9 Ramadhan 1441 H
بسم الله الرحمن الرحيم
1. Siku kama leo 9 Ramadhan 1225 Hijri / 8, Oktoba 1810 wapiganaji wa kimadhehebu ya Muhammad Abdul Wahab (Wahhabi) chini ya utawala wa Abdul-Aziz bin Muhammad bin Saud, mtawala wa pili wa dola ya Saudia walivamia katika mji wa Najaf Sharif, Iraq na kuleta uharibifu mkubwa.
Wapiganaji hao wa kimadhehebu ambao idadi yao karibu 12,000 kutoka mji wa Najd walivamia mji wa Karbala na kuuwa Waislamu wasio na hatia wakiwemo wazee, watoto wadogo na wanawake kiasi cha 2000- 5000, wakivurugavuruga maeneo ya makaburi ya mjukuu wa Mtume SAAW Imam Hussein ibn Ally ibn Abi Twalib. Pia walipora kiwango kikubwa cha mali zikiwemo fedha, vito vya thamani, dhahabu nk.
Uvamizi huo wa kimadhehebu ulichukuwa masaa nane, na baadae wapiganaji hao wakaondoka na zaidi ya ngamia 4000 wakibeba mali nyingi walizopora wakidai kuwa ni ngawira.
Wapiganaji hao wa madhehebu ya kiwahabi walitenda dhulma, uporaji na ukatili huo kuwafanyia Waislamu wa madhehebu ya Shia kwa madai kwamba wanashikamana na upotofu, na wao Wahabbi kwa kuwa wanashikamana na Uislamu safi wanapaswa kuusafisha Uislamu na kila aina ya doa na bidah.
Buyuk Sulayman Pasha ambaye ni mwakilishi wa Khilafah Uthmania katika eneo lililotokea uvamizi huo ambalo lilikuwa chini ya Khilafah hakusimama kidete ipasavyo katika kukabiliana na uvamizi huo wa Wahabia, jambo lilomfanya Khalifa wa wakati huo kumuondoa katika nafasi hiyo.
——————————————–
2. Siku kama hii 9 Ramadan 1393 Hijri / 25 Oktoba 1973 vilipiganwa Vita vya ‘Harb-ur-Ramadhan (Vita vya Ramadhan / Yom kippur) baina ya nchi ya Misri na Syria kwa upande mmoja dhidi ya kijidola cha Mayahudi (Israel)
Vita hivi viliasisiwa na Raisi Saadat baada ya kufariki Raisi Nasser akishirikiana na Raisi Assad wa Syria.
Lengo la vita sio kuangamiza Israel bali dhamira kuu ilikuwa ni kuzijenga haiba zao, kwa kuwa walikuwa watawala wapya, kuipa nguvu Israel na kuandaa mazingira ya kufanya mazungumzo na kijidola cha mayahudi. Yote haya chini ya maelekezo ya Marekani kwa kuwa watawala hawa walikuwa ni vibaraka wake watiifu.
3. Sheikh Yusuf an-Nabhani alizaliwa mwaka 1265 Hijri katika mji wa Ijzim, akasomeshwa na baba yake kisha akapelekwa chuo cha Azhar, Misri mnamo mwaka 1283 Hijri kwa masomo zaidi.
Sheikh Yusuf an-Nabhani baada ya masomo akawa mtumishi muaminifu wa dola ya Khilafah Uthmania, aliwahi kusomesha ndani ya Palestina, alifanya kazi ya uqadhi (hadi kufikia Qadhi mkuu) ndani ya mji wa Jenin (Palestina), Mosul (Iraq) nk. Pia aliwahi kuwa mhariri wa gazeti la kila siku la Al-Jawaneeb.
Sheikh alikuwa mtetezi mkubwa wa dola ya Khilafah na alisimama kidete kupinga fikra za wazandik waliokuwa wakifanya kazi kuivunja Khilafah, pia aliwapinga wazi wazi wanaharakati waliojaribu kuingiza fikra za upotofu za ‘usasa’ katika Uislamu.
Sheikh Yusuf an-Nabhani ndio babu mzaa mama wa Sheikh mkubwa, mujtahid, mwanafikra na mwanasiasa mahiri Sheikh Taqiuddin al-Nabhan (rahimahullah) ambaye ni mwaasisi wa
Hizb ut Tahrir
Makuzi ya Sheikh Yusuf an-Nabhani kwa mjukuu wake ikiwemo kumpeleka Misri na Azhar kwa masomo zaidi yalichangia pakubwa kufikia darja aliyofikia Sheikh Taqiuddin al- Nabhan.
Sheikh Yusuf an-Nabhani ameandika mamia kama si zaidi ya vitabu, makala, nasaha, mashairi nk. katika fani mbali mbali na kuunufaisha pakubwa Umma wa Kiislamu kwa upande wa maalumat.
Sheikh Yusuf an-Nabhani ameishi katika mji wa Istanbul, mji mkuu wa Khilafah, Beirut nk. Pia aliishi ndani ya Madina mpaka viliporipuka Vita vya Kwanza vya Dunia akarejea Ijzim (Palestina) na kufariki dunia hapo.
09 Ramadhan 1441 Hijri – 02 Mei 2020 Miladi
Maoni hayajaruhusiwa.