Kurudi kwa Swala Ndani ya Hagia Sophia na Kelele za Sauti Zinazoitisha Kurudi kwa Khilafah!

بسم الله الرحمن الرحيم

Swali:

Tunajua kwamba Muhammad Al-Fatih – Mwenyezi Mungu awe radhi naye – pindi alipoifungua Konstantinopoli aliifanya Hagia Sophia kuwa msikiti… Tunajua pia kwamba Mustafa Kamal – laana za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake – aliiondoa sifa hii ya msikiti ya Hagia Sophia na kuifanya kuwa makavazi… Mnamo 2013, Erdogan alikataa ombi kutoka kwa Waislamu la kuigeuza tena Hagia Sophia kuwa msikiti… Mwaka huu, na kwa amri kutoka Erdogan, mahakama ilitoa uamuzi wa kuiregesha Hagia Sophia kuwa msikiti…swala ziliswaliwa humo mnamo Ijumaa 24/7/2020, na michoro ya kikristo katika kuta ilizibwa wakati wa swala pekee. Je, hili linaathiri kuswihi kwa swala? Na je, michoro hii ilitoka wapi, wakati Hagia Sophia ilikuwa ni msikiti tohara na safi kwa takriban miaka 500?!

Tunapata mkanganyiko katika hukmu ya Shariah kuhusu Hagia Sophia pindi Muhammad Al-Fatih alipoikomboa, na tunalotaraji kwako, na tunakushukuru, ni kufafanua hukmu ya Shariah juu ya sehemu za ibada za makafiri katika nchi zilizokombolewa, ili nyoyo zetu ziwe amani na jibu hili.

Jibu:

Ili kupata jibu la wazi kwa maswali haya, ni lazima tutathmini mambo muhimu na kadhia zinazo husiana nayo, na kuonyesha hukmu ya Shariah juu yake. Hivyo tunasema, na mafanikio ni kutoka kwa Mwenyezi Mungu:

Kwanza: Katika hotuba yetu iliyopita mnamo 7 Jumada I 1441 H – 2/1/2020 M juu ya Kumbukizi ya Kufunguliwa kwa Konstantinopoli katika mwaka wa 857 H – 1453 M, ili eleza:

[Al-Fatih alianza kuikomboa na kuizingira Konstantinopoli kuanzia tarehe ishirini na sita Rabii’ ul-Awwal hadi ikafunguliwa alfajiri ya tarehe ishirini ya mwezi huu, Jumada al-Awwal 587 H, ikimaanisha kuwa uzingiraji huo ulichukua takriban miezi miwili. Pindi Muhammad Al-Fatih alipoingia mji huu akiwa na ushindi aliteremka kutoka kwa farasi wake, na kumsujudia Mwenyezi Mungu, akimshukuru Mwenyezi Mungu kwa ushindi huu na mafanikio haya. Kisha akaelekea katika Kanisa la Hagia Sophia ambako Byzantini na watawa wao walikuwa wamekusanyika, akawapa ulinzi. Aliamuru Kanisa la Hagia Sophia ligeuzwe kuwa msikiti, na kuamuru kusimamishwa msikiti mahali pa kaburi la swahaba mkubwa Abu Ayub Al-Answari, ambaye alikuwa miongoni mwa safu za kampeni ya kwanza ya ufunguzi wa Konstantinopoli, na ambako alifariki, rehema na radhi za Mwenyezi Mungu ziwe pamoja naye… Al-Fatih, ambaye alipewa jina hili baada ya ufunguzi huu, aliamua kuifanya Konstantinopoli mji mkuu wa dola yake baada ya awali kuwa Edirne, na akaiita Konstantinopoli [Kostantiniyye] baada ya kufunguliwa kwake “Islambol”, ikimaanisha mji wa Uislamu [Dar al-Islam], na maarufu ikajulikana kama “Istanbul”. Al-Fateh akaingia katika mji huu na kwenda hadi Hagia Sophia ambako aliswali ndani yake na ikawa msikiti kwa fadhila, baraka na sifa za Mwenyezi Mungu…

Hivi ndivyo namna bishara njema ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) ilivyo timia; ile iliyoko katika Hadith tukufu kutoka kwa Abdullah ibn Amr ibn Al-As, aliye sema: “Tulipokuwa kando ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) tukiandika, Mtume wa Mwenyezi Mungu aliulizwa, ni upi kati ya miji miwili utafunguliwa mwanzo, Konstantinopoli au Roma?” Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) akasema:

«مَدِينَةُ هِرَقْلَ تُفْتَحُ أَوَّلاً، يَعْنِي قُسْطَنْطِينِيَّةَ»

