Vita Ya Mazao’ Kati Ya Malawi Na Tanzania

بسم الله الرحمن الرحيم

Habari:

Mnamo tarehe 2 Mei, 2025 Waziri wa Kilimo wa Tanzania, Hussein Bashe pamoja na Waziri wa Kilimo wa Malawi, Sam Kawalenga walifanya Mkutano wa Kidiplomasia baina ya pande mbili Jijini Dodoma kwa lengo la kumaliza vita ya kibiashara iliyozuiya uingizwaji wa mazao ya kilimo baina ya nchi hizi mbili (The Citizen 03/05/2025)

Maoni:

Nchi mbili hizi ziliingia katika vita hii ya kibiashara mwezi wa Aprili 2025 kufuatia serikali ya Malawi kupiga marufuku uingizwaji wa bidhaa za kilimo (mazao) kutoka Tanzania.
Serikali ya Tanzania nayo pia ilijibu mapigo kwa kutangaza marufuku yake kwa bidhaa za mazao kutoka Malawi mnamo tarehe 23/04/2025, na kuiondoa marufuku hiyo siku ya 26/04/2025 ikiwa ni baada ya kufanya kazi marufuku hiyo kwa muda wa siku mbili. Malawi ilizuiya uingizwaji wa bidhaa kadhaa za kilimo kutoka Tanzania ikiwemo unga wa ngano, mchele, tangawizi, ndizi na mahindi
Kutoka nchini Malawi, serikali ya Tanzania ilizuiya uingizwaji wa bidhaa zote za kilimo ikiwa ni pamoja na tufa (apples), machungwa pamoja na mazao mengineyo. Vita hii imeathiri maisha ya pande zote za watanzania na wamalawi ambapo wafanyabiashara, wachuuzi wadogo, na kubwa zaidi imeathiri masikini ambao wanategemea biashara hii kwa maisha yao ya kila siku kwa kupata chakula na masoko.
“Vita ya mazao” inaonesha kwa kiasi kikubwa cha uzembe na upuuzaji mkubwa wa wanasiasa wa kibepari na serikali zao. Licha ya maafa makubwa, pande zote mbili hazikuzingatia athari za marufuku zao kwa wachuuzi wadogo wadogo, kuathirika kwa biashara ya mpakani, na maafa kwa watu wa kawaida ndiyo maana serikali zote mbili zilichukua hatua za “kitoto” za “piga nikupigie”. Wachuuzi wadogo wadogo kutoka katika mji wa Karonga nchini Malawi walilitaarifu Shirika la Habari la Uingereza (BBC) tarehe 25/04/2025 kuwa:“tani za bidhaa (zao) zinaharibika na kutupwa baada ya kuzuiwa kuingia nchini Tanzania. Hali kama hiyo pia ilitokea upande wa Tanzania ambapo tani za nyanya na ndizi ziliharibika mpakani mwa Tanzania na Malawi.
Vita hii ya mazao ni matokeo ya uhasama wa muda mrefu kati ya Malawi na Tanzania unaotokana na mipaka liyolazimishwa na wakoloni. Nchi zote mbili kwa vipindi tofauti zimekuwa katika uhasama kuhusu Ziwa Nyasa (Ziwa Malawi) tangu zilivyopata uhuru wao wa bendera kutoka kwa Uingereza miaka ya 1960.
Mipaka iliyochorwa na wakoloni imeacha matokeo machungu na yenye madhara makubwa kwa nchi za Afrika ikiziingiza nchi hizi katika machafuko makubwa na migogoro mikubwa ya kiuchumi, kidiplomasia na hata kijeshi, migogoro ambayo imepelekea maangamizi makubwa.
Ili kutatua kimsingi tatizo hili la mivutano ya kibiashara mipakani, kunahitajika kung’olewa kwa mfumo mzima wa kibepari kwa kuwa ndio unaoleta maafa haya, na mbadala yake kuwekwa mfumo wa haki wa Uislamu chini ya dola yake ya Khilafah, kwa kupitia dola hiyo tukufu ya (Khilafah) ukombozi wa kweli utapatikana katika biladi za Kiislamu na katika nchi nyingine zinazoendelea zikiwemo zile za bara la Afrika
Imeandikwa na Said Bitomwa
Mwanachama wa Afisi ya Habari ya 𝐇𝐢𝐳𝐛 𝐮𝐭 𝐓𝐚𝐡𝐫𝐢

Maoni hayajaruhusiwa.