Mapinduzi ya Kisayasi Chini ya Ubepari ni Maangamizi Kwa Wanyonge

Ulimwengu leo unapita katika mabadiliko makubwa ya kisayansi na kielimu (madaniyya).Mabadiliko ambayo yamebadili ulimwengu huu kuwa kama kijiji na kuweza kurahisisha kwa haraka shughuli za binadamu katika upande wa uchukuzi, usafiri, mawasiliano, mifumo ya kielekroniki nk.
Aidha, uvumbuzi huu wa kisayansi na mabadiliko ya kiteknolojia umerahisisha katika matibabu kwa uwepo wa vifaa tiba vya kisasa. Bila ya kusahau mapinduzi katika mfumo wa kielekroniki yaliyopelekea kurahisisha shughuli za utunzaji wa kumbumbuku (data), usahali wa malipo katika huduma mbalimbali na kuongeza ufanisi katika shughuli za kila siku. Pia katika sekta ya upatikanaji na upashanaji wa taarifa kumepatika uharaka wa ajabu kwa kupitia vyanzo mbalimbali kama mitandao ya kijamii, televisheni, radio nk.
Bila shaka mapinduzi haya ya kisayansi ni natija/ matokeo ya mwanadamu kuwekeza katika kufikiri na kutafiti ili kufikia njia ya kutatua matatizo yake yanayomkabili kila siku na kufanya shughuli zake za kila siku kwa usahali.

Uislamu umeweka wazi kwamba wanadamu tumedhalilishiwa vyote vilivyomo katika ulimwengu huu kwa ajili ya matumizi yetu. Mola SW Anasema:
وَسَخَّرَ لَكُمْ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الأَرْضِ جَمِيعًا مِنْهُ
‘Na (Mola) kakudhalilishieni vyote vilivyoko mbinguni na ardhini’

Aya hii inatuonesha kuwa Mola SWT kutudhalilishia kutumia na kunufaika na vyote vilivyoko mbinguni na ardhini, hii ina maana kuwa vitu vya kimada anavyovitumia mwanadamu katika kupeleka maisha yake kama vyombo vya usafiri, vifaa vya kielekroniki, vifaa tiba inajuzu kunufaika navyo kwa kuvitumia, kwa Muislamu sharti tu kuzingatia kama havigongani na hadhara (mtazamo wa mfumo) ya Kiislamu.
Kwa bahati mbaya na kwa masikitiko makubwa licha ya mabadiliko yote haya katika sayansi na teknolojia ulimwengu bado ni sawa na pori kubwa ambalo ndani yake wanyama wenye nguvu huwadhuru wanyama wadogo. Watu wa ulimwengu wa tatu na nchi changa kwa jumla wamo katika hali ngumu isiyomithilika kutokana na uwepo wa mfumo dhalimu wa kibepari ambao kipimo chake katika kupeleka mambo ni ‘maslahi, tahamaki natija ya mapinduzi haya ya kisayansi na teknolojia yamekuwa hasi hasa kwa wananchi wanyonge.

Bara la Afrika na nchi changa kwa jumla kuna kila aina ya malighafi muhimu kama vile mafuta, chuma, shaba, urani nk. katika yanayohitajika katika uvumbuzi na mapinduzi haya ya uvumbuzi, tahamaki zimekuwa mahala kana kwamba penye laana.

Kwa masikitiko makubwa mataifa makubwa hasa Marekani, China na nchi za Ulaya Magharibi yamekuwa yakifanya kila aina ya hila na njama chafu katika nchi changa ikiwemo kuwawekea wananchi watawala vibaraka wanaolinda maslahi yao, kuhakikisha nchi hazisongi mbele, iwe katika uvumbuzi au mengineyo kiasi cha kuwaacha daima katika hali ya utegemezi wa kuagiza kutoka nje hata bidhaa duni kama sindano nk.

Mitaala ya elimu katika masomo ya sayansi na utafiti ni ya kikoloni ambayo hubakia katika nadharia na kukaririkariri kama kasuku, hali ambayo ni kikwazo kikubwa katika kufikia malengo ya kuleta mabadiliko msingi kwa wakhitimu hasa wale wa masomo ya juu.

Aidha, sera za kikoloni kuhusu viwanda ambazo hulazimisha nchi changa kuwa na viwanda vyenye kutegemea mitambo na uendeshaji (operators) kutoka nje badala ya kuwa na viwanda vyenye kuzalisha mitambo ya viwanda vyengine na usimamizi wa ndani ambao ungesukuma uvumbuzi na mabadilko ya kweli.

