Ramadhan Inabisha Hodi: Waislamu Bado Hawana Mlinzi na Ngao Yao!

بسم الله الرحمن الرحيم

Waislamu hivi sasa duniani kote wamo ndani ya mwezi wa Shaaban 1440H katika maandalizi ya kuukaribisha mwezi ufuatao uliojaa baraka na kheri nyingi wa Ramadhan 1440H. Mwezi ambao ndani yake imeshukishwa Qur’an kuja kuwakomboa wanadamu kutoka katika kiza cha ukafiri wa kuabudu viumbe mpaka katika nuru ya kuabudu Muumba wa viumbe. Waislamu na wasiokuwa Waislamu tokea kuasisiwa kwa Dola ya Kiislamu ndani ya Mji wa Madina chini ya kiongozi wa kwanza Mtume (saw) walifurahia amani, utulivu, maendeleo na ustawi wa kweli chini ya uongozi wake (saw) na uongozi wa Makhalifa waliotawala baada yeye (saw) kufariki dunia.

Wanadamu walihifadhiwa damu zao, mali zao na heshima zao kwa kuishi chini ya Dola ya Kiislamu. Lakini hali hiyo haikuwafurahisha Wamagharibi wakoloni ambao walikuwa na chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu. Hivyo basi wakapanga njama na kuhakikisha wanafaulu kuivunja Dola ya Kiislamu ambayo ndiyo kiunganishi cha Waislamu wote duniani. Mnamo 28 Rajab 1342H sawa na 3 Machi 1924M walifaulu rasmi kuivunjilia mbali Dola hiyo ya Khilafah kupitia mikono ya vibaraka wa Kimagharibi wakiongozwa na Myahudi Mustafa Kamal!

Dola ya Kiislamu ya Khilafah ilivunjiliwa mbali na kugawanywa kuwa vijidola 54 vilivyo chini ya mipaka iliyochorwa na wakoloni Wamagharibi wakiongozwa na dola kuu enzi hizo Uingereza na Ufaransa na Marekani hivi sasa. Vijidola hivyo vilikabidhiwa kama ngawira watawala vibaraka wajinga ambao kibla chao ni Washington, London na Paris! Watawala vibaraka madhalimu walio tayari kutekeleza lolote katika maagizo wanayopewa na mabwana zao mabepari. Wanatekeleza mfumo batili wa kisekula wa kirasilimali na nidhamu zake zinazonuka ikiwemo demokrasia n.k. Wanakwenda mbio usiku na mchana kuweka vikwazo dhidi ya kurudisha tena Maisha ya Kiislamu kupitia kusimamisha tena Serikali ya Kiislamu ya Khilafah!

Tangu wakati huo Uislamu na Waislamu wamebakia kuwa yatima wasiokuwa na mlinzi na ngao! Damu zao zikimwagwa ovyo, mali zao zikiporwa na wao kuwachwa na umasikini wa kupindukia, heshima na matukufu yao yakikejeliwa kwa mikono ya wakoloni kwa ushirikiano wa vibaraka wao ulimwenguni kote! Waislamu wamelazimishwa kubeba chapa ya Uislamu ambao unawiana na mfumo muovu wa kisekula wa kirasilimali maarufu Uislamu Poa. Uislamu huu unapigiwa debe ulimwenguni kote na dola kuu zikiongozwa na Marekani na washirika wake. Kwani Uislamu Poa unaruhusu Muislamu kubeba fikra za kimagharibi mfano kula riba, kuwa shoga au msagaji, mzinifu, kupiga kura kumpa nguvu mwanadamu kutunga sheria kinyume na za Mwenyezi Mungu (swt) –kupiga marufuku Shari’ah (Qur’an na Sunnah). Upande mwingine wakipiga vita Uislamu na Waislamu wanaokwenda kinyume na mfumo wao batili kwa kuwabandika eti ni Uislamu wa Siasa Kali, Ugaidi, Magaidi, Misimamo Mikali n.k. Kwa visingizio hivyo tunaendelea kushuhudia hadi hivi sasa Waislamu wakishambuliwa mfano Waislamu wa Uyghur walioko Mashariki ya Turkistan (Xinjiang) nchini Uchina wamejazwa katika makambi eti kusafishwa upya mabongo yao ili yaondokane na fikra za kigaidi, itikadi kali na kujitenga! Waislamu wa Rohingya kutoka Burma wameuliwa maelfu kwa tuhuma za kigaidi na misimamo mikali! Miji na Ardhi za Waislamu zikivamiwa na kutekwa mfano Palestina kibla chetu cha kwanza! Hali ni hiyo hiyo Kashmir, Somalia, Afghanistan, Iraq, Syria, Uzbekistan, Tajikistan, Crimea, Yemen n.k.

