Miaka 95 ya Kiza Kinene Kinachosubiri Mwangaza Wa Khilafah
Tarehe 3 Machi,1924 sawa na 28 Rajab 1342 Hijiria, Dola ya Kiislamu (Khilafah) ilivunjwa huko Istanbul, Uturuki. Tukio hili lilitimiza ndoto mbovu ya wakoloni wakimagharibi ya kuiangusha Khilafah. Kwa kuiangusha serikali hii mkoloni Mwingereza Dola Kuu (Super Power) zama hizo alitaka Waislamu wasibakie tena na umoja wao waliokuwa nao kwa karne kumi na tatu. Umoja uliokuwa imara tena chini ya kiongozi (Khalifah) akitabikisha sheria ya Muumba wao Allah (swt). Haya hapa maneno ya aliyekuwa waziri mkuu wa Uingereza akasimulia tendo lao ovu la kuiangusha Khilafah: ‘We must put an end to anything which brings about any Islamic unity between the sons of the Muslims. The situation now is that Turkey is dead and will never rise again, because we have destroyed its moral strength, the Caliphate and Islam”. (Lazima tumalize kabisa chochote kile kiletacho umoja wa Kiislamu miongoni mwa Waislamu. Hali halisi sasa ni kuwa Uturuki imekwisha kufa na kattu haitorudi kusimama tena kwa sababu tumevunja nguvu/nishati yake ya kiimaadili nayo ni Khilafah na Uislamu.’
Baada ya kutumia vita dhidi ya Dola ya Kiislamu kama ilivyodhihirika tokea Mtume (saw) kuanzisha Dola yake Madina, makafiri walizua kila mbinu katika kuhakikisha kuwa Uislamu unabakia pasina na serikali. Licha ya Waislamu kuwa imara kwenye itikadi yao jambo lililowafanya wawashinde maadui zao lakini Wakoloni hawakukata tamaa ya kuvunja Khilafah. Wakaanza kuishambulia itikadi ya Kiislamu ambayo ndio uti wa mgongo wa Uislamu na nishati kubwa ya Waislamu katika kuwapa uhai na dira yao maishani. Wakapenyeza fikra za kizalendo, kitaifa, kikabila ndani ya Waislamu. Wakaja na njama nyengine nayo ni kuuchafua Uislamu na fikra zake hasa pale Waislamu wenyewe wakaanza kuitenganisha lugha ya Kiarabu ambayo ndiyo lugha iliyoteremshiwa kwayo Sheria za Kiislamu. Hali hii ikawafanya Waislamu wanakosa ufahamu safi wa Uislamu hivyo kupelekea kukumbatia hadhara ya Kimagharibi matata. Hapo ndipo Waislamu wakaanza kulemaa kiitikadi na kuwa rahisi Wakoloni kupata vibaraka ndani ya Ummah wa Kiislamu kama vile Mustafa Kamal Ata Turkiy aliyefaulisha uovu wa kuvunjwa Dola ya Mwisho ya Kiislamu 1924!
Maana ya kuvunjika kwa Dola hii ni Waislamu kutohukumu na sheria za MwenyeziMungu (swt) badali yake wahukumiwe na kanuni za kitwaghut. Waislamu wagawanyike katika serikali za kikatuni zilizozochorwa na Wamagharibi na kupachikwa juu yake viongozi makhaini ambao ni wafu wanaojihesabu kuwa wako hai! Utajiri ulioko katika biladi za Kiislamu ukawa unaporwa na wamagharibi kwa niaba ya vibaraka hao. Umma ukabakia hauna hadhara ila hadhara ya kimagharibi wala hauna siasa ila ya kimagharibi. Naam, hivi ndivyo Ummah ulipofikishwa. Kutia msumari moto damu tukufu za Waislamu zimegeuzwa kuwa damu za kunguni zinazomwagwa pasina huruma. Vilio, majonzi katika miji ya Kiislamu kuanzia Burma, Iraq, Afghanistan, Somalia, Yemen, Syria, Palestine n.k.