Mataifa ya kibepari yamekuwa vinara wa ujambazi na uporaji usiomithilika katika nchi changa kwa kisingizio cha uwekezaji, na kufanya nchi hizo ni mashamba ya kupata mali ghafi na masoko ya bidhaa za viwanda vyao.

Leo mabadilko haya ya teknolojia ambayo yangetumika katika kuboresha maisha ya watu na kurahisisha maisha ya watu hususan wa chini katika nyanja za afya, usafiri, uchukuzi nk. yamekuwa ndio chanzo cha kuwanyonya raia wa chini nk.

Mataifa makubwa kama Marekani, Uingereza nk. licha ya kuzifanya nchi changa kuwa ndio masoko ya bidhaa zao za viwandani, lakini bado watumiaji wa mwisho huzipata bidhaa hizo kwa gharama kubwa kutokana na kutozwa tozo nyingi na kodi.

Uislamu katika zama wa utawala wake (Khilafah) iliwekeza sana katika uvumbuzi, kiasi cha wasomi wake kutumia taaluma zao katika uvumbuzi wa kisayansi ili kurahisisha maisha ya wanadamu wakati huo. Daima serikali ilishikamana na uoni kuwa jukumu lake kubwa ni kusimamia maisha ya watu na kuhakikisha huduma msingi zinapatikana kwa wepesi na kwa gharama nafuu. Serikali ya Kiislamu husimamia upatikanaji wa huduma hizi si kwa ajili ya kupata faida bali kwa ajili ya kuhakikisha kila raia anapata huduma muhimu kwa sahali.

Msukumo wa wahandisi na wavumbuzi wa Kiislamu nao ulitokana na kipimo cha Kiislamu cha ‘halali’ na ‘haramu’ na sio maslahi. Itakumbukwa kuwa katika zama za Khilafah ya Abassiya (Abu Jaafar Mansoor) kulikuwa na ukuwaji mkubwa wa miji kama Baghdad nk, kiasi cha kupelekea ongezeko la watu na uboreshaji wa huduma za kijamii kama maji safi, afya nk. Katika hali kama hiyo wahandisi katika dola ya Kiislamu waliweza kuja na ubunifu wa hali ya juu ili kutatua changamoto mpya.

Wanasayansi wa Kiislamu licha ya kuwa nchi kama Iraq, Sham, Misri nk. zilikuwa zina maeneo ya majangwa yasiyofaa kwa makazi kutokana na ukosefu wa maji lakini waliweza kutengeneza mifereji ya chini kwenye majabali kutoka kwenye mito mikubwa kama Furati, Nile nk. ili kusambaza maji safi kwa matumizi kupitia mifereji ijulikanayo kama Qanats. (mawaidha mazuri/khabari za Misri). Jambo hili liliboresha hali ya maisha kwa wakati huo na kupelekea kukuwa kwa miji.

Wasomi na wahandisi wa Kiislamu pia waliujaza takriban ulimwengu mzima kheri kutokana na kuweka misingi mingi ya sayansi na teknolojia ambayo baadae iliweza kutumika katika uvumbuzi wa vifaa mbalimbali katika karne ya 8 – 13 Miladiyya

Hali hiyo iliwapelekea baadhi ya hata waandishi wakubwa wa kimagharibi kukiri ukweli wa mchango mkubwa wa Waislamu. Howard Turner katika kitabu chake ‘Science in Medieval Islam ameandika haya:

‘Muslim artists and scientists, princes and labourers together created a unique culture that has directly and indirectlyinfluenced societies on every continent.’
“Mafundi Waislamu, wanasayansi, watawala na vibarua kwa pamoja walikuja na utamaduni wa aina yake ambao moja kwa moja au sio moja kwa moja uliathiri jamii katika kila bara”

Wakati umefika kwa kwa wakazi wa Bara la Afrika na ulimwengu kwa ujumla kuuchukua Uislamu na kuutupa mfumo batili wa kibepari uliofanya maendeleo ya sayansi kuwa maangamizi kwa nchi changa na wanyonge kutokana na kipimo chao hatari cha ‘maslahi’. Kipimo kinachowafanya wanadamu kutaabika licha ya rasilimali tele na maendeleo makubwa ya kisayansi

إِنْ هُوَ إِلاَّ ذِكْرٌ لِلْعَالَمِينَ (ص: 87
‘Haikuwa hii Quran ila ni ukumbusho kwa walimwengu’

#UislamuNdioUfumbuziSahihi

Ust. Issa Nasib

Risala ya Wiki No. 67
23 Rabi’ al-thani 1441 Hijri 20/12/2019 Miladi
Afisi ya Habari – Hizb ut- Tahrir Tanzania
https://hizb.or.tz/

Maoni hayajaruhusiwa.