12 Ramadhan 1441 H
بسم الله الرحمن الرحيم
1. Siku kama leo mwaka 265 Hijri / 7 Mei 879 ulikamilika ujenzi wa msikiti mashuhuri (Masjid Ibn Tulun) wa jijini Cairo, Misri.
Huu ni msikiti wa tatu kwa ukongwe ndani ya Misri, kando na msikiti wa Amr ibn al As na msikiti wa Al-Askar.
Aidha, ni msikiti mkongwe ndani ya Misri na Afrika kwa ujumla ambao umebakia katika uasili wake, ukiwa ni msikiti wenye eneo kubwa zaidi ndani ya jiji la Cairo.
Ujenzi wa msikiti huu ulianza mwaka 263 Hijri na kumalizika mwaka 265 Hijri chini ya usimamizi wa Ahmad ibn Tulun, gavana wa Khilafah ya Abbassiya ndani ya Misri (868–884) akitumia kiasi cha dinari 120,000 katika ujenzi huo. Mchoro wa msikiti huo uliandaliwa na mhandisi wa kimsiri Saiid Ibn Kateb Al-Farghany, mkiristo wa madhehebu ya Kibti (Coptic Christian).
Msikiti huu kwa miaka mingi pamoja na mambo mengine, katika karne ya 12 ulikuwa ukitumika kama kituo cha kufikia mahujaji wanaopita kutoka Afrika ya Kaskazini kuelekea Hijaz (Makka)
2. Siku kama leo mwaka 597 Hijri / 16 Juni 1201 alifariki dunia Imam Ibn al-Jawzī, mwanachuoni mkubwa wa Kiislamu katika madhehebu ya Hanbal aliyekuwa bahri ya elimu ikiwemo Tareekh, fiqhi, tafsir, Hadith nk. Pia alikuwa mwandishi mahiri na mhadhiri mwenye mvuto mkubwa nk.
Jina kamili la Imam Ibn al-Jawzī, ni Abd al-Raḥmān binʿ Alī bin Muḥammad Abu ‘l-Faras̲h̲ bin al-Jawzī akitokana na kizazi cha Sayyidna Abubakar Swadik, Khalifa wa mwanzo na swahaba mkubwa wa Mtume SAAW.
Ibn al-Jawzī alizaliwa mwaka 510 Hijria mjini Baghdad, na wazazi wake ambao walikuwa katika hali bora kuchumi waliwekeza vya kutosha kumsomesha mtoto wao huyo kwa wanachuoni mashuhuri wa zama zile ndani ya Iraq, naye Ibn al-Jawzī alifanya juhudi kubwa katika masomo kiasi cha kufikia darja ya juu kielimu.
Imam Ibn al-Jawzī alipata umashuhuri zaidi katika zama za Khalifah al-Mustadi , khalifah wa 33 wa Abassiya aliyekuwa akiunga mkono madhehebu ya Hanbal.
Ibn al-Jawzi ameandika vitabu vingi sana katika fani mbali mbali za malumat ya Kiislamu. Al-Dhahab, mwanachuoni mkubwa wa masuala ya Tareekh katika kutaja kipawa cha uandishi cha Ibn al-Jawzi anasema :
‘simjui yoyote miongoni mwa wanavyuoni ambae kaandika vitabu vingi kama Ibn al- Jawzi’. Wengine wamefikia hadi kusema kwamba Imam Ibn al –Jawzi kaandika zaidi ya vitabu 700.
Katika zama za mtawala mwengine wa Abassiya (Al-Nasr) Imam Ibn a- Jawzi alipewa adhabu ya kifungo cha nyumbani (house arrest) kwa miaka mitano baada ya kukosoa na kupinga baadhi ya sera fulani za utawala.
Imam Ibn al-Jawzī alifariki dunia na kuzikwa mjini Baghdad akiwa na umri wa miaka karibu 74.
12 Ramadhan 1441 Hijri – 05 Mei 2020 Miladi
Maoni hayajaruhusiwa.