Uongofu na Upotofu katika Elimu ya Usul (Misingi)

بسم الله الرحمن الرحيم

Swali:

Bismillah ar-Rahman ar-Rahim

Swali kwa Sheikh wetu katika Shakhsiya Juzuu ya Tatu ukurasa wa 301 msitari wa tatu na wa pili unasema: ama matagaa (furu’) hukadiriwa kutoyafuata kuwa ni uovu basi hivyo haiitwi uongofu, niliambiwa kwamba neno “upotofu” linapaswa kuwekwa badala ya neno “uongofu.” Kwa hivyo je! Neno hili hapa limejitokeza kwa makosa? Asante.

Jibu:

Waaleykum salaam wa rahmatullah wa rahmatullah wa barakatuh,

Sehemu ambayo unaiashiria kutoka kwa kitabu cha Shakhsiya ya Kiislamu, Juzuu ya Tatu, imekuja katika mlango “Kila Ijma’ isipokuwa Ijma’ ya Maswahaba sio dalili ya kisheria”, na nakunukulia yale yanayohitajika ili kulijibu swali lako:

(… Ama kuhusu ijma’ ya Ummah, na ijma’ ya Ahl ul-Hal wa al-‘Aqd, na ijma’ ya Mujtahidina, hakika walisema kwamba ijma’ ya Ummah ni hoja ya kisheria, na wakatumia kama dalili ya hilo, maneno ya Mwenyezi Mungu (swt):

﴾وَمَنْ يُشَاقِقِ الرَّسُولَ مِنْ بَعْدِ مَا تَبَيَّنَ لَهُ الْهُدَى وَيَتَّبِعْ غَيْرَ سَبِيلِ الْمُؤْمِنِينَ نُوَلِّهِ مَا تَوَلَّى وَنُصْلِهِ جَهَنَّمَ وَسَاءَتْ مَصِيراً﴿

Na anaye mpinga Mtume baada ya kumdhihirikia uwongofu, na akafuata njia isiyo kuwa ya Waumini, tutamuelekeza aliko elekea, na tutamuingiza katika Jahannamu. Na hayo ni marejeo maovu. [An-Nisaa: 115] na upande wa utumiaji aya hii kama hoja ni kwamba Mwenyezi Mungu (swt) ameonya dhidi ya kufuata njia nyingine isiyokuwa njia ya waumini, na lau kama hilo halingekuwa limeharamishwa, asingeonya dhidi yake, na haingefaa kulikusanya katika onyo kwa jambo lililokatazwa ambalo linampinga Mtume (SAW),  kama vile haifai kukusanya baina ya ukafiri na kula mkate ambapo inaruhusiwa, Kwa hivyo kufuata njia nyengine isiyokuwa ya waumini ni marufuku, na ikiwa ni marufuku kufuata zaidi ya njia yao, basi njia yao lazima ifuatwe; kwa sababu hakuna machaguo mengine, maana yake hakuna upatanishi kati yazo.  Na ufaradhi wa kufuata njia yao unawajibisha kwamba ijma ya ummah ni dalili; kwa sababu njia ya mtu ni kile anachokichagua katika kauli au kitendo au imani. Jibu la hii ni kutoka pande tatu:

Ya kwanza: Aya, hata kama imekatikiwa katika kuthubutu kwake (Qati’ thubut) lakini maana yake si ya kukatikiwa (Dhanni al-Dalalah), hivyo haiswihi kuwa ni dalili kwamba ijma’ ya Ummah ni dalili ya kisheria; Kwa sababu ni lazima ithubutu kuwa ni dalili ya kisheria kwa dalili iliyokatikiwa; Kwa sababu ni katika usul, hivyo dalili isiyo ya kukatikiwa haitoshelezi kwake.

Ya pili:_Uongofu katika aya hiyo unamaanisha dalili ya upweke wa Mwenyezi Mungu (swt) na Utume wa Muhammad (saw) wala haimaanishi hukmu ya sheria; Kwa sababu uongofu katika usul ni kinyume cha upotofu. Ama kwa matagaa, hukadiria kutoyafuata kuwa ni uovu,_  kwa hivyo haiitwi kuwa ni uongofu. Ama njia ya waumini ambayo wanapaswa kuifuata, ni ile wanayopitia waumini, nayo ni Tawhid (imani ya Mungu mmoja), na sio lazima kuwafuata katika mambo ya mubah (yanayoruhusiwa), na sio lazima kuharamisha kila kitu kilicho halifu njia yao, bali hilo husadikishwa kwa sura moja, ambayo ni ukafiri na mfano wake, miongoni mwa yale ambayo hayana ikhtilafu katika usul. Na yale yanayoonyesha kuwa njia ya waumini lazima ifuatwe kwa yale ambayo wamekuwa waumini wakiyafuata, ni kwamba aya hiyo iliteremka kwa mtu aliyeritadi, na sababu ya kuteremka aya hiyo inafafanua maudhui ambayo iliteremka kwayo, hata kama inajumuisha kila kitu kinachotabikika juu yake maudhui haya, hivyo basi aya hiyo ni maalum kwa maudhui ya kuritadi, wala haijumlishi kila njia kwa waumini.) Mwisho wa nukuu kutoka kwa kitabu cha Shakhsiya ya Kiislamu.

