Poleni wa Mtwara kwa Mapigo ya Radi
Taarifa zinasema kuwa jana (Jumanne) mwanafunzi Abdul Athumani Masamba (19) wa Shule ya Sekondari Mikindani, Mtwara amefariki papo hapo baada ya kupigwa na radi, na wanafunzi wengine zaidi ya 30 wamejeruhiwa na kukimbizwa kwenye hospitali ya rufaa ya Ligula mkoani Mtwara kwa matibabu.
Tunachukua fursa hii kwa dhati kuwapa pole ndugu zetu wa Mtwara kwa msiba huu mkubwa wa kufariki dunia kijana Abdul Athumani Masamba. Allah Taala ampokee katika waja wake wema wa pepo ya darja ya juu na pia tunawafariji waliopata majeraha kufuatia qadhaa hii ya Muumba, warejeshewe siha na afya zao ili waendelee na maisha yao. Amiin.
Kiujumla (general rule) tukio la mapigo ya radi ni miongoni mwa matukio ya majaaliwa ya Mwenyezi Mungu, yaani ni matukio ya Qadhaa yaliyo nje ya uwezo wa matendo ya mwanadamu, ambapo mwanadamu hua hana mamlaka ya kuzuiya wala kuathiri kutokea kwake. Muislamu linapotokea tukio kama hilo, amma kumsibu hupaswa kunyenyekea kwa Muumba, kwa kuwa liko nje ya uwezo wa kibinadamu.
وَيُسَبِّحُ الرَّعْدُ بِحَمْدِهِ وَالْمَلاَئِكَةُ مِنْ خِيفَتِهِ وَيُرْسِلُ الصَّوَاعِقَ فَيُصِيبُ بِهَا مَنْ يَشَاءُ (الرعد: 13
“Na radi inamtakasa Mwenyezi Mungu kwa kumuhimidi, na Malaika (wanafanya hivyo hivyo) kwa kumukhofu Yeye (Mwenyezi Mungu). Naye hupeleka mapigo ya radi yakampata amtakaye……” (Ar-Raad : 13)
Hata hivyo, ufahamu wa qadhaa uliomo katika aqiida ya Kiislamu kamwe hautuzuii kutafiti mazingira ya matendo ya mwanadamu katika mchakato wa kukinga na kukabiliana na matokeo ya mapigo ya radi kwa kiwango cha kibinadamu.
Kwa mfano, ikiwa tukio la mapigo ya radi lilitokea katika mazingira ambayo hatua thabiti za tahadhari hazikuchukuliwa, hapo inapaswa kuhojiwa, hatuhoji mapigo ya radi kutokea, tunahoji hatua za hadhari ya kibinadamu ambazo zilipaswa zichukuliwe , na kimsingi kama jambo hilo limepangwa kutokea hata hadhari iwe ya kiasi gani bado litatokea. Lakini Uislamu bado unatutaka upande wa kibinadamu katika hali yoyote kuchukuwa hadhari kadiri ya uwezo wetu. Hilo lipo katika mamlaka yetu, na lau hatukufanya tunakuwa mas’ul mbele ya Allah Taala.
Aidha, na kwa upande wa kukabiliana na tukio baada ya kutokea, ikiwemo huduma kwa majeruhi baada ya ajali, hili lipo katika mamlaka ya mzunguuko wa kibinadamu na inapaswa kujipanga na kuwawajibisha ambao huzembea kwa hilo.
Matukio ya qadhaa, ambayo yako nje ya uwezo na mamlaka yetu yataendelea kutokea, kwa kuwa kuna Muumba ambaye ni wa milele na hufanya alitakalo kwa viumbe vyake. Hata hivyo, uwepo wake kamwe isiwe farasi wa kisingizio cha kufichia uzembe na kukosekana uwajibikaji katika mipango, uratibu na mikakati ya mambo katika maisha yetu.
Lazima ufahamu wa qadhaa uwe wazi, kuwa uko kando na matendo yetu. Tutende yaliyo katika himaya yetu kwa kadiri ya uwezo, vipaji na mikakati yetu, halafu ikija qadhaa ya Muumba tunyekee kwa Muumba wetu.
Tunawapa tena mkono wa pole ndugu zetu wa Mtwara kwa msiba huu.
Inna lllilahi wainna ilayhi rajiuun
06 Machi 2019
Masoud Msellem
Maoni hayajaruhusiwa.