Ijmaa’ ni Hadith ambayo Maswahaba Hawakuisimulia
بسم الله الرحمن الرحيم
Swali:
Assalamu Alaikum wa Rahmatullahi wa Barakatuh Sheikh Wetu, Mwenyezi Mungu akufungulie mikononi mwako, akubali utiifu wako, na atuharakishie nusra na tamkini. Nina swali kuhusu kuvua kutoka kwa Ijmaa’ ya Maswahaba kwa dalili kutoka katika Qur’an na Sunnah; kama ilivyo kuja katika Shakhsiya ya Kiislamu, Juzuu ya Tatu Kwamba ile inayo chukuliwa kuwa ni ijmaa ya Maswahaba ni ijmaa yao pekee kwamba hukmu fulani ni hukmu ya Kisheria, kwa kuwa inaonyesha kuwepo kwa dalili ya Kisheria ya hukmu hii, na kwamba wameisimulia hukmu hii lakini hawakuisimulia dalili yake. Kwa kuwa ijmaa inadhihirisha dalili ambayo hawakuisimulia, basi ni kwa nini tunavua kutoka kwayo kwa dalili kutoka katika Qur’an na Sunnah? Kwa mfano, katika kitabu, Al Amwal (Mali katika Dola ya Kiislamu), zaka ya kondoo iko katika Sunnah na ijmaa ya Maswahaba, vilevile katika kitabu Nidhamu ya Kijamii katika Uislamu kuhusu talaka asili ya uhalali wake ni Qur’an na Sunnah na Ijmaa ya Maswahaba, hivyo ni kwa nini tunavua kutoka kwa Ijmaa ya Maswahaba, Mwenyezi Mungu awe radhi nao, kwa dalili kutoka katika Qur’an au kutoka katika Sunnah? Mwenyezi Mungu akulipe kheri na samahani kwa swali langu refu.
Jibu:
Wa Alaikum Assalam wa Rahmatullahi wa Barakatuh,
Mwenyezi Mungu akubariki kwa dua zako kwetu. Hili hapa ndilo jibu:
1- Ufafanuzi wa Ijmaa’: Imekuja katika kitabu, Shakhsiya ya Kiislamu, Juzuu ya Tatu: (… Ijmaa’ kwa istilahi ya wanazuoni wa Misingi ya Fiqh (Al-Usoul) ni itifaki ya pamoja kuwa hukmu ya tukio fulani ni hukmu ya Kisheria… Hivyo ile inayo chukuliwa kuwa ni Ijmaa’ ya Maswahaba ni ijmaa yao pekee kuwa hukmu fulani ni hukmu ya Kisheria, kwani inaonyesha kuwepo kwa dalili ya Kisheria ya hukmu hii, na kwamba wameisimulia hukmu lakini hawakuisimulia dalili yake.)
2- Yaani, Maswahaba walijifunza jambo kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) na badala ya kutufikishia Sunnah ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) hadi kwetu kupitia simulizi (riwaya) kutoka kwake, walitufikishia hili kupitia ijmaa yao, yaani ijmaa yao ilichukua nafasi ya ufikishaji Sunnah… hivyo basi ijmaa ya Maswahaba, Mwenyezi Mungu awe radhi nao, inafichua kwamba kuna dalili, yaani, inafichua kwamba kuna Sunnah ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) ambayo haikufikishwa kwetu kama andiko (nas) kupitia simulizi, bali ijmaa ya Maswahaba juu ya hukmu yake ikafikishwa kwetu… ijmaa imechukua nafasi ya dalili kutoka katika Sunnah ambayo haikusimuliwa.
3- Hivyo, kama tunavyo vua kutoka katika Ayah au hadith au kutoka katika hadith na hadith, pia huvua kutoka katika Ayah kwa Ijmaa’ au hadith kwa Ijmaa’, kwa sababu Ijmaa’ ni hadith ambayo haikusimulia na Maswahaba bali waliifikisha tu hukmu kama tulivyo onyesha juu, hivyo, Ijmaa’ ni hadith ambayo haikusimuliwa.
4- Kitu kimoja ambacho ni muhimu kuzingatia ni kuwa, ufikishaji wa Ijmaa ya Maswahaba juu ya hukmu fulani pamoja na dalili nyengine kutoka katika Qur’an na Sunnah hutilia nguvu na kuthibitisha hukmu hiyo, kwa sababu hukmu iliyo na dalili katika Ijmaa ya Maswahaba hairuhusiwi kufutwa; kwa sababu Ijmaa’ ilitokea baada ya Mtume (saw), na ufutaji wake hauwezi kuwa isipokuwa kupitia dalili, na kwa kuwa Ijmaa’ ni baada ya kifo cha Mtume (saw) na kisha kukatizwa ufunuo (Wahyi), hakuna tena dalili ya kufuta Ijmaa’… Hiyo ndio sababu tunasema kwamba uwepo wa Ijmaa’ juu ya hukmu maalum inathibitisha na kutilia nguvu hukmu hiyo kwa sababu kufutwa kwake haiwezekani.
5- Hitimisho ni kuwa uvuaji kutoka kwa hadith na Ijmaa’ ni kama uvuaji kutoka kwa hadith na hadith nyengine, na uvuaji kutoka kwa dalili zaidi ya moja, hususan Ijmaa’ hutulia nguvu na kuthibitisha hukmu hiyo.
Nataraji hili litatosheleza, na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi Zaidi na Mwingi wa Hekima.
Nataraji hili litatosheleza, na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi Zaidi na Mwingi wa Hekima.
Ndugu yenu,
Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah
8 Dhul Hijah 1441 H
29/07/2020 M
Maoni hayajaruhusiwa.