Uislamu Unalenga Mapinduzi Ya Kimfumo Sio Mageuzi
بسم الله الرحمن الرحيم
Uislamu ni dini kamili ya kimfumo inayojitosheleza katika kusimamia ustawi na maisha ya ulimwengu huu. Mwenyezi Mungu Allah SWT anatuhakikishia hilo pale alipotuambia katika Surat Al- Maaidah kuwa:
ۚ الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإِسْلَامَ دِينًا ۚ ﴿٣﴾
“Leo Nimekukamilishieni Dini yenu, na Nimekutimizieni neema Yangu, na Nimekuridhieni Uislamu uwe Dini yenu.” (Al- Maidah : 3)
Hivyo, Uislamu ni mfumo wa maisha ulio kamili, una njia na ufafanuzi katika kila nyanja ya maisha, iwe siasa, uchumi, jamii, itikadi nk. Kwa kuzingatia hilo, ni muhimu kutambua kuwa Uislamu umekuja kuleta mapinduzi ya kimsingi na sio mageuzi katika kusimamia Ummah tangu kuasisiwa kwa serikali ya mwanzo ya Kiislamu ndani ya Madina hadi kuvunjwa kwa dola ya Khilafah mwaka 1342 H/ 1924 M katika mji wa Istanbul.
Uislamu umekuja kuleta mfumo wa mapinduzi ya kimsingi (radically) katika kila kitu na sio mabadiliko ya kimageuzi. Kwa kuwa kuna tofauti kubwa kati ya mabadiliko ya mapinduzi ya kimsingi na mabadiliko ya kimageuzi. Katika mabadiliko ya kimapinduzi watu huwa hawaamini kabisa katika mfumo uliopo, na hivyo hutaka kuuondoa mfumo husika wote moja kwa moja. Iwe nidhamu ya kisiasa, kiuchumi, kijamii nk. kwa mbadala wa mfumo mpya na mwengine kabisa.
Amma mabadiliko ya kimageuzi, watu hukubaliana na aina ya mfumo uliopo, isipokuwa tu hujaribu kukosoa mapungufu wanayoyaona wakiwa tayari kuweka marekebisho na viraka viraka , huku mfumo huo ukiendelea kuwepo. Kwa ufupi, watu huunga mkono katika mfumo huo wanayoyakubali, wakipigania kuboreshwa yale wasiyokubaliana nayo.
Lakini kwa mujibu wa Uislamu mabadiliko ya kimageuzi huwa hayakubaliki kwa kuwa hayana tija, kwa vile yenyewe huunga mkono mfumo uliopo, ilhali mabadiliko ya kimapinduzi huwa muafaka, kwavile hulenga kuuondoa kabisa mfumo wote uliopo moja kwa moja na kuleta mfumo mpya katika jamii.
Ili kuweza kuleta mabadiliko ya kweli ya mfumo wa kimapinduzi katika ulimwengu hususan biladi za Kiislamu hulazimu Waislamu kushikamana na manhaj/ njia ya kimapinduzi aliyokuja nayo Mtume wetu SAAW kwa kupitia mpambano wa kifikra na kisiasa bila ya kutumia mabavu au silaha. Kwa njia hiyo Mtume SAAW na masahaba wake watukufu waliweza kubadilisha vipengee vyote kama siasa, jamii, uchumi, elimu, uongozi nk. Kutoka katika utawala wa dola ya kikafiri(Darul kufr) na kupatikana mfumo mpya mbadala chini ya dola ya Kiislamu (Darul Islam).
Katika kufikia mabadiliko ya kimfumo ya kimapinduzi Mtume SAAW kamwe hakuunga mkono mfumo uliokuwepo Makkah, Madina au Bara Arabu kiujumla, bali alishika njia yake na akasimama kidete na mfumo wake wa Kiislamu. Hakuwa ni mwenye kusifia wala kupaka mafuta mfumo wa kikafiri uliokuwepo wala viongozi wake, bali alifanya kazi usiku na mchana kuufedhehi, kuukosoa mfumo huo na kuonesha uzuri na ufumbuzi wa mfumo wake mpya kimapinduzi wa Kiislamu.