Miaka 93 Umma hauna kiongozi! Ummah umekuwa ukidhilalika mbele ya maadui wa MwenyeziMungu (swt) na Mtume wake na Waumini. Je tuendelee kunukuu na kushuhudia maafa juu ya maafa? Je hatujaona jinsi mfumo wa kirasilimali unakurubia kutangaziwa mazishi yake kwani ulifariki kitambo? Jamii ya Kiislamu inapaswa kutambua ufaradhi wa Kuisimamisha Khilafah. Naam, Khilafah sio ndoto wala mawazo ya kuwaza bali ni faradhi kwa Mola wetu ambayo kwayo nguvu na utukufu hupatikana. Ambayo kwa Waislamu hupata hifadhi. Kwayo Waislamu huweza kuhukumu na sheria za Muumba wao.
Wamagharibi waliangusha Khilafah na sasa Ummah umezaa wanaume wanaoitaja Khilafah na kuilingania kwa hali na mali. Leo Ummah kote duniani unaanza kuitamka na kuitaka. Dalili ya haya ni kuwa Wamagharibi wameanza kuichafua Khilafah kabla ya kusimama kwake. Vinatoka vipote vinavyodai Khilafah na kuangaziwa dunia nzima ilhali wanachofanya ni kinyume na Khilafah. Kwa upande wa pili wanaolingania Khilafah ya kikweli kwa usafi wake tena pasina na kubeba silaha hawaangaziwi na ikizidi wanapachikwa majina ya kutamausha ikiwemo eti ni Magaidi au Watu wenye Misimamo Mikali! Twasema Khilafah ni dola iliyoleta amani na utulivu kwa Waislamu na wasiokuwa Waislamu leo yapakwa matope kuonyeshwa kuwa ni adui wa amani na usalama. Khilafah iliotingisha maadui mtingishiko mkubwa. Lakustajaabisha leo wanayoidai hawajatupa hata kombora moja kuinusuru Palestina dhidi ya mayahudi.
Naam, Waliivunja lakini Khilafah inakuja kwa mwendo wa kasi usiozuilika tena. Khilafah itakayo rejesha tena haiba na kuhifadhi hadhi, heshima, mali na matukufu ya Waislamu popote walipo ulimwenguni kwa kuwanusuru dhidi ya kila fedheha na idhilali wanayofanyiwa.
Khilafah inakuja kung’oa mfumo batili wa kibepari unaoangamiza vizazi na mimea. Khilafah inakuja kuwawezesha Waislamu kuhukumu na sheria za MwenyeziMungu (swt) na hapo ndio Allah atafungua Baraka zake mbinguni na ardhini. Lakini kuja huku kunahitaji wanaume wa kweli waliomuahidi Mwenyezi Mungu (swt), wanaume wasioshughulishwa na mauzo wala biashara ila kuilingania faradhi hii iliosahaulishwa kimakusudi. Wanailingania kwa njia ya Mtume (saw) aliyoichukua hadi kufaulu kuisimamisha Serikali ya kwanza ya Kiislamu katika mji wa Madina na hapo ndio waja wa MwenyeziMungu (swt) wakaishi katika nuru na kuingia katika Uislamu makundi kwa makundi. Tunaamini kiza hiki totoro cha udhalimu wa mfumo wa Urasilimali na nidhamu zake chafu ikiwemo ya utawala Demokrasia utaondoshwa na Khilafah itakayowakomboa walimwengu kutoka katika utumwa wa kuabudu wanadamu wenzao hadi kumuabudu MwenyeziMungu Muumba wa wanadamu.
Shabani Mwalimu
Mwakilishi kwa Vyombo Vya Habari
Hizb ut-Tahrir Kenya
Inatoka Jarida la Uqab:3 https://hizb.or.tz/2017/04/01/uqab-3/
Maoni hayajaruhusiwa.