Mazingatio Kwa Kauli Ya Mchungaji Dr. Kimaro

بسم الله الرحمن الرحيم

Taarifa za kusimamishwa kazi kwa siku 60 Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) , Usharika wa Kijitonyama Dr. Eliona Kimaro zimeenea kama moto katika nyasi kavu, ikiaminika hatua hiyo ya uongozi wa KKKT dhidi ya Dr. Kimaro ni kutokana na msimamo wa kauli yake ya kweli kwamba vijana wa Kiislamu ni waaminifu zaidi kuliko vijana wa kikiristo, na akaongeza katika matamshi yake kuwa dhana nzima ya uaminifu haipo na imepotea kwa waumini jumla wa dini ya kikiristo wakiwemo pia viongozi na wazee wa kanisa.
Kauli ya Dr. Kimaro inapaswa kubebwa kwa mazingatio na kumfikirisha kila mtu kuanzia Mchungaji mwenyewe, wakiristo jumla na viongozi wao pia na Waislamu.
Kwa upande wa Mchungaji mwenyewe Dr. Kimaro kauli yake imfikirishe na kumpa mazingatio kwa upana kwamba dini ya Uislamu, licha ya kuangushwa dola yake tangu mwaka 1924 ambayo ndio kinga na kielelezo cha Uislamu, pia kuwepo kampeni kali ya kupigwa vita Uislamu, na Waislamu kuchanganyikiwa hapa na pale, bado na daima itakuwa thabiti kinyume na ukiristo kutokana na msingi wake (aqida), vipimo vyake, ufafanuzi wa nidhamu zake nk. Na hayo ndio yanayofanya dini hii kubakia na uhai licha ya mazingira magumu inayopitia leo.
Msingi wa imani (aqida) ya Kiislamu uko wazi, mwepesi kueleweka na unakinaisha akili. Kwamba yupo Muumba wa kila kitu, ambaye ni Mwenyezi Mungu, Mmoja, hana mshirika, Yeye yupo milele na hakuumbwa, Kwa kuwa lau kaumbwa, basi huwa kakosa sifa ya kuwa Mwenyezi Mungu, na haiwezekani kukutana pamoja sifa mbili za kuwa Kiumbe na kuwa Mungu.
Vipimo vya matendo katika Uislamu ni ‘halali’ na ‘haramu’ navyo ni kutoka kwa Mwenyezi Mungu kupitia wahyi kwa Mtume SAAW na sio kwa akili ya yoyote. Hakuna mabadiliko juu ya vipimo hivyo, kwa aina ya watu wala zama fulani. Kwa hivyo, hakuna wakati au zama ambapo Uislamu utahitaji marekebisho (reformation) au maboresho fulani. Na kimsingi vipimo hivyo, vimekuja kumlenga mwanadamu ambaye katika uasili wake kamwe habadiliki.
Amma kwa upande wa nidhamu zake (systems) Uislamu ukaweka wazi uchumi wake, jamii yake, utawala, elimu, siasa za ndani na nje nk. Na ukawa bayana kuwa msimamiaji na mlinzi wa imani na mtekelezaji wa nidhamu hizo kwa upana ni utawala (Khilafah).
Uimara, uthabiti na ufafanuzi huo wa Uislamu ndio huzalisha vijana wenye walau kiwango cha uaminifu hata katika mazingira machafu yasio ya Kiislamu leo. Jambo hili la ufahamu thabiti wa Uislamu limfikirishe Mchungaji Kimaro na wakiristo wote, tukimnasihi hususan Dr. Kimaro na wote jumla kuukubali na kuingia katika Uislamu na kuachana na dini ya Ukiristo. Quran Tukufu inasisitiza mwito huo kwao:
وَإِذْ قَالَ عِيسَى ابْنُ مَرْيَمَ يَا بَنِي إِسْرَائِيلَ إِنِّي رَسُولُ اللَّهِ إِلَيْكُمْ مُصَدِّقًا لِمَا بَيْنَ يَدَيَّ مِنَ التَّوْرَاةِ وَمُبَشِّرًا بِرَسُولٍ يَأْتِي مِنْ بَعْدِي اسْمُهُ أَحْمَدُ فَلَمَّا جَاءَهُمْ بِالْبَيِّنَاتِ قَالُوا هَذَا سِحْرٌ مُبِينٌ (الصف: 6). ).
”Na kumbuka Isa bin Mariamu aliposema: Enyi Wana wa Israili! Hakika mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu kwenu, ninayethibitisha yaliyo kuwa kabla yangu katika Taurati, na ni mwenye kuwabashiria kuja Mtume atakayekuja baada yangu; jina lake ni Ahmad! Lakini alipowaletea hoja zilizo wazi, walisema: Huu ni uchawi ulio dhaahiri!” (Surat Ass’af : 6)