Aidha, Mtume hakukubali kuunga mkono mfumo kinyume na mfumo wake,wala hakukubali kuwa kiongozi wa mfumo wa kikafiri, au kutawala kwa sheria za mfumo usiokuwa Uislamu. Inajulikana wazi kuwa Maquraishi walimtunuku Mtume Muhammad (SAW) fursa ya utawala kwa kumwambia:!
”إن كنت تريد به ملكا ملكناك علينا“
“Ikiwa unataka kutawala basi tutakuteua wewe kuwa mtawala wetu”
Hata hivyo, Mtume SAAW alikataa hidaya hiyo ya kijanja aliyopewa na Maqureishi, hakuikubali hata kwa bahati mbaya au walau kwa majaribio, licha ya ukweli kuwa fursa hiyo ilikuja katika kipindi kigumu ambacho Waislamu wamegubikwa na wimbi la kutisha katika mateso, propaganda, kususiwa, unyonge, kuuwawa nk. kutoka kwa maadui wao. Bila shaka kama jambo hilo lingekuwa na faida na maslahi kwa Uislamu hapana shaka yoyote Mtume SAAW angekubali. Lakini Mtume SAAW alikuwa wazi juu ya lengo lake la kutaka Uislamu utawale sio Waislamu, alitaka mabadiliko ya kimapinduzi na sio mageuzi, zaidi alitaka mabadiliko yake yasiwe na masharti yanayogongana na akida yake. Mtume(SAW) daima alikuwa akiweka msimamo wake kama alivyosema:
«لَوْ وَضَعُوا الشَّمْسَ فِي يَمِينِي وَالْقَمَرَ فِي شِمَالِي عَلَى أَنْ أَتْرُكَ هَذَا الْأَمْرَ حَتَّى يُظْهِرَهُ اللَّهُ أَوْ أَهْلِكَ فِيهِ مَا تَرَكْتُهُ»
“Lau wataliweka jua katika mkono wangu wa kulia na mwezi katika mkono wangu wa kushoto ili niachane na jambo hili, sitoachana nalo hadi Mwenyezi Mungu anifanye kuwa mshindi, au niangamie kwalo.”
Kwahiyo, Mtume SAAW alibeba ajenda yake ya mapinduzi ya kimfumo kuwa ni mapambano ya kufa na kupona mpaka Mwenyezi Mungu(SWT) akajaalia Uislamu ushindi, na daima Wislamu walishikamana na haki bila ya kutetereka, wakishikamana na subira kwa kipindi chote walipokuwa Makkah mpaka walipoweza kusimamisha dola yao ya mwanzo ya mfumo wa kimapinduzi ndani ya Madina.
Utaratibu huo alioundama Mtume SAAW na masahaba wake ndio njia ya Kiislamu ya kuleta mabadiliko ya kweli ya kimapinduzi ya kimfumo. Kwa njia hiyo Mtume SAAW alipata ushindi na kuondoa kila aina ya udhalili kwa watu wote. Leo Umma wetu una wajibu wa kushikamana na njia hiyo ili kuleta mapinduzi ya kimfumo kwa ajili ya kuwanusuru Waislamu na wanadamu kiujumla kutokamana na makucha thakili ya unyonyaji, dhulma na mateso ya mfumo fisidifu wa kibepari, kwa mbadala wa mfumo adhimu, sahali, wenye Rehma na wa haki wa Kiislamu.
Tuyakumbuke maneno adhimu ya Khalifah Umar Ibn Khattab ra. aliposema:
كنا أمة مهينة ، فشرفنا الله بالإسلام .. فكلما طلبنا الشرف في غير الإسلام يذلنا الله!
“Hakika sisi tulikuwa ni watu madhalili katika dunia kabla ya kuja Uislamu, Allah Swt akatufanya ni watu wenye heshima baada ya kuja Uislamu, ikiwa tutafuata kitu kingine kando na Uislamu, Allah SWT Atatudhalilisha.” (Al Mustadrak)
Risala ya Wiki No. 147
22 Rabi’ al-thani 1444 Hijria / 16 Novemba 2022 Miladi
Afisi ya Habari – Hizb ut Tahrir Tanzania
Maoni hayajaruhusiwa.