Mali Iliyoporwa
بسم الله الرحمن الرحيم
Swali:
Assalamu Alaykum Warahmatullah Wabarakatuh,
Sheikh wetu mkarimu,
Kama inavyojulikana, kuwa ardhi ya Palestina yote imeporwa na kidola cha Wayahudi, kuna majengo mengi (real estates) na ardhi nyingi zilizoporwa wamiliki hasa hawajulikani. Na baadhi ya ardhi hizi dola ya kiyahudi inawamilikisha watu binafsi au makampuni ili kuwekeza humo miradi yao binafsi, nami naishi Palestina nimeelezwa nikodi real estate (sehemu kwa ajili ya kufanyia biashara) katika jengo ambalo analimiliki myahudi kwenye ardhi zilizoporwa katika moja ya vitongoji vya Palestina, na wenye ardhi hii hawajulikani, ima ni wakimbizi au wamehama.
Je inafaa kukodi real estate hii? Na ikiwa wenye ardhi hasa hawajulikani, je hukmu inabadilika? Au huchukuliwa (inaamiliwa) hiyo kuwa ni ardhi iliyoporwa na haifai kuamiliwa kwa kuiuza, kuinunua au kukodi? Allah Akubariki Sheikh wetu Mkarimu na Akuzidishie nguvu katika kiwiliwili na elimu. Na Allah Afungue kupitia mikono yako.
Jawabu:
Waalaykum Salaam Warahmatullah Wabarakatuh,
Ewe ndugu yangu, hakika ya mali iliyoporwa hubakia kuwa ni ya mwenye mali ile, hivyo haifai kuinunua au kuikodi kutoka kwa mporaji. Ufafanuzi wa hayo ni:
Hakika ya mali iliyoibwa au kuporwa huwa ni ya mwenye ile mali popote pale atakapoikuta. Ametoa Ahmad kutoka kwa Samura amesema: Kasema Mtume (SAAW): “Kitakapoibiwa kitu kutoka kwa mtu au kikimpotea mtu kitu chake na akakikuta kwenye mikono ya mtu vilevile kilivyo, basi yeye ndie mwenye haki hasa ya kile kitu. Kisha na arudi mnunuzi kwa muuzaji kwa ajili (ya kuchukua) thamani (yake)”. Nass hii ni kuwa mali iliyoibwa ni haki ya mwenye ile mali. Na pia Mtume (SAAW) anasema: “Dhidi ya mkono ulichokichukua mpaka ukirejeshe”. Ameitoa Tirmidh na akasema hadithi ni hasan. Hayo ni kwa mali iliyoporwa.
Kwahiyo, mwenye kupora ardhi ametenda haramu na amechuma dhambi kubwa kwa kauli ya Mtume (SAAW): “Mwenye kudhulumu ardhi kiasi cha shibri tu atazongwa kwa ardhi saba”. Ameitoa Muslim kutoka kwa hadithi ya Aisha (RA). Yaani mwenye kupora sehemu yoyote ya ardhi iwe ndogo au kubwa atakua ametenda dhambi kubwa na ataadhibiwa kwayo Akhera. Na hapa duniani atastahiki adhabu ya ta’aziir na atalazimishwa kurejesha alichopora katika hali yake vilevile alivyokipora kwa mwenyewe, kutokana na kauli yake (SAAW): “Dhidi ya mkono ulichokichukua mpaka ukirejeshe”. Ameitoa Tirmidh. Na kikiharibika katika mikono ya mporaji kile kilichoporwa au akakibadilisha hali yake kama kakishona kitambaa kilichoporwa au aliyeyusha madini yaliyoporwa au alichinja mnyama aliyeporwa, basi hudhaminiwa thamani yake na mporaji.
Kwahiyo, ukielewa kwamba kitu kimeibiwa au kimeporwa usikinunue na wala usikikodi na ukiwa (ukihisi) na shubha vilevile usikinunue. Mtume (SAAW) anasema: “Wacha lile linalokutia shaka na ulielekee lile lisilokutia shaka”. Ameitoa Tirmidh kutoka kwa Al Hassan bin Ally (RA). Na Tirmidh akasema “Hadithi hii ni hasan na sahih.
Kwahiyo, muda wa kwamba una yakini kuwa hiyo imeporwa, ni sawa ukiwa unamfahamu mwenyewe au humfahamu, la muhimu ni kuwa uwe na uhakika kwamba hiyo imeporwa, itakuwa haifai wewe kuikodi kwasababu mporaji haimiliki na kwa hiyo hawezi kufunga mkataba (‘aqd) wowote na wewe.
Allah akutosheleze na akuepushe na kukodi huko, na tafuta real estate nyengine ili ukodi, na Allah akubariki kwayo na itakua ni kheri kwako katika dini na dunia. Na kwa vyovyote vile iwavyo hiyo real estate usiijutie. Allah yuko pamoja nawe.
Ndugu yenu Ata ibn Khalil Abu Rashta
20, Jamadul akhir 1439H
08/03/2018
Maoni hayajaruhusiwa.