Na ili kulifafanua jibu la swali lako: Je! Ni kama ilivyokuja katika andiko hapo juu (haiitwi uongofu) au kama ilivyokuja katika msemo wa rafiki yako (haiitwi upotofu), hapana budi kuiweka wazi maana ya neno (uongofu):

1- Uongofu katika usul unamaanisha aqeeda (itikadi), yaani kumwamini Mwenyezi Mungu, Mitume wake, Vitabu vyake … nk, na kinyume cha uongofu ni upotofu ..

2- Andiko la aya hiyo linathibitisha hilo, kwani Mwenyezi Mungu amekwisha muonya mtu ambaye hayuko kwenye uongofu kwa Jahannam na ni marejeo maovu yaani, yule ambaye hayuko kwenye uongofu yeye ni kafiri … uongofu ni itikadi ya Kiislamu na sio hukmu za kisheria, na hivyo kutofuata uongofu huo ni ukafiri, yaani upotofu, lakini kutofuata hukmu ya Sharia ni uovu.

3- Hili pia linathibitishwa na sababu ya kuteremka aya hiyo tuliyoitaja awali, ambapo ni kuwa iliteremka kwa mtu aliyeritadi na inatumika kwa kila mtu anayeritadi, na kwa hivyo uongofu katika aya hiyo ni aqeeda, kwa sababu yule aliyeritadi hayuko katika uongofu, yaani, yeye ni kafiri, kwa hivyo uongofu ni aqeeda ya Kiislamu.

4- Kutokana na yaliyo tangulia, suala ni kama ifuatavyo:

A- Kwamba yeyote anayebainikiwa wazi na uongofu, yaani aqeeda ya Uislamu, kisha akampinga Mtume na kufuata njia isiyokuwa ya waumini mbali na kumpwekesha Mwenyezi Mungu na imani, basi yeye ni kafiri aliyepotea na ataingizwa Jahannam na ni marejeo maovu yalioje hayo, yaani uongofu ni kufuata njia ya waumini, yaani imani waliyo nayo. Na kinyume cha uongofu katika maana iliyotajwa ni upotofu.

B – Ama kufuata hukmu za kisheria (matagaa), huo sio uongofu uliokuja katika aya hiyo tukufu, bali hayo ni matendo mema na kinyume chake ni uovu.

C- Na hii inamaanisha kuwa kufuata usul, yaani aqeeda, ndio uongofu na kutofuata ni upotofu … na kufuata matagaa ni katika matendo mema na kutofuata ni uovu.

5- Sasa tulizingatie andiko:

(Uongofu katika aya hiyo unamaanisha dalili ya upweke wa Mwenyezi Mungu na utume wa Muhammad (saw) wala haimaanishi hukmu ya kisheria; kwa sababu uongofu katika usul kinyume chake ni upotofu.

Ama matagaa hukadiriwa kutoyafuata kuwa ni uovu, basi haiitwi uongofu.), na kama unavyoona andiko hilo liko katika sentensi mbili:

Ya kwanza: huitwa kuacha kufuata usul yaani imani (upotofu)… na haiitwi kuacha kufuata usul yaani imani (uongofu)…

Pili: huitwa kuacha kufuata matagaa yaani hukmu za sheria (uovu)… na huitwa kufuata matagaa yaani hukmu za sheria (tendo jema)…

Kama unavyoona andiko hilo liko wazi katika sentensi ya kwanza… ama sentensi ya pili kipande cha kwanza kiko wazi, kuacha kufuata matagaa ni uovu… lakini sisi katika kipande cha pili tumetumia dhamiri hivyo tukasema (haiitwi uongofu juu yake), na hufahamika kutokana na muktadha kuwa dhamiri hapa inarudi katika (kufuata) kwa sababu sisi katika kipande cha kwanza cha sentensi tumetaja (kuacha kufuata), na hivyo kipande cha pili kinakuwa (kufuata), hivyo basi dhamiri katika (juu yake) inarudi katika (kufuata) yaani hivi: (basi haiitwi kufuata matagaa uongofu) na kwa hilo neno (uongofu) hapa ni sahihi, na sio kama alivyosema rafiki yako (upotofu).

Na hivyo maana ya sentensi ya pili inakuwa hivi: (Ama matagaa hukadiriwa kutoyafuata ni uovu wala haiitwi kufuata mataga ni uongofu)

Nataraji kuwa hili limetosheleza na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi Zaidi Mwingi wa Hekima.

Ndugu yenu,

Ata bin Khalil Abu Rashtah

04 Safar 1442 H

Sawia na 21/09/2020 M

Link ya Jibu hili kutoka katika ukurasa wa Amiri (Mwenyezi Mungu amhifadhi) wa Facebook

Link ya Jibu hili kutoka katika ukurasa wa Amiri (Mwenyezi Mungu amhifadhi) wa wavuti

Maoni hayajaruhusiwa.