“Mji wa Heraclius utafunguliwa mwanzo, yaani Konstantinopoli.” Imesimuliwa na Ahmad katika Musnad yake na Al-Hakim katika Al-Mustadrak na akasema: “Hadith hii ni Sahih kwa sharti la mashekhe wawili, lakini hawakuipokea. Adh-Dhahabi alitoa maoni juu yake: “kwa sharti la Bukhari na Muslim”. Vilevile katika Hadith tukufu, kutoka kwa Abdullah bin Bishr Al-Khathami kutoka kwa babake kwamba alimsikia Mtume (saw) akisema:

«لَتُفْتَحَنَّ الْقُسْطَنْطِينِيَّةُ فَلَنِعْمَ  الْأَمِيرُ أَمِيرُهَا وَلَنِعْمَ الْجَيْشُ ذَلِكَ الْجَيْشُ»

“Kwa yakini mtaifungua Konstantinopoli, Amir bora ni Amir wake, na jeshi bora ni jeshi hilo.” Akasema, Maslama bin Abdul Malik aliniita na kuniuliza, hivyo nikamtajia Hadith hii basi akaivamia Konstantinopoli, imesimuliwa na Ahmad. Katika Mujma’ Az-Zawaa’id, katika maoni yake inaeleza: “Imesimuliwa na Ahmad, Al-Bazzar, Al-Tabarani na wapokezi wake ni watu waaminifu…”

Bishara hii njema ilipatikana mikononi mwa kijana huyu, Muhammad Al-Fatih, ambaye umri wake haukuzidi miaka ishirini na moja, lakini alikuwa ametayarishwa sawasawa tangu utotoni mwake. Babake Sultan Murad wa Pili alimlea, na alipata mafunzo mema kutoka mikononi mwa walimu bora zaidi wa zama zake, akiwemo… Sheikh Akshamsaddin Sungkar ambaye alikuwa wa kwanza kupanda akili mwake hadith ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) juu ya “ufunguzi wa Konstantinopoli” tangu utotoni mwake. Hivyo basi kijana huyu alikulia akilenga kufikia ufunguzi huu kwa mikono yake… Mwenyezi Mungu (swt) akamkirimu na kumbariki, akistahiki sifa kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw). Al-Fatih alikuwa kiongozi bora…]

Pili: Tangu wakati huo, Hagia Sophia imekuwa msikiti mkubwa wa Kiislamu, alama kubwa kwa Waislamu, na Muhammad Al-Fatih na wataalamu katika zama zake wakaondoa michoro inayo gongana na Uislamu kutoka katika kuta, na kuiziba michoro ambayo ilikuwa vigumu kuondoka kwa rangi au mfano wake. Ulikuwa msikiti tohara, msafi, unaong’aa ambao Waislamu waliswali, kumsifu Mwenyezi Mungu kwa ushindi huo na ufunguzi ulio wazi… Hili liliendelea hadi mhalifu wa zama hizi Mustafa Kamal alipozuia kuswali ndani ya msikiti huu na kuugeuza kuwa makavazi kupitia uamuzi wake muovu mnamo 24/11/1934 M… Na kabla ya hapo, yeye, Mwenyezi Mungu amlaani, aliufunga msikiti huu kuanzia 1930 kwa takriban miaka minne: [“Hagia Sophia ulifungwa kwa ajili ya wenye kuswali kati ya 1930-1935 M kwa sababu ya kazi ya ukarabati, ambapo ilitekelezwa kwa amri ya Mustafa Kamal, mwanzilishi wa Jamhuri ya Uturuki. Wakati wa kazi hii ya ukarabati, shughuli kadha wa kadha za ukarabati zilifanywa… ikifuatiwa na uamuzi wa Baraza la Mawaziri mnamo 24/11/1934 wa kuigeuza Hagia Sophia kuwa makavazi.” (aa.com.tr/ar/190 Anadolu Agency 11/7/2020 M)]

