Hijjah Yathibitisha Umoja wa Kimaumbile Kwa Ummah Wetu

ِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ

Waislamu kwa mamilioni kutoka maeneo mbalimbali ulimwenguni tayari wanaendelea kutekeleza ibada ya Hijjah katika mji mtukufu wa Makkah. Ibada hii inatukumbusha wito alioutoa Nabii Ibrahim AS pale alipoamrishwa na Allah SWT kuwatangazia watu kwenda kuhiji katika nyumba tukufu ya Al- Kaaba. Allah Taala anasema:

وَأَذِّنْ فِي النَّاسِ بِالْحَجِّ يَأْتُوكَ رِجَالاً وَعَلَى كُلِّ ضَامِرٍ يَأْتِينَ مِنْ كُلِّ فَجٍّ عَمِيقٍ :

“Na watangazie watu habari za Hijjah, watakujia kwa miguu na (wengine) juu ya kila mnyama aliyekonda(kwa machofu ya safari) wakija kutoka maeneo ya mbali”

(TMQ Hajj:2)

Nabii Ibrahim AS alikuwa katika mji wa Makkah kwa wakati huo uliokuwa jangwa bila ya wakaazi, wala hakumiliki vyombo vya kileo kama vipaza sauti, simu au televisheni ya kupeperushia wito wake. Lakini alitekeleza kwa utiifu mkubwa amri ya Allah Taala bila ya kuhoji. Leo hii tunashuhudia misururu na misafara ya watu kutoka kila pembe ya dunia kuitikia wito huo. Waislamu kutoka makabila, mataifa, mabara tofauti wanakusanyika katika kuitekeleza ibada hii, wote wakiwa kitu kimoja, na kuweka mbali kabisa ikhtilafu zao za kimadhehebu na mitizamo yao katika masuala mbali mbali. Huu ni mfano mzuri na dhihirisho la wazi kwamba umoja wa Waislamu ni jambo linalowezekana. Aidha, inatuonyesha bayana kwamba ni ufahamu wa kimakosa kwamba Waislamu hawawezi kuwa kitu kimoja kwa dalili ya kwamba kuna madhehebu na ikhtilafu nyingi miongoni mwa Waislamu. Huu ni ufahamu batili na haufai kubebwa na Muislamu kwani Allah Taala Amefaradhisha Waislamu wawe kitu kimoja pale aliposema:

وَاعْتَصِمُوا بِحَبْلِ اللَّهِ جَمِيعًا وَلاَ تَفَرَّقُوا

“Shikamananeni na kamba ya Allah (Uislamu) Wala Musifarikiane”

(TMQ Imran: 102)

 Hivyo, maadamu umoja ni faradhi kwa Waislamu basi bila shaka unawezekana kwani Allah Taala hawezi kufaradhisha jambo ambalo haiwezekani kulifikia mwanadamu.

Waislamu huwa lazima kuwa kitu kimoja katika mambo ya kimsingi (Usuulu-ddin) na huruhusiwa kutafautiana katika mambo ya furu’u (matawi). Mambo ya kimsingi ni kama aqeeda, mfano kuamini Mungu Mmoja, Mitume wake, Malaika, Siku ya Malipo, Moto, Pepo na kuamini hata mambo ya kiibada yaliyosibu kwa njia ya mutawatir.

Amma mambo ya furu’u kama namna ya uwekaji wa udhu, kufunga mikono kwenye swala, kuweka ndevu nk. Haya ni mambo ambayo yana ufahamu zaidi ya mmoja, na ndio maana wakapatikana maulamaa waliotangulia mfano Imam Shaafi, Imam Malik, Imam Ahmad bin Hambal nk. ambao walikuja na ijtihadi zao katika mambo haya kwa kutegemea dalili fafanuzi kutoka kwa Mtume wetu SAAW.

Kilichokatazwa kwa Waislamu ni kufarikiana (Firka) kama ilivyokuja katika Ayah وَلاَ تَفَرَّقُوا na maana yake ni kutafautiana katika mambo ya msingi wa dini, mfano kupatikane watu wanaodai kwamba Qur’an haijakamilika , hiyo si ikhtilafu bali ni firka.

Aidha, ikhtilafu/kuikhtalifiana ni jambo ambalo linakubalika kisheria (kwa nidhamu maalumu) na walikhtalifiana maswahaba wakati wa uhai wa Mtume SAAW na baada ya kufa kwake katika mambo mbalimbali ya dini na hili halikuwa chanzo cha mizozo wala migogoro (Rejea kitabu : Nidham-ul Islam, Taqiuddin Annabhani). Lakini kwa bahati mbaya  zilipokuja zama za mporomoko na kushuka kwa kiwango cha elimu kama ilivyo leo katika jamii ya Kiislamu watu wengi wakiwemo baadhi ya walinganizi wakakosa ufahamu huu na badala yake wakawa ni wenye  kulazimisha rai za mambo ya furui walizozibeba na kudhoofisha rai za wengine japo zina dalili za kisheria. Jambo hili ikawa ndio chanzo cha mitafaruku na mizozo, migogoro miongoni mwa jamii ya Kiislamu.

Enyi Waislamu:

Wakati tukiadhimisha masiku kumi matukufu katika mwezi huu mtukufu ni muhimu kufahamu kwamba Waislamu sote ni kitu kimoja, na umoja wetu kikweli utadhihirika chini ya dola la Kiislamu ya Khilafah Rashidah, na dola itapambana na kila fikra ya kiubaguzi imma uzalendo, ukabila, urangi, utabaka, utaifa nk. ambayo itavunja umoja wetu.

Tunawatakia kila la kheri Mahujaji wote

Afisi ya Habari –   Hizb ut- Tahrir Tanzania

03 Dhul Hijjah 1439 Hijri 1439 Hijri    | 14-08- 2018 Miladi

https://hizb.or.tz/

https://www.facebook.com/Hizb-ut-Tahrir-Tanzania

Maoni hayajaruhusiwa.