May day: Siku ya Kuwalaza Wafanyakazi Dhidi ya Dhulma Wanazotendewa

بسم الله الرحمن الرحيم

 

Mei Mosi sikukuu inayoadhimishwa duniani kote kama Siku ya Wafanyakazi duniani kote. Siku hii wafanyakazi kwa kupitia Vyama vya Wafanyakazi hupaza sauti za madai yao, hutafakari mafanikio yao na hupanga mikakati mipya ya kupambana na dhulma za waajiri.

Madai ya wafanyakazi kudai haki zao yalishamiri zaidi katikati mwa karne ya 19 katika miji kadhaa ya Ulaya. Hii ni kutokana na kumakinika kwa mfumo wa kibepari. Ndani ya bara la Ulaya kulikuwa na mvutano mkubwa baina ya wafanyakazi na waajiri wao. Kwa kawaida ndani ya mfumo wa kibepari wafanyakazi hunyonywa kwa kufanyishwa kazi kubwa na kupewa malipo duni, kukabiliwa na mazingira magumu ya kazi nk. Unyonyaji huu ulisababisha wafanyakazi wasimame kidete na kuanzisha harakati  katika maeneo ya kazi ili kutatua matatizo yanayowakabili.

Siku ya Mei Mosi imetengwa kimatafa kuwa ni siku ya kupaza sauti na kutafakari madai ya wafanyakazi duniani kote, na vyama vya wafanyakazi huwa kifua mbele katika kuratibu sherehe hizo.

Katika sikukuu hiyo hufanyika madhimisho ambapo wawakilishi wa vyama hivyo huwasilisha malalamiko yao kwa wahusika wa serikali na waajiri wengine ili kuangalia uwezekano wa kuyafanyia kazi.

Kimsingi ndani ya siku hii huonyeshwa hali duni waliyonayo wafanyakazi duniani kote. Lakini pia lazima tukiri kwamba siku hii huwalaza wafanyakazi wasiweze kufikiria mfumo mwingine mbadala wa kutatua matatizo yao na kuwaonyesha kana kwamba ndani ya mfumo wa kibepari matatizo yao yanaweza kutatuka.

Katika mfumo wa kibepari maisha ya wafanyakazi yanazidi kuwa hatarini siku hadi siku na hakuna unafuu wanaoupata. Hufanya kazi kwa malipo madogo, mazingira magumu nk.  Na baada ya mtikisiko wa kiuchumi uliokumba dunia ndani ya mwaka 2009 tumeshuhudia makampuni mengi makubwa yakipunguza idadi ya wafanyakazi na hivyo kupelekea watu wengi zaidi kukosa ajira. Aidha, katika mfumo huu wafanyakazi wamekuwa wakiporwa makato mengi sana kama kodi na za mishahara (Pay as you earn), malipo yanayoitwa ya mfuko wa jamii (social security fund) nk. ambayo huyafanya maisha yao yazidi kuwa magumu siku hadi siku. Makato hayo ni  makubwa sana  kiasi cha kuwafanya washindwe kumudu gharama za kujikumu kimaisha.  Bila ya kutaja ughali wa huduma za jamii kama afya, umeme, maji na makaazi, na  mfumuko mkubwa wa bei katika bidhaa muhimu ambao hutokea mara kwa mara katika uchumi wa kibepari. Kwa hivyo wafanyakazi wengi ndani ya mfumo huu hutumikishwa kinyume na matakwa yao kutokana na ugumu wa maisha. Kiasi cha hunyimwa hata mikataba kitu kinachopelekea kufukuzwa kazi ovyo na kushindwa kulipwa baadhi ya stahiki zao.

Enyi wafanyakazi katika Waislamu na wanadamu kwa jumla: mnashuhudia wenyewe namna mfumo batil wa kibepari unavyokukandamizeni katika suala nyeti la kutafuta rizki. Muda sasa umefika kuubadilisha mfumo huu kwa mfumo mbadala wa Kiislamu kupitia dola yake ya Khilafah ili uweze kudhamini haki za waajiri na waajiriwa kwa uadilifu bila ya upendeleo

Na Kaema Juma.

Maoni hayajaruhusiwa.