Kurogwa kwa Mtume (saw)

ﺑﺴﻢ ﷲ ﺍﻟﺮﺣﻤﻦ ﺍﻟﺮﺣﻴﻢ

Swali:

Je Inawezekana kuwa Mtume ( S.aw ) Alirogwa? Mpaka alikuwa kama anavyopokea Bi Aisha, kwamba alikuwa anadhani kwamba kafikiwa na kitu ili hali hajafikiwa na kitu chochote, mpaka anaendelea kusema bi Aisha kwamba alikuwa anadhani ya kuwa amewaingilia wake na hali ya kuwa hajawaingilia.

Jibu:

Hili tamko la hadithi na yale yaliopokelewa katika kauli:

قال الإمام محمد بن إسماعيل البخاري: حدثنا إبراهيم بن موسى أخبرنا عيسى بن يونس عن هشام عن أبيه، عن عائشة -رضي الله عنها- قالت: سحر رسول الله -صلى الله عليه وسلم- رجل من بني زريق يقال له لبيد بن الأعصم، حتى كان رسول الله -صلى الله عليه وسلم- يخيل إليه أنه كان يفعل الشيء وما فعله (في رواية البخاري من حديث في باب هل يستخرج السحر حديث (5765) من طريق ابن عيينة أن عائشة قالت: ” حتى كان يرى أنه يأتي نساءه ولا يأتيهن “

Amesema Imam Muhammad Bin Ismail Al-Bukhari: ametuelezea Ibrahim Bin Mussa, amesema: ametupa khabari Issa Bin Yunus, toka kwa Hisham, toka kwa Baba yake, Toka kwa Bi Aisha (Allah awe Radhi naye) amesema : Amemroga Mtume ( S.a.w ) mtu toka kabila la Bani Zuraiq, anaitwa Labid Bin Al-a’aswam, Mpaka alikuwa Mtume ( S.a.w ) akidhanishiwa kuwa kafanya kitu na kumbe hakufanya kitu ( Na katika mapokezi ya Bukhari katika hadithi kwenye mlango wenye kichwa cha habari je unatolewa uchawi? Hadithi namba 5765 toka mapokezo Ibn Uyainah kwamba bi Aisha amesema : “Mpaka alikuwa anaona kana kwamba amewaingilia wake zake na hali ya kuwa hajawaingilia”

Nayo ni tafsiri na ubainifu wa yale yaliotajwa kwa jumla na kuenea katika mapokezi) mpaka ilipokuwa siku fulani au usiku fulani na yeye akiwa kwangu, huku akiomba na kuomba, kisha akasema : Ewe Aisha, naona kwamba Allah amenijibu katika yale niliomuomba (yaani ameyakubali maombi yangu)? Wamenijia Wanaume wawili (katika mapokezi ya Ahmd na Twabarani : wamenijia Malaika wawili) akakaa mmoja wao upande wa kichwani kwangu na mwingine upande wa miguu yangu, akasema mmoja kwa mwenzie: Huyo mtu ana maradhi gani? akasema amerogwa amerogwa, akasema : Nani kamroga? akasema: Labid Bin Al-a’aswam, akasema : Kwenye kitu gani? akasema: Kwenye chanuo na kwenye nywele zinazoanguka wakati wa kuchana na (vimewekwa) kwenye kaa (kuti) lililokauka la mtende dume, akasema na liko wapi hilo? akasema lipo kwenye kisima cha Dhar’waan, akalifata Mtume (s.a.w) na baadhi ya Maswahaba wake.(kwenda kulitoa )

Akaja akasema: Ewe Aisha kana kwamba maji (kwenye hicho kisima ) ni  maji yamelalishiwa humo hina kwa ule wekundu wake na kana kwamba vichwa (matawi) ya Mitende yake ni vichwa vya shetani’ nikasema: Kwanini usiitoe (hilo kuti) akaamrisha likafukiwa) Akasema: Allah ameniokoa nalo, na sikupenda kutanguliza kwa watu shari, ameitoa Bukhari kwenye kitabu(mlango) cha tiba.

