Vita vikubwa vya Badri (17 Ramadhani Mwaka wa 2 Hijiria)
بِِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ
Mwezi wa Ramadhani licha ya kuwa ni mwezi wa ibada na taqwa lakini pia katika tareekh ya Kiislamu ni mwezi uliojaa matukio ya ukombozi, ujasiri na ushindi. Kuna vita vingi vikubwa vilivyopiganwa katika mwezi huu. Tukio la Vita vya Badr katika tarehe 17 Ramadhani mwaka wa 2 Hijriya ni moja kati ya matukio mashuhuri lisiloweza kusahaulika.
Hivi ni vita vya mwanzo vikubwa baina ya jeshi la Kiislamu na jeshi la makafiri mara baada ya Mtume (SAAW) kusimamisha Dola ya mwanzo ya Kiislamu ndani ya Madinat-ul Munawara.
Ni tukio lililodhihirisha wazi wazi izza ya waumini na serikali yao ya Kiislamu japo kwa wakati ule ilikuwa changa, kadhalika ilikuwa ni dhila ya waziwazi kwa makafiri na viongozi wao. Na zaidi ni kielelezo cha kuwepo na kuendelea mpaka Siku ya Qiyama kwa mapambano baina ya haki na batili, nuru na kiza, na dhulma na uadilifu.
Mtume (SAAW) alitoka Madina yaliyokuwa Makao makuu ya Dola yake ya Kiislamu kwa lengo la kuufuatilia na kuutia mbaroni msafara wa kibiashara wa dola ya maQureish, dola ambayo ndio (kwa wakati ule) iliyokuwa na wapinzani wakubwa wa Waislamu na serikali ya Kiislamu. Dhamira ya Waislamu ilikuwa na lengo la kuandaa mazingira ya vita dhidi ya maQureish, kuwawekea mazingira magumu kiuchumi na kuwaathiri katika njia zao kuu za kiuchumi yaani misafara yao ya kibiashara ya kuelekea kaskazini kwenda As-Sham.
Pamoja nae Mtume (SAAW) kulitoka kikosi cha Waislamu kilichohesabika takriban watu 313 huku akimpa uongozi wa jeshi hilo sahaba mashuhuri Mus’ab bin Umair Al-Abdar, na Madina akimwakilisha uongozi wa muda kwa Abdullah Ibn Ummu Maktoum.
Abu Sufyan, aliyekuwa kwa wakati ule kiongozi miongoni mwa viongozi wa maQureish na mkuu wa msafara wa maQureish alitambua hatari ya njia za Madina. Kwa hivyo, ilimbidi awe makini kwa kufanya ujasusi wa hali ya juu ili kugundua kama kuna ajenda ya kuvamiwa kwa msafara wake. Na alipotambua na kugundua mpango huu wa jeshi la Waislamu kuuvamia msafara huo, kwa haraka sana alimtuma Damdam bin Ghifar akiwa mjumbe maalum kwenda Makka kupeleka taarifa hii ya hatari kwa vigogo wa kiQureish juu ya balaa linalowakabili la kutiwa nguvuni msafara wao, na hivyo kuwataka maQureishi watoe msaada wa kutetea msafara huo kwa kufa na kupona ili mali yao isiingie mikononi mwa maadui zao yaani Waislamu. Damdam bin Ghifari alipofika Makka alipanda juu ya Ka’aba na kunadi:
“Enyi maQureish! Biashara zenu zilizoko na Abu Sufiyan, msafara wake umeshazingirwa na Muhammad na wafuasi wake! Sijui kitakachotokea kwa msafara huo. Msaada! Msaada!”
Kutokana na taarifa hizi maQureishi kwa haraka nao waliandaa jeshi la askari wapiganaji lisilopoungua watu 1,000 lenye zana nzito za kijeshi kuja kupambana na kikosi cha Waislamu cha watu 313 kikiwa na silaha hafifu ikiwemo farasi wawili na ngamia 70. Hii ikiwa na maana kila ngamia mmoja kwa watu watatu na zaidi kikosi hiki cha Kiislamu hakikuwa na lengo la moja kwa moja la vita vikuu dhidi ya jeshi la maQureish bali zaidi kililenga kuvamia na kuushikilia msafara wa kibiashara tu.
Hatimae Abu Sufiyan aliweza kufanikiwa kuuwokoa msafara ule wa kibiashara, na hivyo kutuma tena mjumbe mwengine kwa jeshi la maQureish lililokuwa tayari limeshajiandaa ili kutengua ujumbe wake wa awali. Yaani hali kwa sasa iko salama, msafara umeshasalimika na kwa hivyo hakuna haja tena kuja kupigana vita. Abu Jahl kiongozi wa jeshi la maQureish kwa kiburi na majivuno mara baada ya kufikiwa na ujumbe huu kutoka kwa Abu Sufiyan alipingana na viongozi wenzake wazi wazi na akalazimisha rai yake kwamba lazima vita viendelee kama vilivyopangwa ili kumaliza kidomo domo cha Muhammad (SAAW), wafuasi wake na Dola yao changa ya Kiislamu.
