Waislamu Na Matayarisho Ya Ramadhani

بسم الله الرحمن الرحيم

Kwa kuwa tumo ndani ya mwezi wa Sha’aban hapana shaka wiki chache zijazo Waislamu tutakuwa na mgeni mtukufu, yaani mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Ramadhani ni mwezi wa Qur-ani, una usiku mtukufu, ndani yake hufunguliwa milango ya pepo, kufungwa milango ya moto, amali za Waislamu hulipwa maradufu na nyoyo za Waumini hulainika kwa kupanda juu ucha-Mungu wao, ukarimu na mapenzi baina yao.
Swala linakuja, jee Waislamu tuna maandalizi yeyote kwa ajili ya mwezi huu mtukufu? Allah Taala anataka katika mambo yetu tuwe na maandalizi Aliposema:
وَلَوْ أَرَادُوا الْخُرُوجَ لَأَعَدُّوا لَهُ عُدَّةً
“Na ingelikuwa kweli walitaka kutoka ( kwenda vitani) bila ya shaka wangejiandalia maandalizi (makubwa)……” ( Tawba: 46)
Bila shaka Waislamu hawako nyuma katika kujiandaa na Ramadhani katika mambo mbalimbali kama futari, kutafuta nguo za sikukuu, kukarabati misikiti, kuandaa maimamu wa tarawekhe nk.
Hata hivyo, Ramadhani inahitaji matayarisho nyongeza zaidi ya hayo yaliyozoeleka.
Awali kabisa, ni kumuomba Allah SW atufikishe kuidiriki Ramadhani, kwani wema waliotangulia (Maswahaba) walikuwa ikimaliza tu Ramadhani wakimuomba Allah SW awakubalie funga na ibada zao. Na ukianza tu mfunguo saba walikuwa wakimuomba Allah Taala awafikishe waidiriki Ramadhani ijayo wakiwa na afya njema ili wanufaike na manufaa makubwa ambayo hayapatikani katika miezi iliyobakia.
Pili, Waislamu ni kujifunza masuala ya msingi kuhusu funga. Yaani wajue nguzo zake, mambo yanayobatilisha swaumu, kusihi kwake nk. ili mfungaji awe na uhakika kielimu wa anachokitenda. Na kama Muislamu hujui basi ni lazima ajiegemeze kwa mwanazuoni Mujtahid ili iwe hujjah kwake kuwa katekeleza ibada hiyo kwa elimu. Allah SW katukataza kutekeleza jambo tusilo na elimu nalo, maana yake ni kuwa jambo hilo tulitafutie maarifa yake. Tumeshuhudia Waislamu hujifunza kwa haraka kuhusu Hijja miezi michache kabla ya safari. Basi na kwa Ramadhani hilo linawezekana.
Tatu, Waislamu katika kipindi hiki tunapaswa kujiandaa kwa kuhakikisha hawazidhulumu nafsi zao kwa kufanya maovu na badala yake wanaziokoa nafsi zao kwa kuhakikisha wanajiweka safi kuingia katika mwezi mtukufu wakiwa safi ili kumridhisha Allah Taala pekee kwa kuheshimu matukufu yake. Allah SW anasema:
ذَلِكَ وَمَنْ يُعَظِّمْ شَعَائِرَ اللَّهِ فَإِنَّهَا مِنْ تَقْوَى الْقُلُوبِ
“Ndio hivyo! Na anayetukuza matukufu ya Mwenyezi Mungu, basi hayo ni katika uchamungu wa nyoyo” (Hajj: 32)
Nne, Waislamu hatuna budi kujiandaa kifikra na kisaikologia kabla ya kuingia Ramadhani, kwa kuweka azma ya kweli, kuifunga Ramadhani yote kwa ikhlasi na unyenyekevu na kujiweka mbali na shubha zote. Pia tujiepushe kuipokea Ramadhani kama jela au kero fulani. Aidha, tujiepiushe kufunga tu ilimuradi watu watuone, au kuogopa kusemwa vibaya ndani ya jamii. Mtume SAAW anatufundisha kuwa vitendo vitalipwa kwa kuzingatia nia ya mtendaji.
Tano, matayarisho pia yanahusisha kwa Waislamu kuanza kujizoesha kufanya ibada mbalimbali ili isije kuwawia ugumu kwao kuzitenda ibada hizo itakapoanza Ramadhani. Ni vyema kuanza kufanya baadhi ya ibada kama qiyamul-layli, kusoma qur-ni kwa kuuzoesha ulimi, kufanya dhikri mbali mbali, kutoa sadaka nk.
Bibi Aisha ra. anasimulia kuwa Mtume SAAW alikuwa akifunga zaidi mwezi wa Sha’abani mpaka unadhania hafungui ataunganisha na Ramadhani…”. Sasa kwetu ni vizuri kuiga mwendo huo mzuri, kama ni matayarisho kwa ibada hii.
Kwa kumalizia, maandalizi ya Ramadhani yana wigo mpana, hivyo, kila jambo jema ambalo litafanya ibada yetu hiyo iwe na ufanisi hatuna budi kuliweka tayari tayari ili kufanikisha ibada hiyo adhimu inayokuja wiki chache zijazo.
Ali Amour
Risala ya Wiki No. 100
09 Shaaban 1442 Hijri
22 Machi 2021 Miladi
Afisi ya Habari – Hizb ut- Tahrir Tanzania

 

Maoni hayajaruhusiwa.