Yaani, msikiti huu ulibakia umefungwa katika kipindi hiki, na katika kipindi hiki, upo uwezekano kwamba baadhi ya watu walikuja kutoka nchi za Magharibi kuchora michochoro hiyo na kisha Makavazi ya Hagia Sophia yakafunguliwa mnamo 1935 M. Baada ya uamuzi huu, ili kuwaonyesha watu kuwa kuna mabaki na michoro ya Wakristo! Kabla ya hilo, Mustafa Kamal alikuwa ametekeleza uhalifu wake mkubwa zaidi wa kuivunja Khilafah ya Kiislamu mnamo 1342 H – 1924 M. Kama ambavyo Mustafa Kamal aliupiga vita vikali kila ulinganizi wa kuirudisha Khilafah; vilevile, aliupiga vita kila ulinganizi wa kuirudisha Hagia Sophia kuwa msikiti… Lakini, Waislamu waliendelea kutamani kuirudisha Hagia Sophia kuwa msikiti kama ilivyo kuwa. Tovuti ya Almodon ilieleza mnamo 26/3/2019: [bado Waturuki wengi wangali wanatazamia siku ambayo Makavazi ya Hagia Sophia yatarudi kuwa msikiti kwa Waislamu. (Mnamo 27/5/2012, maelfu ya Waislamu waliswali mbele ya jengo lake kupinga sheria ya kupiga marufuku ibada ndani yake, katika tukio la kumbukizi ya 559 ya ushindi wa Sultan Muhammad Al-Fatih na ufunguzi wake wa Konstantinopoli. Waandamanaji walitamka kwa kupaza sauti: “Vunjeni minyororo… na fungueni Msikiti wa Hagia Sophia… Msikiti Uliotekwa”) na azma yao haikudhoofika kwa kutaka ifunguliwe kama msikiti [lakini Erdogan akajibu matakwa haya alipokuwa Waziri Mkuu mnamo 2013 M, kwamba hatafikiria kubadilisha hadhi ya Hagia Sophia… (tovuti ya Almodon)].

Tatu: Lakini mtazamo wa Erdogan ulibadilika wakati wa kampeni ya propaganda kwa ajili ya uchaguzi wa manispaa za miji uliofanyika nchini Uturuki mnamo Jumapili, 30/3/2019 ambapo aligundua kushuka kwa kiwango cha uorodheshwaji wake; kana kwamba aliona kuwa kudandia vuguvugu la kutaka kugeuzwa kwa Hagia Sophia kuwa msikiti ingeongeza mgao wake wa kura za ubunge, hivyo akaukumbatia mwito huu kileleni mwa kampeni ya uchaguzi: (Raisi wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alisema mnamo Ijumaa kwamba Hagia Sophia jijini Istanbul inapaswa kupewa jina upya kama msikiti badala ya makavazi baada ya uchaguzi wa Jumapili. Uchaguzi wa kesho wa manispaa utafanywa nchini Uturuki; Chama cha AK kinatazamia kushinda, kama ilivyo kuwa hali mnamo 2014… (Al-Jazeera.net Jumamosi, 30/3/2019). Lakini Waislamu wanatambua kwamba kurudi kwa Hagia Sophia kuwa msikiti kunahusiana na Uislamu, dola ya Uislamu, Khilafah. Hagia Sophia ilikuwa msikiti maridadi wa dola ya Khilafah, anwani ya ushindi na Fath (ufunguzi) dhahiri na kutimia kwa bishara njema ya Mtume mkweli na mwaminifu wa Mwenyezi Mungu (saw)… Hivi ndivyo namna waumini wenye ikhlasi wanataka: kurudi chini ya kivuli cha bendera ya Khilafah, bendera ya hapana Mola wa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu, Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu; sio kufinikwa na kivuli cha bendera ya usekula na nidhamu zilizotungwa na wanadamu! Hivyo basi, kampeni ya uchaguzi wa ubunge ya Erdogan haikupata kurudi kwa Hagia Sophia kama msikiti, haikupata lengo lake, na akashindwa Istanbul na Ankara; yaani miji miwili mikubwa zaidi nchini Uturuki! Alishindwa na nani?

Mbele ya Chama cha Watu, miongoni mwa wafuasi wa Mustafa Kamal, aliyeigeuza Hagia Sophia kuwa makavazi!! Hii ni kwa sababu watu hawakuona tofauti kubwa baina ya vyama hivi maadamu hakuna chochote kilichotaka Hagia Sophia kufinikwa na kivuli cha Khilafah.

Nne: Erdogan hakutambua kuwa kurudi kwa Hagia Sophia kama ilivyokuwa, msikiti, hakutazaa matunda na kusaidia umaarufu wake pekee ikiwa haitafuatanishwa na kurudi kwa Khilafah. Ingawa aliliona hili peupe katika matokeo ya uchaguzi, lakini aliendelea kufuata njia ile ile! Hivyo, kwa mujibu wa amri na matakwa yake, Mahakama ya Upeo ya Uturuki ilitoa hukmu mnamo 10/7/2020 ya kuyageuza Makavazi ya Hagia Sophia jijini Istanbul kuwa msikiti pasi na kutaja uhusiano wake na kurudi kwa Khilafah na kisha swala za Ijumaa zikaswaliwa mnamo 24/7/2020 huku mfumo wa kisekula na sheria zilizotungwa na wanadamu bado zikisalia hai zikipumua juu ya Msikiti wa Hagia Sophia!!

