Kuingia bwana harusi katika ukumbi wa wanawake

بسم الله الرحمن الرحيم

Swali la Samih Rayhan Abu Maysara:

Assalamu Alaykum Warahmatullah, je kuna uharamu bwana harusi kuwajulisha wanawake kuwa ataingia harusini kwa bi harusi, bi harusi akae na wanawake wengine wote kwa heshima na haya waondoke asibakie yeyote ila maharimu zake (bwana harusi) wanawake wamuombee baraka. Wale wanawake ajnabii wamejitenga kwa haya na heshima wamekaa katika viti vyao, wala hapakutokezea mchanganyiko baina yao na bwana harusi pale alipoingia katika sehemu ile ya hafla? Allah akupe baraka. 

Swali la Al-Khilafah Wa’adullah:

Je inafaa bwana harusi kukaa ubavuni mwa bi harusi wake ili amvishe mapambo. Wakati inaeleweka kwamba wanawake wote wamejihifadhi na wengi wao maharimu, baada ya hapo yule bwana harusi aondoke? 

Swali la Sufyan Qasrawi:

Assalamu Alaykum Warahmatullah Wabarakatuh, Sheikh wetu mkarimu, mimi nina swali nalo ni: Ikiwa utawekwa wakati maalumu wa kufurahi maharim na wakati mwengine maalumu kwa wasiokuwa maharim, je itafaa kwa bwana harusi kuingia ukumbini wakati wanapokuwepo maharim tu? 

Jawabu:

Waalaykum Salam Warahmatullah Wabarakatuh

Hakika maswali yenu matatu yamo katika maudhui moja, kwa hiyo tunayajibu yote kwa pamoja kwa idhini ya Allah:

Tumetangulia kujibu tarehe 6, Jumada Thaniya 1424 sawa na 8, August 2003 juu ya maudhui ya kuchanganyika (wanawake na wanaume) katika kumbi za furaha jawabu ya kina. Na miongoni mwa yaliyomo humo ni haya yafuatayo:

“-Hakika ya mchanganyiko wa wanaume na wanawake ni haramu na dalili zake zimejaa. Maisha ya Waislamu wakati wa Mtume (SAW) na masahaba baada yake yanazungumza jambo hilo. Na haifai mchanganyiko ispokuwa kwa haja ambayo sharia imeikubali na nass ya Kitabu cha Allah au Sunna ya Mjumbe wake  ikapatikana kuhusu haja hiyo, mfano kuuza na kununua, kuunga ukoo… n.k.

Hakuna nass  inayojuzisha mchanganyiko wa wanaume na wanawake katika kumbi za furaha (harusi). Lakini kinachopatikana (katika nass) katika wakati wa Mtume (SAW) na masahaba zake ni kwamba wanawake walikuwa wanakuwa pamoja na bi harusi, wao na yeye peke yao. Na wanaume peke yao. Kwa hiyo mchanganyiko katika kumbi ni haramu bila ya kutofautisha (ghair mustathnaa). Na kilichopatikana pia katika harusi ni kumpeleka mke kwenye nyumba ya mumewe hapo inafaa wampeleke wanaume na wanawake kwenye nyumba ya mumewe kisha wanabaguka wanaume kutokana na wanawake…

Kwa hivyo, kupatikana wanaume na wanawake katika kumbi za furaha bila ya kutengana, yaani katika ukumbi mmoja sio katika kumbi mbili, hilo ni haramu. Na ikiwa tupu ziko wazi kama ilivyoenea sana (siku hizi) katika hali kama hizi basi uharamu unakuwa mkubwa. Na pia kukaa bwana harusi ubavuni mwa bi harusi wake ikawa amezungukwa (bwana harusi) na wanawake maharimu na wasiokuwa maharimu hilo ni haramu, na hasa wakiwa tupu zao ziko wazi, jambo ambalo mara nyingi wanawake huwa hivyo wakiwa wamemzunguka bi harusi siku hizi…

Ama kauli ya kwamba jambo hili ndio limeshazoeleka na kuenea, kauli hiyo hailifanyi la haramu kuwa ni halali. Na ni kauli yenye kurejeshwa kwa mwenyewe (marduudun ‘alaa swaahibih)  kwa vile inapingana na sharia. Bali kuna hadithi zinazowasifu wale wanaoishika vyema dini yao kuwa ni kama mwenye kushika kaa la moto kutokana na mitihani inayomfika Muislamu pindi akishika vyema Uislamu wake. 

قال رسول الله : «يَأْتِي عَلَى النَّاسِ زَمَانٌ الصَّابِرُ فِيهِمْ عَلَى دِينِهِ كَالْقَابِضِ عَلَى الْجَمْرِ»….” انتهى.

Mtume (SAW) amesema: “Watu zitawafikia zama, mwenye kusubiri katika dini yake ni kama mwenye kushika kaa la moto”… Mwisho.

Kwa hiyo, bwana harusi kukaa pamoja na bi harusi wake katika ukumbi wa mchanganyiko wa wanaume na wanawake ni haramu. Na pia kukaa bwana harusi katika ukumbi wa wanawake pamoja na bi harusi wake na wanawake wamewazunguka maharimu na wasio maharimu ni haramu. Na yote hayo yakiambatana na kuwa wazi tupu za wanawake na wamejipamba kuvutia, hilo litakuwa haramu juu ya haramu…

Ama ikiwa katika ukumbi kuna maharimu zake tu (bwana harusi), hapo inafaa kwake kuingia ukumbini na kukaa pamoja na bi harusi wake na pamoja na hao maharimu zake na amvishe mapambo kisha atoke. Baada ya hapo waingie wanawake wengine.

Ufupisho:

  1. Haufai mchanganyiko wa wanaume na wanawake katika kumbi za furaha, sawa ikiwa tupu ziko wazi au zimesitiriwa. Na ikiwa tupu zenyekuharamishwa ziko wazi, basi uharamu unakuwa mkubwa.
  2. Haifai bwana harusi kuingia katika ukumbi wa wanawake ili aketi na bi harusi wake muda wa kwamba wanawake ajnabi wapo hapo ukumbini, hata kama atawaeleza hao wanawake kabla hajaingia ili wajisitiri miili yao, na wasimkurubie bwana harusi, wamkurubie maharimu zake tu… muda wa kwamba wanawake wengine ajnabi katika ukumbi wa furaha wapo wamekaa kwenye viti vyao wanashuhudia, yaani pale ukumbini. Basi hilo halifai.
  3. Inafaa kuingia bwana harusi katika ukumbi wa furaha na kukaa pamoja na bi harusi wake, ukitengwa muda maalumu kwa ajili ya maharimu tu, katika hali ambayo hapatakuwa na yeyote ukumbini wakati anapoingia na anapokaa pamoja na bi harusi wake isipokuwa maharimu zake. Kisha bwana harusi atoke, halafu tena waingie wanawake wengine baada ya kutoka yeye (bwana harusi).

Ndugu yenu Atta bin Khalil Abu Rashta

7, Muharam 1437 – 20, October 2015

Maoni hayajaruhusiwa.