Vipi Khilafah Itaisimamia Ramadhani ?
بسم الله الرحمن الرحيم
Tumo ndani ya mwezi mtukufu wa Ramadhani. Mwezi wa Rehma, Maghfira, uchaMungu na kujikurubisha zaidi kwa Allah Ta’ala. Ni wajibu na muhimu katika mwezi huu tukumbuke kwamba katika Uislamu kila aina ya ibada hata ile inayotendwa kwa kujitakasa mtu kibinafsi bado kufanikiwa kwake hutegemea msukumo wa dola (Khilafah).
Dola huihamasisha na kuitetea kifikra ibada husika na pia huchukua hatua za kinguvu kuilinda ibada ya faradhi kwa kutoa adhabu kali ya taazir. Kwa mfano, ibada ya Swala, japo kwamba ni ibada inayotendwa na mtu kibinafsi lakini dola kwa upande wake itaisimamia kwa kuihamasisha kupitia mbinu mbalimbali kama maskuli, vyuo, misikiti, vyombo vya habari nk.
Pia, Khilafah itasimamia misikiti, itachagua maimamu na kuwalipa, kadhalika kuwatia adabu Waislamu watakaozembea ibada hii. Vivo hivyo ndivyo ilivyo pia kwa upande wa ibada ya Saumu ya Ramadhani. Ibada ambayo ni wajibu amma pakiwa pana dola au pasiwe na dola. Lakini ili kufikia upeo na ufanisi wake lazima uwepo usimamizi kamili wa dola ya Kiislamu ya Khilafah.
Kwa bahati mbaya na kwa masikitiko makubwa ibada yetu ya Saumu leo kama zilivyo ibada nyengine haziko chini ya usimamizi thabiti wa utawala. Na kwa hivyo, kila siku zinapoteza haiba yake ya Kiislamu na ladha yake ya asili kutokana na kuwa kwetu chini ya usimamizi wa mfumo usiokuwa wa Kiislamu, mfumo batil wa kidemokrasia.
Khilafah katika usimamizi wake thabiti kwa ibada hii, kwanza, itaandaa mazingira mazuri kifikra na uhamasishaji wa ufaradhi wake kwa Umma ili waipokee Ramadhani kwa imani na unyenyekevu kumtumikia Mola wao. Kinyume na hali ilivyo leo namna Ramadhani inavyooneshwa kimakosa na baadhi ya watu kama jela inayowafunga watu kukosa kufanya ‘mambo yao’, kiasi cha makafiri kuwaburuza baadhi ya Waislamu waliochanganyikiwa katika sherehe zinazoitwa ‘vunja jungu’ ili kukomoa kufanya uovu kwa mara ya mwisho na kufunga rasmi raha za maovu, siku chache kabla ya kuingia ati katika ‘jela’ ya Ramadhani. Fikra ya hatari inayoshikiliwa kimakosa na baadhi ya Waislamu na inayoweza kumtoa mtu katika Uislamu , lau ataikinai na hakutubu kwa Mola wake.
Khilafah itapambana vikali dhidi ya fikra kama hizi potofu za kuidhalilisha amri ya ibada ya Saumu, pia na fikra nyengine, kama kuiona Ramadhani kuwa ni mwezi wa ibada za kiroho tu bila ya kufungamanisha na upande mwengine wa kimfumo. Kama Mtume SAAW alivyotuonesha kivitendo ndani ya Ramadhani kwa kupigana vita vya Badr, kuifungua Makka (Fathu Makka) na mapambano mengi baada yake kama Fathi ya Spain, Vita vya Hittin chini ya Jemadari Salahuddin nk. Matukio haya yote kutokea ndani ya Ramadhani ni dalili kwamba mwezi huu si tu ni mwezi wa ibada za kiroho bali pia ni mwezi wa kubeba ajenda pana ya kimfumo.
Pili, Khilafah itasimamia kwa umakini mkubwa suala la mwandamo wa mwezi, Khalifah atatangaza kuandama mwezi kwa Waislamu wote kama Umma mmoja, bila ya kuzingatia mistari iliyochorwa na makafiri (mipaka). Na dola itaweka ufafanuzi wa kutosha juu ya usimamizi wa muandamo wa mwezi kisiasa na kifiqhi ili kuondoa utata usio wa lazima kwa Umma wa Kiislamu.
Kisiasa, Ramadhani ni miongoni mwa ibada ambayo kuanza na kumalizika kwake lazima isimamiwe na dola pekee. Hivi ndivyo ilivyokuwa tangu zama za Mtume SAAW na makhalifa waliotangulia. Kwa kuwa ibada hii hupelekea moja kwa moja muda wa ibada kubwa ya Hijja na dira nzima ya kalenda ya Kiislamu. Amma kifiqhi, katika misingi ya kifiqhi, mujtahid hulazimika kubwaga rai yake anayoishikilia (tabanni) endapo inagongana na rai nyengine inayounganisha umoja wa Waislamu wote, au inayogongana na rai inayoshikiliwa na Khalifah, katika suala ambalo kiasili liko chini ya usimamizi wa Khalifah pekee. Katika hali hiyo mujtahid kwa ikhlasi ni wajibu kubwaga rai yake na kushikilia rai ya kiongozi wa dola. Jambo hili ni maarufu katika zama zote za makhalifah na linatokana na ‘Ijmaa’ ya Maswahaba wote, hadi katika fani ya misingi ya Sheria za Kiislamu ikazaliwa qaida inayosema: “Amri ya Khalifah huondosha ikhtilafu”. Kwa ufupi, mgogoro uliopo leo usio wa lazima na unaokuzwa na makafiri juu ya muuandamo wa mwezi utakufa kifo cha kawaida na kubakia katika kurasa za historia kwa njia ya kisiasa na kifiqhi, na kutuliza nyoyo za Waislamu.
Khalifah atakapotangaza muandamo wa mwezi katika moja ya ardhi za Waislamu hulazimika Waislamu wote kufunga au kufunguaa hata kama mujtahid ana rai kinyume, bado huwa faradhi kwake kutii rai ya kiongozi. Na rai ya mujtahid kinyume na ya Khalifah, kwa kuwa ni rai ya Kiislamu, itaheshimiwa na itaruhusiwa kufundishwa lakini itakayofuatwa na kufanyiwa kazi ni rai ya Khalifah pekee.
Mwisho, Khilafah Rashidah itawapa adhabu kali wasiofunga (makobe) katika Waislamu, na pia kuwatia adabu wale wote amma wakiwa Waislamu au wasiokuwa Waislamu wanaokula hadharani, wanaohamasisha wengine wasifunge, wanaoneza fikra potofu kwa makusudi dhidi ya Ramadhani ili kuulinda utukufu, haiba na hadhi ya mwezi huu mtukufu.
Kutoka Jarida la Khilafah la Ramadhani 1432 Hijria (Agosti 2011 )
Maoni hayajaruhusiwa.