Swala hiyo ilidhihirisha namna gani Waislamu wanavyo tamani kurudi kwa Khilafah na kurudi kwa Msikiti wa Hagia Sophia kama ulivyo kwa miaka 500. Hili lilidhihirika kwa kusherehekea watu wengi kwa yale yaliyozungumzwa katika hotuba ya Ijumaa na Ali Arbash, mkuu wa Maswala ya Kidini wa Uturuki, tarehe tatu Dhul-Hijjah 1441 H mnamo 24/7/2020 M ndani ya Msikiti wa Hagia Sophia baada ya swala kurudi ndani yake baada ya kufungwa kwake kwa miaka 90… hususan aliposema: (Sifa njema zote na shukran ni za Mola wetu Azza Wa Jal aliyetufanya tukutane pamoja katika siku hii tukufu ya kihistoria. Rehma na amani zimshukie Mtume wetu mtukufu zaidi (saw) alitoa bishara njema ya ufunguzi katika hadith yake:

«لَتُفتَحَنَّ القُسْطَنْطينيَّةُ؛ فَلَنِعْمَ الْأَمِيرُ أَمِيرُهَا، وَلَنِعْمَ الْجَيْشُ ذَلِكَ الْجَيْشُ»...

“Kwa yakini mtaifungua Konstantinopoli, Amir bora ni Amir wake, na jeshi bora ni jeshi hilo.”

Na rehma ziwe juu ya maswahaba watukufu waliojitokeza katika njia ya Mwenyezi Mungu kutimiza bishara hii njema, huku Abu Ayub Al-Ansari (ra) akiwa msitari wa mbele ambaye anachukuliwa kama muasisi wa maadili wa Istanbul, na juu ya wale wanaofuata nyayo zao na juu ya mashahidi na wanajeshi wetu wote walioifanya Anadolu (Anatolia) kuwa nyumba yetu, kuilinda, na kuikabidhi kwetu.

Na rehma ziwe juu ya Akshamsaddin, mwenye elimu na hekima, aliyeyachonga mapenzi ya ukombozi moyoni mwa Sultan Muhammad Al-Fatih, ambaye aliowaongoza waumini katika swala ya kwanza ya Ijumaa katika Msikiti wa Hagia Sophia mnamo 1/6/1453 M. Na rehma ziwe juu ya Amiri huyu mchanga na mtambuzi na mkombozi Sultan Muhammad Khan… ambaye, kwa neema na utunzaji wa Mwenyezi Mungu Azza Wa Jal, aliweza kuikomboa Istanbul… Na pia, rehma ziwe juu ya fundi mkubwa, Mi’mar Sinan, aliyeipamba Hagia Sophia kwa minara.

Hagia Sophia ni alama kuu ya ukombozi, na amana ya Al-Fatih. Sultan Muhammad Al-Fatih aliifanya sehemu hii kuwa wakf kwa sababu hadhi yake ni msikiti hadi Siku ya Kiyama, na aliuacha mikononi mwa waumini. Katika imani yetu, mali ya wakf haiwezi kulegezwa msimamo; sharti lililowekwa na mtu aliyeifanya mali kuwa wakf ni muhimu mno. Anayelikiuka anastahiki kulaaniwa / kulaumiwa. Hivyo basi, Hagia Sophia kuanzia wakati huo hadi leo sio tu ni moja ya majengo matukufu ya nchi hiyo; bali pia ni moja ya matukufu ya Ummah wa Muhammad (saw)… (aa.com.tr/ar/192 24/7/2020 Istanbul / Anadolu).

Tano: Fahamu za Uislamu zinakorogeka nyoyoni mwa Waislamu, hususan wanaposikia bishara njema ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) ya kufunguliwa kwa Konstantinopoli, na wanatambua kwamba utawala wa Uislamu ndio ulioifungua Istanbul, na ndio uliopelekea Hagia Sophia kuwa msikiti. Istanbul na msikiti wake, Hagia Sophia, ziliendelea kama kituo cha Khilafah ya Uthmani kwa miaka mia tano. Hizi ndizo fahamu za Khilafah zinazoingia nyoyoni mwao, na hata wakati mmoja zilikuwemo ndani ya vyombo vya habari kama ilivyo elezwa na jarida, Gerçek Hayat – Maisha Halisi. Ash-Sharq Al-Awsat ilitaja: Jumanne – 7 Dhul-Hijjah 1441 H – 28 Julai 2020 M: [Wakati huo huo, jarida moja linaloitwa Gerçek Hayat – Maisha Halisi katika toleo lake jipya, lililotolewa juzi, kwa ajili ya tangazo la Khilafah nchini Uturuki. Jarida hili lilichapisha katika jalada lake msemo wa Kiarabu unaosema: “Ikiwa si sasa, basi lini?”]. Erdogan alipaswa kujibu hilo badala ya msemaji wa chama chake aliye zungumza dhidi yake:

