17 Ramadhan
بسم الله الرحمن الرحيم
1. Siku kama hiyo 17 Ramadhan mwaka wa 2 Hijria. Waislamu chini ya Mtume SAAW walipigana vita vya Badri.
Hivi ni vita vya mwanzo vikubwa baina ya jeshi la Kiislamu na jeshi la makafiri mara baada ya Mtume (SAAW) kusimamisha Dola ya mwanzo ya Kiislamu ndani ya Madinat-ul Munawara.
Ni tukio lililodhihirisha izza/ nguvu ya Waumini na serikali yao ya Kiislamu, japo kwa wakati ule ilikuwa change. Kadhalika Ilikuwa ni idhilali ya waziwazi kwa makafiri na viongozi wao.
Na zaidi ni kielelezo cha kuwepo na kuendelea mapambano baina ya haki na batil ,nuru na viza, na dhulma na uadilifu mpaka Siku ya Qiyama.
2. Siku kama leo katika Vita vya Badr waliuliwa baadhi ya viongozi mashuhuri wa Maqureish na wapinzani wakubwa wa Mtume SAAW na Uislamu kwa jumla.
Miongoni mwao viongozi hao ni :
Abu Jahl, (Fir-aun wa zama Umma huu), Walid ibn Utbah, Utbah ibn Rabi’ah, Umayyah ibn Khalaf, Shaybah bin Rabiah nk.
Vifo vyao vikatimiza bishara ya Mtume SAAW alipowahi kuwambia wapinzani hao kwamba siku moja watakabiliwa kwa kuchinjwa.
3. Siku kama hii tarehe 17 Ramadhan 58 Hijria (16 July 678) alifariki dunia bi Aisha bint Abubakar, mke wa Mtume SAAW na Mama wa Waumini.
Mama Aisha alikuwa mke wa tatu wa Mtume SAAW baada ya Mama Khadija na Mama. Sawda.
Ndoa ya bi. Aisha na Mtume SAAW inaaminika kufanyika miaka miwili au mitatu kabla ya Hijra, na kudumu na Mtume SAAW kwa miaka tisa na miezi mitano kufuatia kufariki dunia Mtume SAAW.
Bi. Aisha alifariki dunia Madina akiwa na umri wa miaka karibu kama 64, na kuzikwa katika makaburi ya Jannat al-Baqi hapo hapo Madina.
4. Siku kama hii, kwa munasaba wa masahaba watatu walioanza mapigano na maqureishi katika medani ya Vita vya Badr, Allah SW aliteremsha aya maalum ya Quran kuelezea tukio hilo kubwa.
Masahaba wa awali walioanza Vita ni Imamu Ali ibn Abi Talib (ra.) akikabiliana kafiri Walid bin Utbah, sahaba Hamza (ra) akimkabili kafiri Utbah bin Rabiah, na sahaba Ubaydah bin Al-Harith (ra.) akikabiliana na Shayba bin Rabiah.
Katika mchakato huo wa kuanzia vita, Imamu Ali papo hapo alimuuwa Walid bin Utbah, Hamza nae alimuuwa mara moja kafiri Utbah bin Rabiah na sahaba Ubaydah akajeruhiwa vibaya na Shayba bin Rabiah. Lakini haikuchukua muda Shayba bin Rabiah nae akauliwa hapo hapo.
Allah Taala Aliteremsha aya maalum kwa munasaba wa jambo hili kuwasifu upande wa Waislamu namna walivyojizatiti katika vita dhidi ya makafiri, na pia aya zikawatangazia makafiri hao wa kikureishi kwamba ni watu wa motoni.
Quran inasema:
هَذَانِ خَصْمَانِ اخْتَصَمُوا فِي رَبِّهِمْ فَالَّذِينَ كَفَرُوا قُطِّعَتْ لَهُمْ ثِيَابٌ مِنْ نَارٍ يُصَبُّ مِنْ فَوْقِ رُءُوسِهِمُ الْحَمِيمُ
يُصْهَرُ بِهِ مَا فِي بُطُونِهِمْ وَالْجُلُودُ
“Hawa ni mahasimu wawili(makundi mawili) waliogombana kwa ajili ya Mola wao. Basi waliokufuru watakatiwa nguo za moto, na yatamiminwa juu ya vichwa vyao maji yanayochemka.
Kwa maji hayo vitayayushwa vilivyomo matumboni mwao, na pia ngozi zao”.
(TMQ 22: 21-22).
17 Ramadhan 1441 H – 10 Mei 2020 M
Maoni hayajaruhusiwa.