‘Kelele Nyumba za Ibada’ Sio Mwanzo Wa Demokrasia Kupuuza Dini

Tumeshuhudia hivi karibuni namna serikali kupitia Baraza la Taifa la Uhifadhi wa Mazingira (NEMC) ikikumbusha uwepo wa sheria inayokataza nyumba za ibada ikiwemo misikiti kupaza sauti wakati wa ibada na miito ya ibada kwa kile kinachoitwa kuzuiya uchafuzi wa hali ya mazingira kupitia sauti za juu kutoka kati nyumba hizo.

Ili kuweza kufahamu suala hili kwa kina yafaa tufafanue nidhamu ya kidemokrasia ambayo ndio muhimili uliowasukuma kuchukua hatua kama hizi.

Demokrasia ni nidhamu ya kiutawala inayodhamini haki na usawa katika jamii kupitia kuchunga maslahi ya mtu mmoja mmoja au kundi la jamii ya watu fulani. Msingi wa kupima haki au usawa huo ni kupitia matakwa ya mtu binafsi. Ambapo matakwa hayo husababishwa na ubinadamu wa mtu, akili yake, kipaji chake na dhamira yake juu ya maisha. Na yote hayo yamejengwa juu ya imani ya kwamba kila mwanadamu kazaliwa huru na ana haki ya kuheshimiwa mbele ya wengine.

Kwa msingi huo demokrasia imepuuza fikra zote zilizojengwa kwa misingi dini, na kubaki na msimamo ya kwamba ubinadamu uliodhahiri au uliochochewa (stimulated) ndio unaostahili kuhukumu maana ya haki na usawa katika jamii.
Dini ni imani juu ya Muumba aliyeumba mwanadamu, uhai, na ulimwengu (vitu vinavyounda maisha) ambapo kwa utukufu huo na mapungufu aliyonayo mwanadamu yampasa (mwanadamu) amuabudu (Muumba huyo) na kufuata muongozo wake juu ya maisha kufikia (mwanadamu) kupata utulivu wa nafsi na kusawirisha haki na usawa katika maisha.

Demokrasia inaamini uwepo wa dini (kwa mtu binafsi) lakini inapinga fikra na miongozo ya kidini kuisimamia jamii, kwa imani ya kwamba itikadi ni katika hitajio msingi kwa mwanadamu, na wanadamu huzaliwa huru kiitikadi, hivyo demokrasia huona misingi ya kidini haiwezi kuipelekea jamii kusimama katika misingi ya haki na usawa kwa kuwa itikadi ni katika matakwa ya mtu binafsi.

Ni wazi kwamba Demokrasia ni fikra iliyokuja kupingana na dini katika ngazi ya maisha na hata kwa mtu binafsi. Kwa upande wa maisha (kuisimamia jamii) demokrasia inapinga kijumla, tena wazi wazi, kwa mtutu wa bunduki kuwa usimamizi wa masuala ya kijamii, kiuchumi, na kisiasa haupaswi kuwa wa kidini kwa kuwa kufanya hivyo ni kukandamiza nafsi za watu na kuwanyima uhuru wa kuyaendea maisha watakavyo kwa kuzongwa na fikra kandamizi za kiuungu ilhali nafsi zao mara nyingine au nafsi moja kwa nyingine huwa kinyume na yaliyoamrishwa na Mungu.

Huo ni upande wa kimaisha, ama upande wa kibinafsi demokrasia inapingana na dini kwa kumuonyesha mtu binafsi kuwa kuna uhuru wa kiitikadi, hivyo mtu anaweza kubeba itikadi yeyote ikiwemo kutoamini uwepo wa Mungu, na yule anayeamini uwepo wa Mungu asilazimike au asilazimishwe kufuata maadili na miongozo ya dini yake. Kwa mantiki hiyo Demokrasia inasimamia maisha pamoja na kumsimamia mtu binafsi kinyume kabisa na itakavyo dini na badala yake inawasimamia watu kwa misingi (imani) ya kisekula (kupuuza dini).

Hivyo basi ndani ya jamii ya kidemokrasia imani ya dini ni jambo la kupuuzwa na halina nafasi hata chembe katika kuisimamia jamii (kiserikali), na kwa watu binafsi ni yenye kukashifiwa, na kiroho ni yenye kutukanwa kwa kukutanisha imani zote katika jukwaa moja (licha ya kupingana kiitikadi), anayemuomba na kumuabudu Allah (SWT) hupewa nafasi sawa na mshirikina au kafiri.

Licha ya demokrasia kuzuiya fikra na miongozo ya kidini kusimamia maisha bado sheria zake zote zipo kinyume na maadili na miongozo ya kidini. Imeporomosha nafasi na utukufu wa dini kwa kiasi kikubwa sana mpaka kufikia kwa nchi za Waislamu kama Saud Arabia kupuuza sheria na maadili ya dini kwa kuanzisha maovu mbalimbali ikiwemo kuanzisha kumbi za starehe na matamasha ya muziki wa manguli katika kuchupa mipaka ya kiroho na kimaadili.

Jambo hili na mengineyo kama baadhi tuliyoyataja hapo awali ni ishara tosha ya Waislamu kutanabahi kwa kina nafasi ya dini mbele ya demokrasia ili kuchukuwa hatua za mabadiliko na kujilinda kutokana na uadui wa demokrasia.

Uislamu unatuwajibisha kupingana na kila baya na kuhakikisha dini hii inasimamia wanadamu kwa mustakbali mwema kufikia haki na usawa kikweli, kinyume na mfumo wa kikafiri wa demokrasia unaochochea chuki, mchafukoge na vururgu katika jamii.
Anasema Allah (SWT):
ِ وَمَا دُعَاءُ الْكَافِرِينَ إِلاَّ فِي ضَلاَلٍ (الرعد:
“ Na haukuwa mwito wa makafiri ila katika upotovu”

Abdinassir Said
Risala ya Wiki No. 49
01 Dhu Hijjah 11440 Hijri / 02 Agost 2019 Miladi
Afisi ya Habari – Hizb ut- Tahrir Tanzania
https://hizb.or.tz/
https://www.facebook.com/Hizb-ut-Tahrir-Tanzania

Maoni hayajaruhusiwa.