Na inawezekana kufupisha shubha zilizopo katika hadithi katika mambo matatu:

Moja: Kwamba hadithi hii ijapokuwa kaipokea Bukhari na Muslim hiyo ni hadithi ahadi, haichukuliwi katika mambo ya Itikadi, na pia haichukuliwi katika jambo la  kuhifadhiwa Mtume (S.a.w) na kutokuathirika na uchawi katika akili yake, itikadi katika itikadi, haiwezi kuchukuliwa katika kuthibitisha yale yaliokinyume chake isipokuwa kwa yakini kama hadithi mutawatiri, na wala haitoshi hadithi dhannii katika hilo.

Pili: Hakika hadithi inapingana na Qur’ani ambayo ni Mutawatir na Yakini, katika kukanusha kurogwa Mtume (S.a.w), Qur’an imewakosoa washirikina na kuwafedhehi kwa kunasibisha uchawi kwa Mtume (S.a.w) amesema Allah :

وقال الظالمون إن تتبعون إلا رجلا مسحورا

 * انظر كيف ضربوا لك الأمثال فضلوا فلا يستطيعون سبيلا

“Na Madhalimu wakasema “Nyinyi hamumfuati ila mtu aliyerogwa”

Tazama jinsi wanavyokupigia mifano (isiokuelekea) basi wamepotea wala hawataweza (kushika) njia  ilionyooka. (TMQ 25 : 8-9 )

Na anasema tena:

{ نحن أعلم بما يستمعون به إذ يستمعون إليك وإذ هم نجوى إذ يقول الظالمون إن تتبعون إلا رجلا مسحورا * انظر كيف ضربوا لك الأمثال فضلوا فلا يستطيعون سبيلا }

“Tunajua sana sababu wanayosikilizia, wanapokusikiliza, na wanaponong’ona wanaposema hao madhalimu ( Kuwaambia Waislamu kwa ajili ya kutaka kuwapoteza) “Nyinyi hamumfuati isipokuwa Mtu aliyerogwa”.

Tazama jinsi wanavyokupigia Mifano ( ya uwongo, mara amerogwa, mara muongo, mara…) Basi wakapotea, kwa hivyo hawawezi kupata njia ( ya kuwapelekea katika haki )  [TMQ 17 : 47-48]

Kwamba lau ingefaa kwa Mtume ( S.a.w ) adhani kwamba kafanya kitu, kubwa hajafanya kitu, basi ingefaa pia adhani kwamba kachukiwa na kitu ( Wahyi ) kumbe hajashukiwa na chochote kile, au adhani kuwa kafikisha Ujumbe Fulani kumbe hajafikisha chochote, na hilo ni jambo muhali katika haki ya Mtume ( S.a.w ) kwani hilo linapingana na Is’ma ( kuhifadhiwa kwake ) katika ujumbe na kufikisha.

Tatu:  Na wapo walioithibitisha hadithi hii na wakasema kuwa ni hoja hadithi ahadi katika Itikadi na wakatafsiri kule kurogwa kwa Mtume ( S.a.w ) ili wathibishe madai yao kuwa ni kurogwa katika mwili wake pasina akili yake na kauli, kauli hizi hazina msingi wowote wa kiakili wala wa kisheria hazitegemewi,na sisi msimamo wetu ni kutokuchukua hadithi ahadi katika mambo ya itikadi . na Allah ndio Mjuzi.

Anasema Sayyid Qutb –Allah amrehemu – katika kitabu chake cha Fii Dhilalil-Qur’an akitafsiri suratil- Falaq “Na shari ya wale wanaopuliza Mafundoni’… Wanaopuliza katika Mafundo ni Wachawi wanaeneza ubaya kwa njia ya kuhadaa Hisia na kuhadaa mishipa, na wao wanafunga fundo kwenye uzi au Kitambaa (Leso) na wanapulizia humo kama kuiga uigaji wa kiuchawi na kuingiza athari kwenye nafsi na kuathiri hisia!

Na uchawi haubadilishi tabia ya Vitu, na wala hauleti hakika nyingine ya kitu, lakini huleta dhana katika Hisia zile anazozitaka Mchawi.