[Ankara (gazeti la Uturuki la Zaman) – Msemaji wa chama tawala cha Uturuki cha Uadilfu na Maendeleo, Omer Celik, alilaani mabishano yaliyozuka baada ya kufunguliwa kwa Msikiti wa Hagia Sophia, kufuatia miito ya Khilafah. Jarida la Gerçek Hayat (Maisha Halisi) leo lilichapisha katika jalada lake misemo inayotoa wito wa kuifufua tena Khilafah ya Kiislamu. Celik alieleza kuwa Uturuki ni dola ya kikanuni ya kidemokrasia, kisekula na kijamii, na ni makosa kuunda upendeleo wa kisiasa kuhusiana na nidhamu ya kisiasa ya Uturuki… aliendelea kusema: “Namuombea rehma kiongozi wa vita vya huru na muasisi wa jamhuri na mtawala wake wa kwanza, Mustafa Kemal, (Ataturk), na viongozi wote wa Vita vya Uhuru. Tutawasili na hatua mwafaka na imara katika matakwa ya watu wetu na kwa uongozi wenye ujuzi wa raisi wetu. Dua zetu ziko pamoja na watu wetu na lengo letu ni umoja wa nchi. Ishi maisha marefu jamhuri ya Uturuki…” (Zaman Turkey 27/07/2020)]. Hivyo basi, msemaji huyo wa chama tawala anafichua kwamba jambo hili si kwa ajili ya Mwenyezi Mungu bali ni kwa ajili ya lengo linalopita la kidunia!

Hii sio jinsi mambo yanavyoendeshwa ewe raisi wa Jamhuri! Ingawa kila Muislamu aliye na ikhlasi katika Uislamu wake, moyo wake ulijaa furaha kwa kuregea kwa msikiti wa Hagia Sophia, lakini kila Muislamu aliye na ikhlasi na Uislamu wake pia anautaka uwe kama Muhammad Al-Fateh alivyo uanzisha, anwani ya ushindi na ufunguzi wazi, moto unaowaka katika ushindi wa Khilafah Uthmani, Khilafah ya Kiislamu, kutimia kwa biashara njema ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw)… hivi ndivyo namna kila Muislamu mwenye ikhlasi anavyo taka, msikiti unaong’aa ambao bendera ya Uislamu itapandishwa juu yake, bendera ya utawala wa Uislamu, bendera ya Khilafah ambayo iliufinika kwa kivuli chake kwa karibu miaka 500. Na sio kurudi kwa Hagia Sophia kuwa msikiti kwa lengo la uchaguzi linalopita, wa manispaa au ubunge! Ambao unafinikwa na bendera ya usekula na kanuni zilizotungwa na wanadamu zinazotumikia maslahi ya wakoloni makafiri, na sio maslahi ya Uislamu na Waislamu! 

Sita: Ama kuhusu lile lililokuja mwisho wa swali (Tunapa mkanganyiko katika hukmu ya Shariah kuhusu Hagia Sophia pindi Muhammad Al-Fatih alipoikomboa, na tunalotaraji kwako, na tunakushukuru, ni kufafanua hukmu ya Shariah juu ya sehemu za ibada za makafiri katika nchi zilizokombolewa, ili nyoyo zetu ziwe amani na jibu hili…)

Ndugu yangu, si sahihi kuwepo na mkanganyiko katika hukmu ya Shariah, na hata kama kuna rai tofauti tofauti katika baadhi ya matagaa miongoni mwa wanachuoni wa fiqh wa Kiislamu, zitaangukia chini ya yale wanayoona kuwa na kiwango cha chini cha shaka kwa msingi wa ufahamu wao sahihi wa dalili za Kisheria ambazo wanazichukulia kuwa sahihi, hivyo hakuna mkanganyiko.

Ama kuhusu swala hili, sio jipya, bali wanachuoni walilizungumzia nyuma, na baada ya kulitafiti, ni wazi kwamba;

Nchi zilizofunguliwa zinaangukia ndani ya moja ya vigawanyo hivi

1- Ardhi ambazo Waislamu wamezijenga na kuziimarisha, kama vile Kufa, Basra, Wasit na mithili yake, hairuhusiwi kujenga kanisa au sinagogi ndani yake. Endapo Dhimmi (raia wasiokuwa Waislamu) wataingia ndani ya maeneo haya, hawatapewa uwezo wa kuuza au kununua… nk kunywa pombe, au kufuga nguruwe, kwa sababu ni Dar ul Islam (Makaazi yaliyo asisiwa ya Uislamu) kwa Waislamu hii ni kutokana na hadith ya Mtume (saw):

«لا تُبْنىَ بيعةٌ في الإسلام ولا يجدد ما خرب منها»

