Uislamu Uko Mbali Na Vitendo Vya Ugaidi
بسم الله الرحمن الرحيم
Mnamo mwaka tarehe 11 Machi 2002 aliyekuwa Raisi wa Marekani George Bush alitangaza kumakinisha kampeni kubwa ya kulimwengu iliyojulikana kama “Vita dhidi ya Ugaidi”.
Sehemu ya hotuba yake ilisomeka hivi:
‘Marekani imekusudia kuingia katika hatua ya pili vita dhidi ya ugaidi, Marekani inahimiza na kutarajia kuungwa mkono na serikai zote duniani kusaidia kuondoa viashiria vya ugaidi ambavyo vinahatarisha nchi zao na amani ya ulimwengu’
Hilo ndio tangazo la kampeni chafu na thakili iliyoacha na kuendelea kueneza makovu na maumivu kwa Umma wa Kiislamu. Punde baada ya tangazo hilo sehemu kubwa katika dunia ikazidi kushuhudia uadui mkubwa na wa wazi zaidi dhidi ya Uislamu na Waislamu. Ikapelekea nchi kama vile Iraq na Afghanistan kuvamiwa chini ya kisingizio cha kupambana na ugaidi au kusaka magaidi.
Baada ya tangazo hilo, nchi nyingi zikiwemo za ulimwengu wa tatu zilipitisha sheria tata, thakili na kandamizi ya kupambana na ugaidi ambayo imekuwa ikiwadhuru Waislamu na ikiongeza chuki katika jamii na kuupaka matope Uislamu kwa kupotosha weupe wake.
Licha ya sheria hiyo kupingwa na kukosolewa vikali kila mahali kwa kuwa inapingana na hata na sheria zao za kimataifa, misingi ya utoaji haki na katiba za nchi, bado ilipitishwa kwa nguvu na mabavu kwa matakwa ya madola makubwa hususan Marekani, huku nchi change zikinyenyekea.
Kupitishwa kwa sheria ya ugaidi kumepelekea mamia kama sio maelfu ya Waislamu kukamatwa, kuteswa, kuuwawa na kuwekwa kuzuizini kwa muda mrefu kwa kile kinachotajwa ni tuhuma za kujihusisha na ugaidi. Hayo kwa hapa Tanzania yanadhihirika kwa kuwekwa vizuizini maustadh, masheikh wanaharakati wakiwemo wa Hizb ut Tahrir na Jumuiya ya Uamsho.
Itakumbukwa pia kuwa kabla ya kuanza kwa kampeni ya kupambana na ugaidi kulikuwa na mahusiano mema miaka nenda miaka rudi baina ya jamii ya Kiislamu kwa kuishi vizuri na jamii za dini nyingine kwa amani na utulivu. Jambo ambalo limekuja kuvurugwavurugwa na kampeni hiyo.
Ni jambo lililo wazi kwamba matendo mengi yanayoripotiwa kufanywa na magaidi ni matukio ya kutengeneza yenye malengo ya kuupaka matope Uislamu na Waislamu na kudhihirisha kuwa vita hivi ni mwendelezo wa chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu. Aidha, vikundi kadhaa vinavyofanya ugaidi pia huundwa na madola makubwa ikiwemo Marekani, kama alivyodhihirisha wazi Raisi Trump kwamba kundi la kigaidi la ISIS liliundwa na Marekani kupitia aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Kigeni Hilarry Clinton.
Vita vya kigaidi ni mbinu ya kupora rasilmali katika nchi mbalimbali changa chini ya kisingizio cha kupambana na magaidi, huku wao ndio yanayomakinisha makundi ya kuleta vurugu na fujo kama ilivyo nchini Nigeria na sasa tunayoshuhudia Msumbiji. Itakumbukwa pia siku moja kabla ya shambulio la Septemba 11 mwaka 2001 aliyekuwa Waziri wa Ulinzi wa Marekani Donald Rumsfield alitangaza kuwa zaidi ya kitita cha dolari 2.3 tirioni kilipotea makao makuu ya ulinzi Pentagon, na mara baada ya tukio la Septemba 11 upotevu huo haukutajwa tena (Weakleaks 10/9/2019).
Waislamu na Uislamu ndio walengwa wakuu wa vita hivi, ni vigumu na ni muhali sana kusikia kuna mtuhumiwa wa ugaidi asiye Muislamu, licha ya kuwepo matukio na mauaji ya kinyama yanayofanya na wasiokuwa Waislamu lakini kamwe hayananasibishwi na ugaidi. Kwa mfano hivi karibuni tumeshuhudia mauaji ya kinyama yaliyofanywa na askari wa kizungu dhidi ya mwafrika George Floyd huko Marekani, mauaji yaliyochochewa na fikra za chuki za kibaguzi dhidi ya watu weusi na kufanyika hadharani lakini hayakuitwa kuwa ni mauaji ya kigaidi.
Kwa upande wa Uislamu dini yenye sifa kama mfumo wa kumsimamia mwanadamu katika maisha yake ikiwemo kudhamini amani unahimiza kuishi na jamii za dini nyingine kwa insafu na uadilifu. Aidha, licha ya kuwepo mgongano wa kifira katika msingi wa dini zao na Uislamu, kweli Uislamu unahimiza kuwalingania wasiokuwa Waislamu lakini kwa kutumia njia ya Mtume Muhammad (SAAW) kwa hoja na dalili bila ya kutumia nguvu wala mabavu. Na kimsingi Uislamu unapinga uharibifu wa miundombinu na kulaani vikali matumizi ya nguvu na silaha kwa wasiokuwa na hatia, awe Muislamu au mwengineo.
Uislamu wakati wote huliona suala la kumwaga damu ya asiye na hatia ni jambo ovu na kumfananisha mwenye kutenda hayo ni sawa na mtu aliyemwaga damu ya watu wote
مِنْ أَجْلِ ذَلِكَ كَتَبْنَا عَلَى بَنِي إِسْرَائِيلَ أَنَّهُ مَنْ قَتَلَ نَفْسًا بِغَيْرِ نَفْسٍ أَوْ فَسَادٍ فِي الأَرْضِ فَكَأَنَّمَا قَتَلَ النَّاسَ جَمِيعًا وَمَنْ أَحْيَاهَا فَكَأَنَّمَا أَحْيَا النَّاسَ جَمِيعًا
“Kwa sababu ya hayo, tukawaandikia wana wa Israeli, ya kwamba atakayemuua mtu bila ya yeye kuuwa mtu, au bila ya kufanya fisadi katika nchi, ni kama amewaua watu wote, na mwenye kumwacha mtu hai (kumsaidia kuishi) ni kama amewaacha hai watu wote (TMQ 5: 32 )
Imeandikwa na Ust. Issa Nasibu
Risala ya Wiki No. 78
01 Dhu al-Qi’dah 1441 / 22 Juni 2020 Miladi
https://www.facebook.com/Hizb-ut-Tahrir-Tanzania
#KomeshaUkandamizajiWaKisheriaNaUtekaji
#StopOppressiveLawsAndAbduction
Maoni hayajaruhusiwa.