Kila Kilichoharamishwa kwa Watu Mauzo Yake pia ni Haramu
بسم الله الرحمن الرحيم
Silsila ya Maswali Yaliyowasilishwa kwa
Amiri wa Hizb ut Tahrir
Sheikh Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah katika Ukurasa Wake wa Facebook
Swali:
Assalamu Alaikum Wa Rahmatullah Wa Barakatuh,
Mwenyezi Mungu akulinde, ewe Sheikh wetu, na awanufaishe wengine kupitia wewe na elimu yako.
Nilipewa kazi (mwakilishi wa mauzo) kwa kampuni inayouza bidhaa za vipodozi na manukato; baadhi ya vitu vina asilimia tofauti tofauti ya pombe (cologne, ambayo ina viwango vya juu vya pombe ya ethyl, na bidhaa zilizo na ethyl, methyl, na pombe ya isopropyl, kama vile manukato na vipodozi).
Swali: Je, inajuzu kwangu kufanya kazi kama mwakilishi wa mauzo? Vile vile, je, inajuzu kwangu kufanya kazi ndani ya kampuni hii katika nyanja nyingine isiyokuwa mauzo, kwa mfano, kazi ya kiidara?
Jazak Allah Khair
Jibu:
Wa Alaikum Assalam Wa Rahmatullah Wa Barakatuh
Kuanza, naelewa kuwa unauliza kuhusu kufanya kazi katika kampuni zilizoundwa kulingana na msingi sahihi na sio kufanya kazi katika kampuni zisizo sahihi. Jibu la swali hili ni kama ifuatavyo:
1- Hukmu ya kufanya kazi kama mwakilishi wa mauzo katika kampuni inayouza baadhi ya bidhaa zilizoharamishwa (manukato na vipodozi vyenye pombe ya ethyl…n.k.):
Jambo hili tumelizungumzia katika vitabu vyetu na tumelibainisha kuwa ni haramu. Imeelezwa katika kitabu, Shakhsiya ya Kiislamu, katika sura, “Kila Kilichoharamishwa kwa Watu Mauzo Yake pia ni Haramu”:
[Kuna vitu ambavyo Mwenyezi Mungu ameviharamisha kuliwa, kama nyama mfu, na vitu alivyoharamisha Mwenyezi Mungu kuvinywa, kama vile pombe, na vitu alivyoharamisha Mwenyezi Mungu kuviabudu, kama masanamu na vitu ambavyo Mwenyezi Mungu ameharamisha kumiliki, kama masanamu, na vitu ambavyo yeye (swt) ameharamisha kuvitengeza, kama masanamu. Mambo haya yametajwa katika nususi za Shariah katika Aya na Hadith zinazoviharamisha. Vitu alivyoviharamisha Mwenyezi Mungu kwa watu katika vile vilivyoharamishwa na andiko la Shariah, ima iwe ni haramu kula au kunywa au vyenginevyo; uuzaji wake ni haramu kwa sababu ya kuharamishwa thamani yake. Kutoka kwa Jabir kwamba alimsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) akisema
«إِنَّ اللَّهَ وَرَسُولَهُ حَرَّمَ بَيْعَ الْخَمْرِ وَالْمَيْتَةِ وَالْخِنْزِيرِ وَالْأَصْنَامِ. فَقِيلَ: يَا رَسُولَ اللَّهِ، أَرَأَيْتَ شُحُومَ الْمَيْتَةِ فَإِنَّهَا يُطْلَى بِهَا السُّفُنُ، وَيُدْهَنُ بِهَا الْجُلُودُ، وَيَسْتَصْبِحُ بِهَا النَّاسُ؟ فَقَالَ: لَا، هُوَ حَرَامٌ. ثُمَّ قَالَ رَسُولُ اللَّهِ ﷺ عِنْدَ ذَلِكَ: قَاتَلَ اللَّهُ الْيَهُودَ، إِنَّ اللَّهَ لَمَّا حَرَّمَ شُحُومَهَا جَمَلُوهُ ثُمَّ بَاعُوهُ فَأَكَلُوا ثَمَنَهُ»
“Mwenyezi Mungu na Mtume wake wameharamisha uuzaji wa pombe, nyama mfu, nguruwe na masanamu.” Akaulizwa: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, wasemaje kuhusu mafuta ya nyama mfu, kwa hutumiwa kukarabati masafina, kulainisha ngozi, na kutengezea mafuta ya taa? Yeye (saw) akasema: Hapana, ni haramu. Kisha Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) akasema: “Mwenyezi Mungu awalaani Mayahudi! Pindi Mwenyezi Mungu alipowaharamishia mafuta ya nyama mfu, waliyayeyusha, kisha wakayauzwa na kula thamani yake.” [Imesimuliwa na Al-Bukhari]. Neno “Jammaluh” linamaanisha waliyayeyusha.