“Chini ya Uislamu hakujengwi kanisa wala lililoharibika halifanyiwi ukarabati.” Imepokewa na Alaa Din Al-Burhan Furi (aliyefariki: 975 H), katika Kanz Al-U’mal fi Sunnan Al-Aqwal na Al-Af’al kutoka kwa Ibn Asakir kutoka kwa Umar, pia imepokewa na As-Siyuti katika Al-Jami’ Al-Kabir. Ibn Abbas amesema katika riwaya ya Ikrimah kutoka kwake:

«أَيُّمَا مِصْرٍ مَصَّرَتْهُ الْعَرَبُ فَلَيْسَ لِلْعَجَمِ أَنْ يَبْنُوا فِيهِ بِنَاءً، أَوْ قَالَ: بِيعَةً»

 “Nchi yoyote iliyoundwa na Waarabu basi asiyekuwa Muarabu haruhusiwi kujenga jengo, au alisema: kujenga kanisa” [imepokwa na Ibn Abi Shaybah katika Musanaf yake].

2- Ardhi ambazo Waislamu wamezifungua kwa amani, hukmu ya mahekalu na makanisa imejengwa juu ya masharti ya amani yaliyoko juu yake, na ni bora zaidi kuweka amani nao kwa vifungu ambavyo Khalifah Umar, Mwenyezi Mungu awe radhi naye, alikubaliana nao mwaka wa 15 H – 638 M katika mkataba wa Umar na watu wa Eliya (Al-Quds) wakati Waislamu walipoifungua.

3- Ardhi ambazo Waislamu walizifungua kwa nguvu, hairuhusiwi kuweka chochote katika hivi ndani yake (kujenga makanisa nk.) kwa sababu imekuwa ni mali ya Waislamu. Kuhusu kabla ya ufunguzi wake, kuna mambo mawili:

Mojawapo ni kuwa kupitia ufunguzi (kwa nguvu) imekuwa ni nchi inayomilikiwa na Waislamu, Dar ul Islam (makaazi ya Uislamu), hivyo hairuhusiwi kuwa na hekalu au kanisa, mithili ya nchi zilizoundwa na Waislamu.

La pili, ni kuwa inaruhusiwa kuyabakisha maabadi yao, kwa sababu katika Hadith ya Ibn Abbas iliyo pokewa na Abi Shaybah katika Musanaf yake:

«أَيُّمَا مِصْرٍ مَصَّرَتْهُ الْعَجَمُ يَفْتَحُهُ اللَّهُ عَلَى الْعَرَبِ وَنَزَلُوا يَعْنِي عَلَى حُكْمِهِمْ فَلِلْعَجَمِ مَا فِي عَهْدِهِمْ…»

 “Nchi yoyote iliyoundwa na wasiokuwa Waarabu kisha Mwenyezi Mungu akaifungua kwa Waarabu na akawaondosha (wasiokuwa Waarabu) katika utawala wake, basi haki za wasiokuwa Waarabu ziko katika ahadi zao”

Hivyo basi, ni juu ya mfunguzi aliyeifungua ardhi kwa nguvu, kwa mujibu wa yale anayoyaona kuwa maslahi ya Uislamu na Waislamu na usimamizi wa mambo ya raia, Waislamu pamoja na watu wa Dhimma (wasiokuwa Waislamu).

Na kwa sababu mada ya Konstantinopoli inakuja katika sehemu ya (Ufunguzi kwa nguvu), nitafikisha rai za baadhi ya wanachuoni wa fiqh ili kutoa uhakikisho zaidi.

A- Imeelezwa katika Mughni Al-Muhtaj Ila Ma’rifat Alfath Al-Minhaj na Muhammad Al-Sherbini, aliyefariki mnamo 977 H, katika kufafanua maandishi ya Minhaj At-Talibeen ya An-Nawawi (aliyefariki: 676 H).

[(Na tunawazuia kujenga kanisa katika nchi tuliyoiunda au ambayo watu wake wameingia katika Uislamu, ambayo haikufunguliwa kwa nguvu, hawawezi kuliasisi (kanisa) na wala kupewa idhini ya kanisa lililokuwemo ndani yake, hii ndio sahihi zaidi. Au ikiwa (imefunguliwa) kwa amani, maadamu ardhi hii ni yetu, sharti la makaazi yao, na kubakisha makanisa yao linaruhusiwa, ikiwa hili litakuwa ni jumla, sahihi zaidi ni kuwazuia, au kuamuliwa kwa ajili yao, na huenda wakaliasisi (kanisa), hii ndio sahihi zaidi.)

