Uharamu wa ‘Siku ya Wapendanao’ (Valentine’s Day)
Katika nchi zote za Ki-magharibi na nchi za Waislamu kwa kuigiza wamagharibi tayari kauli mbiu ya “acha msimu wa mapenzi uanze” inaanza kusikika tena. Ni wakati kama huu wa mwezi wa Februari ya kila mwaka ambapo maua husambazwa, wapenzi hupeana stika, kadi za mapenzi, hutumiana sms za mahaba, kukiri makosa ya kimapenzi na kupeana miadi mipya (ambayo ni nadra mno kutekelezeka).Yote hayo kwa lengo la kuchapua mapenzi baina ya wapendanao katika ‘Siku ya Wapendanao’ (Valentines’Day)
Siku ya Februari 14 ya kila mwaka inajulikana kama ‘Siku ya Valentine’ inayonasibishwa ati ni ‘Siku ya wapendanao’. Ni siku ambayo kwa karne nyingi imeandaliwa maalum kuwatukuza wapendanao. Katika siku hiyo kadi hufurika kwa watu kutuma ujumbe wa “penzi la kweli (true love)” kwa wanaowapenda. Watoto nao pia huwamasishwa kuitukuza siku hiyo ya Valentine, na hata wanapokuwa katika viwanja vya michezo huhimizwa kuwaonesha mapenzi ya udhati kwa watoto wenzao wanaowapenda.
Jee kuna madhara gani kusherehekea siku hiyo? Anaweza mtu kuuliza, kwa kuwa mwisho wa yote, hii ni siku ya kuwaonyesha hisia zako jinsi gani unamjali na unavyowapendampenzi wako na kwa watoto huwa ni kama kujifurahisha tu. Lakini , Jee umeshawahi kujiuliza Valentine alikuwa nani na wapi utamaduni huo wa siku ya Valentine umetoka na nini malengo ya sikukuu hiyo?
Mnamo karne ya tano Kanisa Katoliki lilitaka kumaliza ukuwaji wa mila za wapagani ambapo Waroma walikuwa wakizifanya kila mwaka tokea karne ya 4 BC.
Kutokana na mila za za Waroma wakati huo, walikuwa wakifanya ndani ya siku ya Februari 14 aina ya kamari maalum kuwashirikisha vijana wao wa kike na wa kiume kwa ajili ya kupeleka zawadi kwa “mungu”wao Lupericus. Vijana wa kike walishiriki katika kamari hiyo kwa kuweka majina yao kwenye kiboksi na kasha la vijana wa kiume. Na vijana wa kiume huchagua majina hayo. Kupitia kamari hiyo msichana aliyebahatika kuchaguliwa na mvulana fulani, hapo huwa na mvulana huyo kwa mahusiano ya kimapenzi kwa kipindi chote cha mwaka mzima hadi kamari ya mwaka unaofuata.
Kanisa halikufurahishwa kabisa na mpango huo wa kiibada za kiroma ambazo hupelekea kufanya mapenzi kiholela kupitia kamari na likaamua kutokomeza mila hiyo kwa kuchagua “Mpenzi ”, ambaye hutunukiwa badala ya mila ya kamari ya “mungu” Lupericus. Kanisa likamchagua Askofu Valentine, mtu ambaye alihukumiwa kuuwawa katika karne ya 3 AD kutokana na kukaidi amri ya mtawala (Emperor Claudius). Mtawala ambaye alipiga marufu kuoa kwa madai ya kuwa wanaume wanaoowa wanafanya vibaya vitani na wakati mwengine huwa hawataki kuwacha familia zao na kwenda vitani. Askofu Valentine alikuwa anawaalika wanaotaka kuoana na kuwaozesha kwa siri.
Kwa sababu hiyo akauwawa. Kabla ya kuuliwa alikuwa akituma ujumbe wa kimapenzi kwa binti wa mlinzi wa jela aliyewahi kuwa na mahusiano nae kimapenzi. Ujumbe wake ulikuwa: “kutoka kwa wako Valentine (from your Valentine)”.
Kwa hivyo Kanisa Katoliki likamchagua Askofu Valentine awe mfano wa kuigwa kwa wapendanao na kutokemeza ibada za kipagani za kufanya mapenzi kiholela kwa kuchagua mwanamke kwa njia ya kamari. Na badala yake likahimiza kuowana. Lakini kutokana na nidhamu ya kidemokrasia kuibuka katika nchi zao na watu kuwacha mafunzo ya kidini na kuburuzwa na fikra za ‘uhuru’, siku hiyo ikawarejesha kule kule katika zama za wapagani kwa kuhamasisha uchafu wa zinaa nje ya ndoa.
