Mazingatio ya Ramadhani – 1
بسم الله الرحمن الرحيم
Uwepo wa Hisia ya Udhaifu na Utegemezi wa Mwanadamu (Fitra)
Moja katika dhihirisho na zingatio muhimu ndani ya mwezi wa Ramadhani ni udhaifu na utegemezi wa mwanadamu, kwa kule mwanadamu kuhisi udhaifu wa kuhitaji chakula na maji.
Udhaifu huu unadhihirisha kuwepo ndani ya maumbile ya mwanadamu hali ya kutojitosheleza na utegemezi usioepukika, kwa kuwa mwanadamu akikosa chakula au maji maisha yake huwa hatarini.
Kuhitajia huku chakula, maji, yaani hali ya uwepo wa njaa na kiu ndani ya nafsi yake bila ya matakwa yake, na kuwa na mahitajio mengine ya kibaologia kama hewa ni dalili ya kuwa mwanadamu ni kiumbe. Na tabia ya kila kiumbe ni udhaifu na utegemezi kwa kiumbe kingine. Hivi ndivyo alivyo mwanadamu huishi duniani kwa kuhitajia chakula, maji na kuvihatia viumbe vyengine mbalimbali kufanikisha maisha yake.
Kuhisi na kuukubali udhaifu huu mwanadamu ndio huitwa ‘fitra’. Maana ya fitra ni ile hali ya mwanadamu kuhisi udhaifu wake wa kimaumbile na mazingira yaliyomzunguuka na kuhisi pia kuwepo Mwenye nguvu anaeyaingilia maisha yake bila ya ridhaa au matakwa yake.
Mwanadamu anahitaji chakula ili aishi, na chakula kwa kuwa nacho ni kiumbe kuwepo kwake huhitaji kiumbe kingine kama ardhi na maji. Na ardhi na maji kwa kuwa navyo ni viumbe hutegemea vyengine kuwapo kwao. Na hii ndio tabia ya viumbe vyote.
Allah Taala kwa kuwa Yeye ni Muumbaji wa kila kitu, kamwe hategemei wala hahitaji chochote kuwepo kwake, hahitaji chakula, maji wala kiumbe chochote. Bali viumbe vyote humuhitajia Yeye kwa kila kitu.
Ndio maana Allah Taala katika kuvunja msimamo wa manaswara/wakiristo juu ya madai yao ya uungu wa Nabii Issa As. na mama yake, akaleta hoja nzito kwamba wote wawili Issa As. na mama yake sio miungu, kwa kuwa walikuwa wanakula chakula. Vipi Mungu awe dhaifu na tegemezi na muhitaji kwa kiumbe kingine?
مَا الْمَسِيحُ ابْنُ مَرْيَمَ إِلاَّ رَسُولٌ قَدْ خَلَتْ مِنْ قَبْلِهِ الرُّسُلُ وَأُمُّهُ صِدِّيقَةٌ كَانَا يَأْكُلاَنِ الطَّعَامَ انظُرْ كَيْفَ نُبَيِّنُ لَهُمْ الآياتِ ثُمَّ انظُرْ أَنَّى يُؤْفَكُونَ
“Masihi mwana wa Maryam si chochote ila ni Mtume. Wamekwishapita Mitume kabla yake. Na mama yake ni mwanamke mkweli. Wote wawili walikuwa wakila chakula. Angalia jinsi tunavyowabainishia Aya, kisha angalia vipi wanavyogeuzwa” (Surat Maida: 75)
Mwanadamu akitaka kuutambua na kuukubali dhahiri udhaifu na utegemezi wake wa kimaumbile, huwa hana namna ila kumnyenyekea Muumba wa kila kitu. Mpaka hapo huwa ana jukumu la kutafuta namna sahihi ya ibada kwa ajili ya kumnyenyekea Muumba wake, ambae sio muhitaji wa chochote.
18 Ramadhan 1441 Hijri – 11 Mei 2020 M
Maoni hayajaruhusiwa.