Kutoka kwa ibn Abbas kwamba Mtume (saw) amesema:
«قَاتَلَ اللَّهُ الْيَهُودَ ثَلَاثاً، إِنَّ اللَّهَ حَرَّمَ عَلَيْهِمُ الشُّحُومَ فَبَاعُوهَا وَأَكَلُوا أَثْمَانَهَا، وَإِنَّ اللَّهَ إِذَا حَرَّمَ عَلَى قَوْمٍ أَكْلَ شَيْءٍ حَرَّمَ عَلَيْهِمْ ثَمَنَهُ»
“Mwenyezi Mungu awalaani Mayahudi! Alisema haya mara tatu. Pindi Mwenyezi Mungu alipowaharamishia mafuta (ya nyama mfu); waliyauzwa na kula thamani yake. Pindi Mwenyezi Mungu anapowaharamishia watu ulaji wa kitu, huwaharamishia ulaji wa thamani yake vilevile.” [Imesimuliwa na Al-Bukhari] Mwisho.
Hivyo basi, kufanya kazi katika nyanja hii ni haramu.
2- Ama kuhusu kazi ya kiidara katika kampuni ambayo biashara yake inajumuisha uuzaji vitu vilivyoharamishwa, mambo haya yanapaswa kuzingatiwa:
– Ikiwa kazi ya kiidara inahusiana moja kwa moja na uuzaji wa nyenzo zilizoharamishwa, kama vile kufanya kazi katika utayarishaji uagizaji unaohusiana na uuzaji wa nyenzo zilizoharamishwa, au mfano wake, basi kazi hii ya kiidara ni haramu kwa sababu inahusishwa na kazi iliyoharamishwa, ambayo ni uuzaji wa nyenzo zilizoharaishwa.
– Lakini ikiwa kazi ya kiidara haihusiani na uuzaji wa nyenzo zilizoharamishwa, kwa hiyo si katika kazi yako ya kiidara kuandaa maombi ya uuzaji wa nyenzo zilizoharamishwa au mfano wake. Kazi hii ya kiidara haijaharamishwa hata ikiwa ni katika kampuni ambayo biashara yake ni uuzaji wa nyezo za haramu, kwa sababu wewe, katika hali hii, hufanyi kitendo kilichoharamishwa.
Hata hivyo, mtu kuchunga Dini yake sio tu kwa kujiepusha na yale yaliyoharamishwa, bali hata kutokana na baadhi ya vitu vinavyoruhusiwa kwa kuhofia kwamba kuna kitu kilicho haramishwa karibu navyo. Maswahaba wa Mtume (saw) walikuwa wakijiweka mbali na milango kadhaa ya vilivyoruhusiwa (mubah), kwa kuhofia kuvikaribia vilivyoharamishwa. Imesimuliwa kutoka kwa Mtume (saw) kuwa Yeye amesema:
«لَا يَبْلُغُ العَبْدُ أَنْ يَكُونَ مِنَ المُتَّقِينَ حَتَّى يَدَعَ مَا لَا بَأْسَ بِهِ حَذَراً لِمَا بِهِ البَأْسُ» “Mja hatafikia kuwa miongoni mwa wachaMungu mpaka awache lile ambalo halina madhara kwake kwa kuchelea lile lenye madhara kwake.”
At-Tirmidhi ameipokea na akasema hii ni Hadith Hassan. At-Tirmidhi pia ametoa, na akasema ni Hadithi Hassan Sahih, kupitia kwa Al-Hasan bin Ali, Mwenyezi Mungu amuwiye radhi, ambaye amesema: Nimeyahifadhi katika kumbukumbu yangu maneno haya ya Mtume wa Mwenyezi Mungu:
«دَعْ مَا يَرِيبُكَ إِلَى مَا لَا يَرِيبُكَ»“Acha lenye kukutia shaka kwa lile lisilokutia shaka.”
Kwa hivyo, ni bora kwa muulizaji, na bora kwa Dini yake, kujiepusha na kufanya kazi na makampuni kama hayo na kutafuta kazi ambayo atapata riziki nzuri, na Mwenyezi Mungu (swt) huwafungulia njia ya kutokea wale wamchao Yeye:
[وَمَنْ يَتَّقِ اللَّهَ يَجْعَلْ لَهُ مَخْرَجاً * وَيَرْزُقْهُ مِنْ حَيْثُ لَا يَحْتَسِبُ وَمَنْ يَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّهِ فَهُوَ حَسْبُهُ إِنَّ اللَّهَ بَالِغُ أَمْرِهِ قَدْ جَعَلَ اللَّهُ لِكُلِّ شَيْءٍ قَدْراً]
“Na anaye mcha Mwenyezi Mungu humtengezea njia ya kutokea * Na humruzuku kwa jiha asiyo tazamia. Na anaye mtegemea Mwenyezi Mungu Yeye humtosha. Hakika Mwenyezi Mungu anatimiza amri yake. Mwenyezi Mungu kajaalia kila kitu na kipimo chake.” [At-Talaq: 2-3].
Nataraji kwamba hili linatosheleza na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi Zaidi, Mwingi wa Hekima.
Ndugu Yenu,
Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah
23 Shawwal 1443 H
23/5/2022 M
Link ya jibu hili kutoka kwa ukurasa wa Amiri wa Facebook.
Maoni hayajaruhusiwa.