Mengi yanaweza kusemwa kutokana na utamaduni huo, lakini kuna fikra moja msingi ambayo Waislamu wanapaswa kushikamana nayo. Uislamu ni mfumo kamili wa maisha uliokamilika ambapo kwamba, chimbuko lake ni Hukmu za Ki-Sheria. Hukmu hizo za kisheria ndio chanzo cha mila, desturi, utamaduni na matendo ambayo Muislamu ameruhusiwa kuyafanya. Kutokana na chanzo hicho (i.e Hukmu za Ki-sheria), Uislamu kwa uwazi umeharamisha kushiriki katika Sikukuu zote za kikafiri, kama vile kusherehekea sikukuu ya Valentine ambayo mwanzoni ilikuwa ya kipagani na kisha ikaboreshwa tena katika sura tofauti na kanisa na pia sikukuu nyengine zote.
Uislamu kupitia Hukmu za Kisheria umeeleza kwa uwazi ni zipi sikukuu za Kiislamu. Imeelezwa kwamba, Anas bin Malik (ra) amesema:
“Wakati Mtume (saw) alipokuja Madina, watu walikuwa wana skukuu mbili kutoka katika
masiku ya ujinga”. Yeye Mtume (saw) amesema: “Wakati nilipokuja kwenu, mulikuwa na
sikukuu mbili mulizokuwa mukisherehekea katika kipindi cha ujinga. Allah (swt) ameziondoa
na kuwapatia badala yake, Skukuu ya kuchinja (Eid-l-adha) na Eid-el-Fitr. (Ahmad)
Kwa hivyo, japokuwa kuna sikukuu nyingi katika ulimwengu lakini hizo ndio sikukuu zetu Waislamu ambazo Allah (swt) ametuchagulia. Kuigiza mila na vitendo vya kimagharibi ni mbinu ambayo makafiri hutumia kuwatumbukiza Waislamu katika mwenendo usiokuwa wa kiislamu. Kila mara makafiri wanafikiria jinsi gani
wataweza kuwamaliza kabisa Waislamu, na kujaribu kupanga mbinu mbali mbali ili kuweza kutimiza azma yao ya kuutokomeza kabisa Uislamu.
Katika jamii tunayoishi leo, kwa bahati mbaya, dhana ya mchanganyiko usiokuwa na mipaka baina ya wanawake na wanaume ni jambo linalopigiwa debe na makafiri na kupandikizwa katika mabongo ya Waislamu ili lionekane kuwa ni jambo la kawaida, na kututaka tuzikubali fikra zao hizo kwa kisingizio chao kwa kuwa sisi ni sehemu katika jamii yenye mila mchanganyiko (Multicultural Society).
Inafaa tuelewe kwamba umma wa Kiislamu unatakiwa uwe makini na kutambua mbinu hizo za makafiri, ili tuweze kuhuisha na kushikamana na uelewa wetu juu ya miondoko yetu ya kimaisha kama ilivyopokelewa kutoka katika Qur-an na hadithi za Mtume (Saaw). Uislamu wetu umeweka wazi juu ya jinsi gani Waislamu waishi maisha yao baina ya wanawake na wanaume, mahrim na wasiokuwa mahrim, katika maisha ya ndani (Private live) na maisha ya nje (Public life)nk.
Sikukuu ya Valentine ni moja ya mifano, ambapo mahusiano nje ya taasisi ya ndoa si tu huruhusiwa bali pia huhimizwa.Vyombo vya habari pamoja matangazo mbali mbali hupigia debe mahusiano hayo hasa katika sikukuu hiyo. Ni ukiukaji wa Sheri’a ulioje, ambapo mila hizi za kidemokrasia huwafanya vijana kuchanganyikiwa na kukimbilia mahusiano hayo kwa kutafuta kuwa na mpenzi hususan inavyohimizwa na sikukuu hiyo.
