13 Ramadhan 1441 H

بسم الله الرحمن الرحيم

1. Siku kama leo katika zama za Khilafah ya Umar bin Khattab vilipiganwa Vita vya Buwaib baina ya Waislamu na Jeshi la Mafursi.

Jemadari wa Khilafah Umar kwa jina Al-Muthanna ibn Haritha aliongoza jeshi la kikosi cha Waislamu kutoka Madina kama 8,000 dhidi ya Mafursi 60,000 au 70,000.

Jeshi la Waislamu liliweka kambi yake upande wa magharibi wa mto Furat. Al-Muthanna ibn Haritha alifanikiwa kubuni mbinu ya kuligawa kati kati jeshi la Mafursi na kuweza kukabiliana nao kwa nguvu na ujasiri mkubwa. Kamanda wa Kiislamu Jarir ibn Abdullah akamuuwa Mehran, kamanda mkubwa wa Mafursi na kupelekea kudhoofika hamasa ya mafursi katika medani ya vita.

Nguvu ya mafursi ikapotea wakaanza kukimbia huko na kule na kutoroka vitani, lakini wakazingirwa na kupewa kichapo cha fedheha na idhilali kiasi cha kuuliwa Mafursi 50,000.

Waislamu walipata ushindi mkubwa katika vita hivi, ambapo ushindi huu ulikuwa nyeti kwa siku za mbele kuweza kuifungua Fursi yote kwa ujumla wake.

 

2.  Siku kama leo mwaka 15 Hijria Khalifa Umar ra. aliwasili Jerusalem, baada ya eneo hilo kuwekwa chini ya mamlaka ya Waislamu

Khalifah Umar bin al-Khattab akaoneshwa sehemu ambayo Mtume SAAW alianza safari ya kimiujiza ya Miiraj, akaamrisha eneo hilo lisafishwe, na kuna kauli kwamba alishiriki yeye binafsi kusafisha eneo hilo kwa nguo yake.

Kisha akatoa maelekezo paadhiniwe na akaswali swala ya Alfajiri eneo hilo.

Na adhana ya mwanzo ikaweza kusikika katika mji wa Jerusalem

13 Ramadhan 1441 Hijri –  6 Mei 2020 M

Masoud Msellem

Maoni hayajaruhusiwa.