Ufafanuzi: (na wazuieni) huu ni wajibu (ujenzi wa kanisa) na hekalu au kwa watawa, na hekalu la moto la Majusi (katika nchi tuliyoiasisi)… (au) nchi (walioingia watu wake katika Uislamu)… (na) nchi yoyote ambayo (imefunguliwa kwa nguvu) kama vile Misri na Isfahaan nchi ya Maghreb (Kaskazini Magharibi mwa Afrika) (hawawezi kulijenga huko); kwa sababu Waislamu wamezimiliki na kuzichukua, hivyo kanisa haliwezi kujengwa. Na kama ambavyo imeharamishwa kulijenga, hairuhusiwi kuregeshwa upya endapo litavunjika (hawapewi idhini ya Kanisa ambalo lilikuwemo ndani yake, sahihi zaidi) kama ilivyo tajwa… na (rai) ya pili ni kuwapa idhini; kwa sababu maslahi huenda yakahitaji hilo, na swala la kutofautiana ni juu ya lile (kanisa) ambalo tayari lilikuweko wakati wa ufunguzi…].

B- Imeelezwa katika (Fath al-Qadeer) na Kamal al-Din Muhammad, anayejulikana kama Ibn al-Hammam (aliyefariki: 861 H) (fiqh ya Hanafi):

(Ya pili ni ile iliyofunguliwa na Waislamu kwa nguvu; hairuhusiwi kujenga huko, hii ni itifaki, na ikiwa kuna jengo huko, linapaswa kuvunjwa? Malik na Shafi’i wamesema katika maneno ya Ahmad katika riwaya; kuwa ni wajib (kuvunjwa). Na sisi tunasema tutawafanya wasimamizi wa mambo yao katika kuyabadilisha makanisa yao kuwa makaazi na wanazuiwa kufanya ibada humo, lakini hayatavunjwa. Hii ni kauli ya Shafi’i na riwaya ya Ahmad, kwa sababu maswahaba walizifungua ardhi nyingi kwa nguvu na hawakuvunja kanisa lolote, wala hekalu, na kamwe haikusimulia juu ya hili).

C- Imeelezwa katika Al-Mughni, na Ibn Qudamah, (aliyefariki 620 H)

(Sehemu ya pili, zile ambazo Waislamu wamezifungua kwa nguvu, hairuhusiwi kujenga jengo la aina yoyote, kwa sababu sasa imekuwa ni mali ya Waislamu, na ama kuhusu majengo ambayo tayari yapo, kuna rai mbili, ya kwanza, kuwa ni wajib kuvunjwa, na inaharamishwa kuyabakisha kwa sababu ni ardhi inayomilikiwa na Waislamu, hairuhusiwi kuwa na kanisa ndani yake, mithili ya nchi ambayo Waislamu ndio walioiunda.

Rai ya pili ni kuwa inaruhusiwa; kwa sababu katika Hadith ya Ibn Abbas:

«أَيُّمَا مِصْرٍ مَصَّرَتْهُ الْعَجَمُ، فَفَتَحَهُ اللَّهُ عَلَى الْعَرَبِ، فَنَزَلُوهُ، فَإِنَّ لِلْعَجَمِ مَا فِي عَهْدِهِم»

“Nchi yoyote iliyoundwa na wasiokuwa Waarabu kisha Mwenyezi Mungu akaifungua kwa Waarabu na akawaondosha (wasiokuwa Waislamu) katika utawala wake, basi haki za wasiokuwa Waarabu ziko katika ahadi zao”).

Saba: Kutokana na haya, majibu ya maswali yaliyotajwa katika swali kwa mukhtasari ni kama yafuatavyo:

1- Ikiwa nchi imefunguliwa kwa amani, itaamiliwa kwa mujibu wa masharti ya maridhiano, kama yaliyotokea katika Mkataba wa Umar (Mapatano ya Umar) wakati wa ufunguzi wa Bait ul Maqdis (Jerusalem).

2- Na ikiwa nchi imefunguliwa kwa nguvu, basi jambo lake litarudishwa kwa mtawala wa Kiislamu aliyeifungua kulibakisha kwa ajili ya ibada zao au kutolibakisha, kwa mujibu wa lile atakalo tabanni kwa maslahi ya Uislamu na Waislamu na katika usimamizi wa mambo ya raia, Waislamu na Dhimmi.

3- Hivyo basi, alilofanya Muhammad Al-Fateh, Mwenyezi Mungu amrehemu, na awe radhi naye, kwa kuigeuza Hagia Sophia kuwa msikiti, ni sehemu ya mamlaka yake, kwa sababu nchi hii ilifunguliwa kwa nguvu.