Baada ya kikosi cha Waislamu kupata taarifa hii, Mtume (SAAW) alifanya shura na masahaba zake kuamua kundi lipi katika yale mawili walikabili, jeshi la maQureish kutoka Makka au msafara uliokuwa ukiongozwa na Abu Sufiyan. Rai ya kulifuata jeshi la maQureishi iliwafikiwa na wengi. Kwa hivyo, Mtume (SAAW) na Waislamu hawakuwa na namna ila kukabiliana na maQureish kwa mara ya mwanzo ana kwa ana katika medani ya vita wakiwemo maadui wakubwa wa Waislamu na Uislamu kama Abu Jahl mwenyewe, Utba bin Rabi’ah, Shayba ibn Rabi’ah na wengi wengineo. Huku Mtume (SAAW)akiwaahidi Waislamu ushindi hadi kutaja maeneo watakayoanguka maadui kesho katika medani ya vita. Na hii ikawa bishara ya Nusra ya Allah Ta’ala kwa Mtume Wake (SAAW). Bishara ambayo daima ni ukweli usiobwatika wala kuambulia patupu.
Vita vilianza kwa kufanya mubaraza, yaani kwa kila upande kutowa watu wao mashuhuri kupambana baina yao mbele ya majeshi yao kabla ya mapigano ya jumla jamala kuanza. Katika hatua hii ya awali maQureish walishindwa na kuwapoteza majemadari wao, wakati Ali (RA) alimkata kichwa Al-Waleed, Hamza (RA) nae kumuuwa Shaibah, na Utbah kujeruhiwa vibaya na Ubaidah bin Al Harith (RA) mpaka hapo makafiri tayari waakanza kujawa na khofu na woga.
Mtume (SAAW) aliomba dua ya nusra ya Allah Ta’ala kwa Waislamu hadi kilemba chake kumuanguka, na Allah Ta’ala aliwapa Waislamu nusra kwa kuwateremshia Malaika kuwasaidia Waislamu na sio kupigana kwa niaba yao.
Waislamu walipambana na makafiri kwa ushujaa wa aina yake na kuweka pembeni mafungamano yote isipokuwa Uislamu tu. Umar (RA) alidiriki kumuuwa mjomba wake ‘Ass bin Hisham bin Al-Mughirah na Abu Ubaida (RA) nae akamuuwa baba yake wa kumzaa! Na wakati Musab bin Umair (RA) alipomuona kaka yake ambae bado alikuwa mshirikina kafungwa akiwa mateka kwa Waislamu baada kushindwa vitani, akamsisitiza Answari anaemlinda amfunge imara zaidi kwa sababu mama wa mateka huyo ana utajiri wa kutosha kumkomboa. Yote hayo yalitendeka bila ya kuzingatia kipimo chochote isipokuwa msimamo wa Uislamu na umuhimu wa kuuangamiza Ukafiri.
Waislamu waliweza kuwashinda vibaya maQureish kwa kuwauwa 70 miongoni mwa vigogo vyao na kuwateka pia watu 70. Miongoni mwa vinara vya uadui vilivyouwawa alikuwemo Abu Jahl, Uqba Ibn Muit, Utbah, Shayba na wengine waliokuwa awali maadui wakubwa wa Mtume (SAAW) na Uislamu. Mtume (SAAW) aliwahi kubashiri kwa ushujaa na ujasiri wa hali ya juu kwamba viongozi hawa wa makafiri watachinjwa alipokuwa Makka. Bishara hiyo aliitowa hata kabla ya kusimama serikali ya Kiislamu !
Taarifa za ushindi kwa Waislamu zilin’garisha Madina na kuinua juu haiba ya dola mpya na changa ya Kiislamu katika Bara Arabu yote pamoja na kutia doa na kiza cha idhilali kwa maQureishi na dola yao ya kikafiri. Na kwa hivyo ikatimia ahadi ya Allah Ta’ala ya kuwapa Waislamu Nusra Yake dhidi ya maadui zao na maadui wa Allah Taala maadamu tu Waislamu watasimama kidete kuulingania Uislamu pasina kuregeza misimamo yao.
Tunapolikumbuka tukio hili kubwa ndani ya mwezi huu mtukufu wa Ramadhani inatulazimu kufanya bidii kwa ikhlasi ya kuubeba ulinganizi wa Kiislamu kimfumo kwa lengo la kuushinda kila mfumo na dini kinyume na Uislamu. Hilo ni kwa kusimamisha serikali ya Khilafah, ambayo ndiyo chombo pekee chenye mamlaka na uwezo wa kuandaa nguvu na uwezo wa kweli kwa ajili ya kupambana dhidi ya makafiri na dola zao ulimwengu mzima huku tukiwa na matarajio ya ushindi na nusra ya Allah Ta’ala na kutaraji Radhi Zake pekee. Allah Ta’ala anasema:
هُوَ الَّذِي أَرْسَلَ رَسُولَهُ بِالْهُدَى وَدِينِ الْحَقِّ لِيُظْهِرَهُ عَلَى الدِّينِ كُلِّهِ وَلَوْ كَرِهَ الْمُشْرِكُونَ
“Yeye ndie aliyemtuma Mjumbe Wake kwa Uongofu na Dini ya Haki ili kuidhihirisha (kuifanya iwe juu) ya dini zote hata kama washirikina watachukia!” [TMQ 61:9]
www.hizb.or.tz
https://www.facebook.com/Hizb-ut-Tahrir-Tanzania
13 Ramadhan 1437 AH 18/06/2016 Miladi