmoja Dar es Salaam na nchi nzima, pia kusafiri nje ya nchi, kazi ambayo imeleta matunda makubwa ya watu kusilimu, na Waislamu kujenga thika /kujiamini na Uislamu wao kwa dalili na hoja.
Mazishi ya sheikh Matata yatakua nyumbani kwake Kawe, mukabala na iliyokua Tanganyika Packers zamani, nyumba yake ikiwa imeambatana na msikiti.
Hizb ut Tahrir Tanzania inatoa mkono wa Ta’azia kwa Umoja wa Wahadhiri Tanzania khaswa, Waislamu wote amma, familia, masheikh, maustadh, walimu nk. kwa msiba wa kuondokea na muhimili mwengine muhimu katika Uislamu.
Tunamuomba Allah Taala Amsamehe marehemu, Amrehemu na kumuingiza katika Jannat Firdaus.
اللهم اغفر له وارحمه واسكنه في الجنة وعافه واعف عنه وأكرم نزله ووسع مدخله واغسله بالماء والثلج والبرد ونقه من الذنوب والخطايا كما ينقى الثوب الأبيض من الدنس
Aidha, Tunamuomba Allah Taala awalipe malipo makubwa wafiwa na kuwamakinisha kwa subra na istiqama katika kipindi hiki kizito cha Msiba. Amiin
Tunakumbusha kuwa alama kubwa aliyoacha marehemu ni kuulingania Uislamu, jambo ambalo hatuna budi kushikamana nalo Waislamu sote, kwa kuwa ni faradhi, iwe kwa Masheikh, maustadh, wahadhiri nk. Tulinganieni Uislamu kwa njia ya Mtume wetu (s. a. w) isiyohusisha nguvu wala mabavu ili kurejesha tena maisha ya Kiislamu na kufikia wanaadamu wote ulimwenguni waongozwe na Mwongozo wa Allah Taala
Innallillah wainnailahi raajiuun
Sheikh Mussa Kileo
Mwenyekiti Kamati ya Mawasiliano Hizb ut Tahrir Tanzania
15 Ramadhan 1441 Hijri – 08 Mei 2020 M
Maoni hayajaruhusiwa.