4- Kuna riwaya kwamba Muhammad Al-Fatih alimlipa Papa wa dhehebu la Kigiriki la Orthodox bei ya ununuzi wa Hagia Sophia, kwa muktadha wa muamala mwema na madhimmi, yaani Wakristo jijini Istanbul, na baadhi ya nyaraka za kihistoria kwa mujibu wa riwaya hizi zinathibitisha kuwa Sultan Muhammad wa pili aliyejulikana kama Muhammad Al-Fatih alilipa bei hiyo iliyotangulia kutajwa ya ununuzi [kutoka katika pesa zake na sio pesa za dola, na akaisajili kwa hati miliki ya kibinafsi kwa jina lake. Jambo hili lilinakiliwa kupitia mkataba wa mauzo na ukabidhi wa mali hii, na uthibitisho wa malipo ya pesa kwa bili za malipo, baada ya kuufungua mji wa Konstantinopoli wakati wa utawala wake wa Dola ya Uthmani. Kisha akairembesha mali hii kwa manufaa ya jumuiya kama Wakf kwa jina la Abu Al-Fath Sultan Muhammad…] Na ima riwaya hizi ni za kweli au zenye tetesi, kuhusu ununuzi huo, mtawala anaye tawala kwa Uislamu, anapofungua ardhi za makafiri kwa nguvu, anaruhusiwa kuyabakisha mahekalu yao na anaruhusiwa kutoyabakisha kama tulivyo onyesha juu.

5- Ama kuhusu kuswihi kwa swala, kwa kuwepo michoro kutani, na kuiziba tu wakati wa swala pekee… maadam imezibwa, swala inaswihi… lakini hairuhusiwi kuidhihirisha baada ya swala, na dola inaingia katika dhambi kubwa kwa hilo. Hukmu ya Shariah ni uharamu wa picha juu ya kuta za msikiti au sehemu yoyote ndani yake. Endapo zitapatikana ni lazima ziondolewa. Ikiwa hili haliwezekani kwa sababu fulani, basi zinapaswa kuzibwa kwa njia ya kudumu kupitia mbinu mwafaka, ambazo zitazizuia kuonekana tena. Miongoni mwa dalili ni:

Bukhari amepokea kutoka kwa Ikrimah kutoka kwa Ibn Abbas (ra)

«أَنَّ النَّبِيَّ ﷺ لَمَّا رَأَى الصُّوَرَ فِي الْبَيْتِ “يعني الكعبة” لَمْ يَدْخُلْ حَتَّى أَمَرَ بِهَا فَمُحِيَتْ…»

“kwamba Mtume (saw) pindi alipoziona picha ndani ya nyumba (yaani Ka’aba) hakuingia mpaka baada ya kuamrisha zifutwe.” [Imepokuwa na Ibn Habban katika Sahih yake].

Katika Musnad ya Ahmad, kutoka kwa Jabir Ibn Abdullah:

«أَنَّ النَّبِىَّ ﷺ نَهَى عَنِ الصُّوَرِ في الْبَيْتِ وَنَهَى الرَّجُلَ أَنْ يَصْنَعَ ذَلِكَ وَأَنَّ النَّبِىَّ ﷺ أَمَرَ عُمَرَ بْنَ الْخَطَّابِ زَمَنَ الْفَتْحِ وَهُوَ بِالْبَطْحَاءِ أَنْ يَأْتِي الْكَعْبَةَ فَيَمْحُوَ كُلَّ صُورَةٍ فِيهَا وَلَمْ يَدْخُلِ الْبَيْتَ حَتَّى مُحِيَتْ كُلُّ صُورَةٍ فِيهِ»

“Kwamba Mtume () alikataza picha ndani ya nyumba, na akakataza mtu kuzitengeza… na kwamba Mtume () alimwamrisha Umar ibn al-Khattab aliyekuwa al-Batha’ wakati wa ufunguzi (wa Makkah) aje katika Ka’aba afute kila picha ndani yake na hakuingia katika nyumba hiyo mpaka zilipofutwa picha zote ndani yake.” Hii pia imepokewa na Bayhaqi katika As-Sunnan Al-Kubra.

Kwa haya, ni haramu kuweka picha msikitini au sehemu ya ibada nyakati zote, haitoshelezi kufinikwa tu wakati wa swala pekee na kisha kufunuliwa baadaye, la sivyo utawala utakuwa na hatia.

Kuhitimisha, namuomba Mwenyezi Mungu (swt) kuharakisha kusimama kwa Khilafah mikononi mwa wafanyikazi wake miongoni mwa Waislamu, ili kila kitu katika bishara njema ya Mtume (saw) kitimie: ukombozi wa Ardhi Iliyo Barikiwa kutokana na najisi ya Mahayudi, ufunguzi wa Roma baada ya mtangulizi wake Konstantinopoli kufunguliwa, na ardhi itang’aa kwa utukufu wa Uislamu na bendera ya Uislamu itapepea juu ya bendera nyengine zote.

[وَاللَّهُ غَالِبٌ عَلَى أَمْرِهِ وَلَكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لا يَعْلَمُونَ]

“Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kushinda katika jambo lake, lakini watu wengi hawajui” [Yusuf: 21]

Siku ya Arafah 1441 H

30/7/2020 M

Maoni hayajaruhusiwa.