وَمَنْ أَظْلَمُ مِمَّنِ افْتَرَى عَلَى اللَّهِ الْكَذِبَ وَهُوَ يُدْعَى إِلَى الإِسْلاَمِ وَاللَّهُ لاَ يَهْدِي الْقَوْمَ الظَّالِمِينَ (الصف: 7
”Na ni nani mwenye kudhulumu zaidi kuliko yule anayemzulia Mwenyezi Mungu uwongo, naye anaitwa kwenye Uislamu? Na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu madhaalimu” (Surat Ass’af : 7)
قُلْ يَا أَهْلَ الْكِتَابِ تَعَالَوْا إِلَى كَلِمَةٍ سَوَاءٍ بَيْنَنَا وَبَيْنَكُمْ أَلاَّ نَعْبُدَ إِلاَّ اللَّهَ وَلاَ نُشْرِكَ بِهِ شَيْئًا وَلاَ يَتَّخِذَ بَعْضُنَا بَعْضًا أَرْبَابًا مِنْ دُونِ اللَّهِ فَإِنْ تَوَلَّوْا فَقُولُوا اشْهَدُوا بِأَنَّا مُسْلِمُونَ (آل عمران: 64).
”Sema: Enyi Watu wa Kitabu! Njooni kwenye neno lilio sawa baina yetu na nyinyi: Ya kwamba tusimuabudu yeyote ila Mwenyezi Mungu, wala tusimshirikishe na chochote; wala tusifanyane sisi kwa sisi kuwa Waola Walezi badala ya Mwenyezi Mungu. Na wakigeuka basi semeni: Shuhudi- eni ya kwamba sisi ni Waislamu. ” (Surat Imran : 64)
Na lau kama Mchungaji Dr. Kimaro na wengine hawajawa tayari, kwa sababu moja au nyengine, basi jambo hilo limpe yeye na wengine chachu na msukumuo mpya wa kutafiti udhati wa Uislamu kwa insafu na uadilifu, nasi tuko tayari kumpa yeye na yoyote kila msaada unaohitajika katika utafitti wao ili baada ya hapo wasilimu, au walau kuungalia Uislamu kwa jicho la uadilifu lililo kando na propaganda za kiuadui za kimagharibi.
Amma kwa upande wa mazingatio kwa viongozi na wafuasi jumla wa kanisa , kauli ya Dr. Kimaro sio ya kubezwa wala kuifanyia hasira, bali ni kauli ya kutafakari na kuleta mazingatio mapana. Kwa kuwa jambo hilo liko wazi. Leo tunashuhudia viongozi mbalimbali wa makanisa wakitenda vitendo vya kimaajabu kwa jina la miujuza ili kutapeli wafuasi wao, tunatarajia viongozi hao wanatoa funzo au muongozo gani kwa wafuasi wao kuhusu uaminifu?
Tabia ya viongozi wa makanisa kutokua waaminifu sio tu ni kauli ya Dr. Kimaro, bali ni kauli ya Muumba aliyotahadharisha miaka 1400 iliyopita. Quran Tukufu inakumbusha:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِنَّ كَثِيرًا مِنْ الأَحْبَارِ وَالرُّهْبَانِ لَيَأْكُلُونَ أَمْوَالَ النَّاسِ بِالْبَاطِلِ وَيَصُدُّونَ عَنْ سَبِيلِ اللَّهِ
”Enyi mlioamini! Hakika wengi katika makuhani na wamonaki wanakula mali za watu kwa batil na wanazuilia Njia ya Mwenyezi Mungu….” (Surat Tawba : 32)
Viongozi wa makanisa waache vitendo vya utapeli, na utapeli mkubwa ni kubakia katika dini iliyojengwa juu ya msingi wa kitapeli, na hivyo kuendelea kuzalisha utapeli.
Amma kwa upande wa Waislamu, kauli ya Dr. Kimaro isiwape kichwa bali iwafikirishe zaidi kuona thamani na uthabiti wa dini yao Uislamu, kuendelea kushikamana nao kiukweli kiutekelezaji, kuusoma na kuwalingania wengine waingie. Waislamu waone leo hata katika kiwango cha kibinafsi Uislamu wao umeweza kuhisika ilhali upeo wa kuhisika athari ya Uislamu ni pale Uislamu unapokua umeshika hatamu katika maisha, yaani utawala. Basi jee katika mazingira mazuri ya Kiislamu hali ingekuwaje?
Hivyo, Waislamu wafanye kazi ipasavyo kwa njia ya Mtume SAAW ya mgongano wa kifikra na kisiasa isiyohusisha nguvu, silaha wala mabavu ili kuweza kuutawalisha Uislamu kwa kuanzia katika ulimwengu wa Kiislamu na kuenea maeneo mengine mashariki na magharibi.
Risala ya Wiki No. 150
08 Rajab1444 Hijri / 30 Januari 2023 Miladi
Afisi ya Habari – Hizb ut- Tahrir Tanzania

Maoni hayajaruhusiwa.