Hali hiyo imepelekea Waislamu kuishi kwa hofu wasijue kesho wataamkia lipi jipya! Hakika katika hali hiyo ngumu Waislamu kila kukicha wanaendelea kuona muozo na maangamivu chini ya kivuli cha mfumo muovu wa kisekula wa kirasilimali na dola zinazoupigia debe. Alhamdulillah, Waislamu wanaendelea kuzinduka na kupaza sauti zao wakidai mageuzi kutokana na kukosa pumzi kwa ukandamizaji wa kisiasa, kiuchumi, kijamii na kielimu ambao unaendelea kuwasambaratisha kila siku zinavyo songa!

Wakati umewadia kwa ndugu zetu wanajeshi mukhlisina waliojaa katika kambi za kijeshi ndani ya Biladi za Waislamu mfano Pakistan, Algeria, Tunisia, Misri, Jordan n.k watoe Nusrah (nguvu za kijeshi) kwa ndugu zao wa Hizb ut Tahrir ili kuweza kutimiza hatua ya kuchukua mamlaka na kurudisha tena Maisha ya Kiislamu kwa kusimamisha Serikali ya Kiislamu ya Khilafah kwa njia ya Utume.  Kwani chini ya Khilafah ndio Waislamu wataunganishwa tena kuwa Ummah Mmoja chini ya Dola Moja inayohukumu kwa Shari’ah Moja kwa usimamizi wa Kiongozi Mmoja, Khalifah mchamungu anayekwenda mbio kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu (swt) kinyume na watawala vibaraka wanaokwenda mbio kutafuta radhi za mabwana zao wakoloni waliowaweka madarakani!

Twamuomba Mwenyezi Mungu (swt) ailainishe mioyo ya ndugu zetu wanajeshi mukhlisina katika biladi za Waislamu kwa kuwango’a mamlakani watawala vibaraka na badala yake kuunga mkono kundi la Mwenyezi Mungu (swt): إِنَّ حِزۡبَ ٱللَّهِ هُمُ ٱلۡمُفۡلِحُونَ))Hakika kundi la Mwenyezi Mungu ndilo lenye kufanikiwa.” [Al-Mujadila 58: 22] Kupitia mikono yao iliyo na baraka za Muumba wao, tupate zawadi ya kuishi chini ya Khilafah kwa njia ya Utume ndani ya Mwezi ujao wa Ramadhan 1440H! Tufanye ibada zetu n.k tukiwa chini ya Ulinzi na Ngao madhubuti ya Khilafah kwa njia ya Utume! وَيَوْمَئِذٍ يَفْرَحُ الْمُؤْمِنُونَ)) “Na siku hiyo Waumini watafurahi.” [Ar-Rum 30: 4]

Ali Nassoro Ali

Mwanachama wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Kenya

Inatokwa: http://hizb.or.ke/sw/2019/04/12/ramadhan-inabisha-hodi-waislamu-bado-hawana-mlinzi-na-ngao-yao/

Maoni hayajaruhusiwa.