Umoja wa Afrika Katika Miaka 60 ya Kuimarisha Ukoloni Mamboleo
بسم الله الرحمن الرحيم
Habari:
Umoja wa Afrika (AU) ambao hapo awali ulijulikana kama Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) uliundwa mjini Addis Ababa, Ethiopia mnamo tarehe 25 Mei 1963, wakati wakuu wa nchi 32 kutoka mataifa “huru” ya Afrika walipokutana jijini humo kutia saini mkataba uliounda OAU, ambapo ilikuwa karibu 60% ya nchi katika bara (Afrika) zilikuwa zimepata uhuru wao wa bendera. Taasisi hiyo ya kusimamia bara hilo ililenga kuleta kile walichokiita uhuru ‘kamili’ wa Afrika kutoka kwa ubeberu, ukoloni na ubaguzi wa rangi. Kwa hivyo, mnamo Mei 25, 2023 iliadhimisha kumbukumbu ya miaka 60 tangu kuundwa kwake.
Maoni:
Kama ilivyoainishwa katika Mkataba wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) / kwa sasa Umoja wa Afrika (AU), malengo yake makuu yalikuwa ni kukuza umoja na mshikamano wa nchi za Afrika, kufikia maisha bora kwa watu wa Afrika, kulinda uhuru wa nchi wanachama, kuondoa ukoloni katika bara hili na kuoanisha kipamoja sera za wanachama wake za kisiasa, kidiplomasia, kiuchumi, kielimu, kitamaduni, afya, ustawi, kisayansi, kiufundi na ulinzi.
Miaka sitini baadaye hakuna hata moja katika malengo yaliyotajwa lililofikiwa! Afrika imekuwa katika vita visivyoisha na migogoro ya kisilaha tangu 1963. Zaidi ya vita 35 na migogoro ya kisilaha zaidi ya 100 imetokea katika Afrika baada ya ukoloni mkongwe, ambayo mingi ni baina ya mataifa ya Afrika yenyewe kwa yenyewe. Kwa mfano, mwaka wa 2019, migogoro 27 ya kisilaha inayohusisha serikali ilirekodiwa, mwaka 2020, takribani migogoro 30 na mwaka 2021, migogoro 25. Hii ina maana Umoja wa Afrika(AU) umeshindwa kuleta umoja, mshikamano na amani barani Afrika.
Licha ya kuwa Afrika ina utajiri mkubwa duniani ikiwa na asilimia 30 ya madini yote duniani, yakiwemo 40% ya dhahabu yote duniani, 90% ya madini aina ya chromium na platinum, shehena kubwa ya madini ya cobalt, almasi, platinum, uranium nk. bila ya kusahau asilimia 65 ya ardhi inayofaa kwa kilimo duniani, lakini Afrika ndilo bara lenye maendeleo duni zaidi duniani likiwa na nchi 34 kati ya 49 maskini zaidi duniani. Zaidi ya 40% ya wakazi wa bara hili wanaishi katika umasikini wa kupindukia wa chini ya dola moja ya Marekani kwa siku. Umoja wa Afrika (AU) umeshindwa kuleta maisha bora kwa watu wa Afrika.
Kuhusu kulinda mamlaka ya nchi wanachama na kuondokana na ukoloni, sote tunajua Umoja wa Afrika (AU) hauwezi kufanya na haujawahi kufanya lolote kulinda mamlaka ya wanachama wake na Afrika iko chini ya ukoloni mamboleo. Ukoloni mamboleo unatekelezwa kupitia viongozi vibaraka na mapinduzi kwa maslahi ya mabwana zao, hali ya utegemezi ambayo wa Afrika kupitia sera za kifedha za kikoloni na taasisi za kifedha kama Shirika la Fedha la Kimataifa(IMF) na Benki ya Dunia(WB), hali duni ya kukosa kujiamini ikiambatana na kukosekana kwa usawa wa kibiashara kupitia mashirika ya kikoloni na sera kama vile Shirika la Biashara la Kimataifa (WTO), mfumo wa kielimu ambao fikra na thaqafa za kikoloni zinalazimishwa barani Afrika na utegemezi wa kijeshi. Hakuna mamlaka yoyote ya Afrika ambayo Umoja wa Afrika (AU) imelinda, wala kuondoa ukoloni, kwa sababu wakoloni walibadilisha tu mtindo wa ukoloni kutoka ukoloni mkongwe hadi ukoloni mamboleo wakitumia mbinu tofauti tofauti.
Kwa hiyo, miaka sitini ya Umoja wa Afrika(AU), haijafikia malengo na sababu za kuundwa kwake bali imekuwa ikitumika kueneza ukoloni mamboleo na kuwasaidia wakoloni katika unyonyaji wa utajiri na rasilimali za Afrika. Umoja wa Afrika (AU) unatuma vikosi vya kijeshi kulinda vitega uchumi vya wakoloni katika nchi zenye vita kama Kongo (DRC) kwa mbadala wa rushwa inayoitwa fedha za kusaidia shughuli za kulinda amani. Pia (AU) inafanya kazi kama wakala wa kueneza ajenda na kampeni mbaya ya vita dhidi ya ugaidi na kuhamasisha ushoga ambapo mataifa ya Afrika yanalazimishwa kuuwa na kuwafunga raia wao wenyewe kwa ajili ya kupata rushwa kutoka kwa wakoloni wagharibi kwa jina la fedha za kupambana na ugaidi na kusambaratisha na kuharibu mfumo wa kijamii na maadili.
Kwa ukweli ulio bayana Umoja wa Afrika (AU) uliundwa kuwa chombo cha kikoloni, na matokeo ya makubaliano ya wakoloni kuyaleta pamoja makoloni yao ili iwe rahisi kuyapa maagizo kwa pamoja, katika hali kama hii kamwe haitafikia malengo yake yoyote.
Afrika itakombolewa kikweli kutokana na minyororo ya kikoloni pale tu Dola ya Kiislamu ya Kiulimwengu (Khilafah Rashidah) itakaposimamishwa tena. (Afrika) itakuwa na nafasi ya izza kama zama zile za utawala wa Kiislamu ulipotawala awali, ambapo waafrika walifikia viwango vya juu vya maisha bora na kukomeshwa umaskini mpaka kufikia kukosekana mtu wa kupewa zaka. Imepokewa na Yahya Ibn Said, ambaye alikuwa Gavana wakati wa utawala wa Khalifa Umar Ibn Abdul Aziz, amesema:
“Nilitumwa na Umar Ibn Abdul Aziz (ra.) kukusanya zaka katika Afrika, baada ya kuikusanya, nilikusudia kuwapa watu masikini. Hata hivyo, sikumpata masikini yeyote kwani Umar Ibn Abdul Aziz alikuwa amemfanya kila mtu kuwa tajiri wakati wake. Hatimaye niliamua kutumia hazina ya zakat kuwakomboa watumwa.”
(Ibn Abd Hakam, Abdullah (1994) Al Khilafat Al Adil Umar Ibn AbdulAziz: Khamis Al Khulafah Al Rashidin, Dar Al Fadilat)
Imeandikwa na Said Bitomwa
Mwanachama wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Tanzania
Kwa ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir
Maoni hayajaruhusiwa.