Na huu ndio Uchawi kama ulivyoelezwa na Qur’an katika kisa cha Nabii Mussa katika Surat Twaha aya ya 65- 69:

قالوا يا موسى إما أن تلقي وإما أن نكون أول من ألقى  قال بل ألقوا  فإذا حبالهم وعصيهم يخيل إليه من سحرهم أنها تسعى  فأوجس في نفسه خيفة موسى  قلنا:لا تخف إنك أنت الأعلى  وألق ما في يمينك تلقف ما صنعوا إن ما صنعوا كيد ساحر ولا يفلح الساحر حيث أتى

“Wakasema Ewe Musa ! Je ! Utatupa wewe (Kwanza uchawi wako) au tutakuwa sisi wakwanza kutupa? (Musa) Akasema : “Bali tupeni nyinyi (Kwanza) tahamaki kamba zao na fimbo zao zikaonekana mbele (Musa) kwa uchawi wao, zinakwenda mbio mbio. Basi Musa akatia (akaona) Khofu katika Nafsi yake. Tukasema: “Usiogope! Hakika wewe ndiye utakayekuwa Mwenye Kushinda”  Na kitupe kilicho Mkononi mwako wa kuume  (wa Kulia) kitavimeza walivyovitengeza. Hakika wao wametengeneza hila za Mchawi tu, wala Mchawi hafaulu, (Hafuzu ) Popote afikapo”.

Lakini ulionekana kwa watu – miongoni mwao Musa – kwamba zile fimbo zinatembea mpaka kufikia kiwango cha kuingiza khofu katika nafsi ya Musa, na kama hivi kiukweli Fimbo zao hazikugeuka kuwa nyoka wa kiukweli mpaka ilipomjia Ithibati. Kisha hakika na ukweli  ukawa wazi pale ilipogeuka fimbo ya Mussa kiukweli ikawa nyoka, ikameza zile kamba na fimbo zilizogeuzwa nyoka kiuwongo na   wachawi  .

Na hii ndio tabia ya wachawi kama inavyotakikana tuikubali, na kwa tabia ndio wanawaathiri watu na wanapata hisia kwa mujibu wa vitendo vyao, hisia ambazo zinawatisha na kuwaudhi na kuwaelekeza muelekeo ambao unautaka wachawi na kwa kiwango hiki tunasimama katika kufahamu tabia ya Uchawi na kupuliza katika Fundo..

Nayo ni shari ya Kujilinda kwayo kwa Allah na kuelekea kwake kwa Ulinzi.

Katika mji wa Madina… – Pamesemwa siku nyingi na pamesemwa Miezi  – kwa hakika zimepokelewa Riwaya – baadhi yake ni sahihi lakini hazifiki kiwango cha mutawatir – kuwa Labid Bin A’aswam Myahudi alimroga Mtume (S.a.w) mpaka alikuwa akidhani kuwa amewaingilia wake zake na hali ya kuwa hajawaingilia, na katika Riwaya nyingine …. Mpaka alikuwa Mtume (S.a.w) akidhani kuwa kafanya kitu fulani na ilihali hajafanya chochote, na ulipoletwa uchawi uliokusudiwa – kama ilivyoelezwa katika kuona kwake- na kwamba sura mbili zimeteremshwa ikiwa ni zinguo kwa Mtume (S.a.w) na ule ubaya wa uchawi ukamuondoka.

Na lakini mapokezi yote haya yanakhalifu msingi wa kuhifadhiwa Mtume (S.a.w) kutokufanya makosa katika vitendo na kufikisha, na wala haziwezi kuwa sawa na itikadi ya kiislamu ambayo inatufundisha kuwa kila kitendo katika vitendo vyake Mtume (S.a.w) na kila kauli katika kauli zake ni Sunnah na ni sheria, na pia zinagongana na Qur’ani ambayo inakanusha kuwa Mtume (S.a.w) karogwa, na inawakadhibisha washirikina katika madai yao haya ya uongo. Kutokana na hayo hadithi hizi zinawekwa mbali… na hadithi ahadi hazichukuliwi katika mambo ya itkadi. Na marejeo ni Qur’ani, na kuja kitu kikiwa mutawatiri ni sharti la kukubalika hadithi katika Misingi ya Itikadi. Na mapokezi ya hadithi hizi sio mutawatir, zaidi ya kwamba kushuka kwa sura hizi mbili katika mji wa Makkah ndio kauli yenye nguvu, kitu ambacho kinadhoofisha msingi wa Mapokezi Mengine.

Ndugu yenu Atta bin Khalil Abu Rashta

Maoni hayajaruhusiwa.