Takriban ulimwengu nzima, mashule, vyuo, vilabu vya usiku zimo katika maandalizi ya sherehe hizo za skukuu ya wapendanao. Pia kwa bahati mbaya huwajumuisha baadhi ya Waislamu waliochanganyikiwa katika matukio hayo ya michanganyiko ya jinsia tofauti kwa jina la mchanganyiko wa kimapenzi. Jambo linaloonesha namna baadhi ya Waislamu walivyokuwa mbali na fikra yao safi ya kiislamu na hatimaye kukumbatia fikra na mila za kikafiri. Ni vigumu kufikiria kile ambacho kanisa katoliki kilitaraji kukifikia kwa kutaka kuhifadhi taasisi ya ndoa na kuzipinga mila za kipagani na kuanzisha siku ya Mtakatifu Valentine! Hawakulifikia hilo kwa kuwa Ukiristo sio mfumo wa maisha na hivyo kimaumbile hauna nguvu na ujasiri
isipokuwa kusalimu amri kwa nidhamu ya kidemokrasia.
Na badala yake leo tunaona mahusiano ya kiholela ya kimapenzi yamerudi tena na yamezidi katika jamii, na sikukuu hii ya Valentine imekuwa ndio kichocheo kikubwa ambayo matokeo yake ni uzinifu, mimba nje ya ndoa, na utoaji wa mimba na yote yanayopelekea kuporomoka kwa maadili na kupoteza utukufu/ heshma ya jamii. Jee huo ndio ujumbe tunaotarajia kuwafikishia watoto wetu kutoka katika siku hii?
Katika Uislamu mahusiano ya kimapenzi baina ya mwanamke na mwanamume yameelezwa wazi wazi na Sheria kupitia utaratibu maalumu ambao ni ndoa. Ibn Masoud amesema kuwa. Mtume (saw) amesema:
“Enyi makundi ya vijana, yeyote mwenye uwezo wa kuoa na aoe kwani jambo hilo litamsaidia
kuinamisha macho yake, na itamuhifadhia sehemu zake za siri kutokana na uchafu wa zinaa. Na
asiyeweza kuoa basi na afunge kwani hiyo itakuwa ngao kwake”.
Hukmu za kisheria zinahakikisha kuwa jamii iliyosimama juu ya misingi hiyo itakuwa mbali na uzinifu wa kiholela na itakuwa na mwamko wa kimaadili. Mambo ambayo waziwazi yamekosekana katika jamii za kimagharibi na kwa bahati mbaya tunayaona yanafikishwa katika ardhi za Kiislamu pia.
Sheri’a inatambua mahitaji na hisia ya kimaumbile ya matamanio waliyonayo wanawake na wanaume na ndio maana zikaweka taratibu maalum katika kuzishibisha ghariza/hisia hizo na mahitaji hayo katika utaratibu ambao mwanadamu atapata utulivu bila ya kudhurika.
Sisi Waislamu tunapaswa kufahamu kwamba matendo yetu yote lazima yafuatane na Hukmu za Kisheria ikiwa ndio chanzo kitukufu cha mwongozo kwetu sisi. Aidha ikiwa ni kwa vitu vidogo vidogo au kwa maamuzi makubwa, katika maisha ya ndani (private) au ya nje (public), tunalazimika kutenda baada ya kufahamu kile alichokiteremsha Allah (swt) juu ya suala husika. Vyenginevyo tutaingia katika makucha ya mafisadi, kama vile uhuru, demokrasia, michanganyiko ya jinsia tofauti pamoja na maslahi binafsi. Vile vile ikiwa tutachukua taratibu zisizokuwa za kiislamu katika maisha yetu, kwa ajili ya kuwaridhisha wale waliotuzunguuka, lazima tufahamu kuwa kufanya hivyo kutatufanya tuwe madhalili na starehe zao zitakuwa pigo kwa dini yetu.
Allah (swt) anasema:
وَلَنْ تَرْضَى عَنْكَ الْيَهُودُ وَلاَ النَّصَارَى حَتَّى تَتَّبِعَ مِلَّتَهُمْ
“Hawataridhia Mayahudi na Manaswara mpaka mfate mila zao…” (TMQ 2:120).
Wakati umefika tuwe macho Waislamu na mbinu za makafiri, iwe katika michezo yao (movies), vitabu vyao vya hadithi, sherehe zao nk. Malengo makubwa ambayo wameyaficha makafiri katika vifua vyao yana athari mbaya kwa ummah wa kiislamu. Ni wakati wa kuamka na kutafuta dola yetu (Khilafah) katika ulimwengu ili tuonje ladha ya Uislamu kivitendo na kukomesha mila na sherehe potofu za kikafiri.
Adam J. Haji
Maoni hayajaruhusiwa.