Mwaka Mpya wa Kiislamu Utuhamasishe Zaidi kubeba Majukumu Yetu
Kwa ikhlasi tunaupongeza Umma mtukufu wa Kiislamu kwa kuingia mwaka mpya wa Kiislamu 1440 Hijria. Licha ya kuingia ndani ya mwaka mpya, kwa masikitiko makubwa hali ya maumivu na machungu kwa Ummah wetu mtukufu bado iko vile vile, kama si kuzidi kamwe.
Ummah wetu unabubujika mito ya damu ndani ya Yemen, Burma, Afghanistan, Palestina, Somalia, Syria nk. Ambapo kwa hivi sasa, ndani ya Syria mjini Idlib kunaendelea mauaji ya kinyama na kikatili. Hayo yanajiri kwa khiyana ya Uturuki na Iran kwa kushirikiana na Urusi. Wakati maangamizi hayo yakiendelea, kama inavyotarajiwa, watawala wa nchi za Waislamu wako kimyaa bila ya hatua yoyote thabiti kuyazuiya.
Suala la kuanza mwaka mpya wa Kiislamu lazima lifungamanishwe na wajibu wetu na kuendelea kubeba majukumu yetu ipasavyo, kama yafuatayo:
- Kuyatumia Vyema maisha ya kidunia: Uislamu ukiwa ni mfumo kamili na fafanuzi haukupuuza maisha ya dunia, bali umeweka taratibu maalumu kuamilina nayo. Kuanza mwaka mpya, ni muda muwafaka kwetu kujipanga, kuchukua hatua za kiutendaji na kukabiliana na changamoto kwa namna ya kuboresha hali kulinganisha na mwaka uliotangulia. Daima mwerevu huifanya hali yake ya leo bora zaidi, kuliko siku iliyopita.
- Kujiandaa na maisha yajayo ya Akhera : Kuanza mwaka mpya maana yake Allah Taala kwa Rehma zake katutunuku neema ya umri kuendelea kuwepo katika ulimwengu huu. Kwa hivyo, ni wajibu kuutumia vyema umri huu mfupi wa kupita, kwa kushikamana na maamrisho Yake (SW) na kujitenga kando na makatazo Yake ili kumridhisha Yeye, tukitaraji Pepo Yake. Ni wajibu pia kujizatiti kuitumia vyema neema ya umri mpaka mwisho wa pumzi zetu, kwa kuwa muda ukipita haurudi tena .
- Ubebaji wa Ulinganizi wa Uislamu: Masahaba katika zama za Khilafah ya Umar bin Khatwab, mwaka wa 16 Hijria kwa umoja, wote waliwafikiana (ijmaa) kulichagua tukio la Hijra kuwa ndio mwanzo wa kuhesabu mwaka wa mwanzo wa Kiislamu, licha ya kuwepo matukio mbalimbali muhimu na matukufu katika tareekh ya Kiislamu. Hii ni kwa sababu Hijra ni tukio la kipekee, lililouhamisha Uislamu kutoka hatua ya kinadharia kuupeleka katika hatua ya usimamizi na kiutekelezaji kwa kuasisiwa dola ya mwanzo ya Kiislamu ndani ya Madina. Dola hiyo ilitawala kwa makarne kwa mafanikio makubwa mpaka ilipoangushwa mwaka 1924 kwa mkono wa Uingereza, Washirika wake, na kwa msaada wa vibaraka miongoni mwa Waturuki na Waarabu.
Ijmaa ya masahaba katika uteuzi wa tukio la Hijra kama ndio mwanzo wa kuhesabu ya kalenda ya Kiislamu inatuonesha wazi wazi kwamba ukombozi kamili wa Ummah wetu utapatikana kwa kuwepo dola ya Kiislamu. Kuanza mwaka mpya wa Kiislamu kuuhamasishe zaidi Ummah wetu juu ya jukumu tukufu na qadhia nyeti ya kurejesha tena dola ya Khilafah. Dola inayopaswa kuanzia katika nchi kubwa za Waislamu, kisha kueneza uongofu, nuru na uadilifu wake kwa wanadamu wote, bila ya kuzingatia asili zao, rangi zao, dini zao wala makabila yao. Allah Taala Anasema :
﴿يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اسْتَجِيبُوا لِلَّهِ وَلِلرَّسُولِ إِذَا دَعَاكُمْ لِمَا يُحْيِيكُمْ﴾
“Enyi Mlioamini, muitikieni Allah na Mtume wake wanapokuiteni katika mambo yanayokupeni uhai .”
Masoud Msellem
Mwakilishi kwa Vyombo vya Habari
Hizb ut Tahrir Tanzania
Maoni hayajaruhusiwa.