Udukuzi wa Mitandao

Tukio la mwanasiasa Nape Nnauye na wanasiasa wenzake kuomba msamaha kwa Raisi kufuatia sauti za maongezi yao ya simu zilizosambaa siku za nyuma ni dalili ya wazi kwamba simu zao zilidukuliwa. Sauti hizo ambazo baadhi wanazihusisha kuwa dhidi ya Raisi zilizua mjadala ndani ya jamii, na hata kabla ya baadhi yao kuomba msamaha, mwanasiasa Bernard Membe yeye alikiri hadharani kwamba sauti iliyodukuliwa ni yake.

Udukuzi ni kitendo cha kuingilia bila ya idhini mfumo wa chombo cha kimawasiliano kama komputa, simu na mfano wake kwa ajili ya kujipatia au kujikusanyia taarifa fulani kutoka kwa mtumiaji. Mara nyingi kama sio zote suala la udukuzi huwa lina nia ovu.

Kitendo cha udukuzi kimekuwa maarufu kwa miaka mingi, na tamko udukuzi/ hacking lilianza kutumika ndani ya miaka ya 1970, na kuongezeka umaarufu ndani ya miaka ya 1980.

Udukuzi unaweza kutendwa kwa dhamira nyingi, kama vile katika wizi katika kadi za mabenki nk. Kuna udukuzi wa kiushabiki, kwa mfano, mdukuzi fulani kuonesha kipawa na ujuzi wake wa kucheza na kuingilia mfumo wa kimitandao. Pia kuna udukuzi unaosukumwa na ushindani wa kibiashara baina ya taasisi za kibiashara au makampuni makubwa katika kudhoofisha kampuni au biashara ya mpinzani. Bila ya kusahau udukuzi kwa maslahi ya kidola, baina ya dola moja kwa nyengine ili kupata siri au taarifa nyeti zitakazosaidia nchi moja katika malengo mbalimbali ya kisiasa , kiuchumi, kijeshi au kijasusi :
https://www.malwarebytes.com/hacker/

Kwa maumbile ya kibinadamu namna yalivyo ya kutaka kuhifadhi maisha (survival instinct) ikiwemo khofu ya kwekwa wazi faragha yake, ni wazi udukuzi unagusa roho ya maisha yake, kiasi cha kujenga khofu juu ya faragha na usalama katika matumizi ya mitandao mbalimbali hususan simu. Baada ya udukuzi wa sauti za wanasiasa hao tumeshuhudia uwepo wa kampeni fulani ya kususia mashirika ya simu yanayosemekana kushirikiana na wadukuzi.

Itakumbukwa kwamba mnamo mwezi wa Septemba 2018 mtandao wa Shirika la Habari la BBC ulisambaza taarifa kwamba mtandao wa kijamii wa Facebook unafanya udukuzi wa taarifa za wateja wake. Taarifa hiyo ilidai kwamba zaidi ya akaunti milioni 50 zilidukuliwa na kwamba shirika hilo la mtandao wa kijamii limepata ufumbuzi wa udukuaji wa taarifa.

Aidha, serikali ya Ujerumani imewahi kudai kudukuliwa taarifa zake. Gazeti la Berliner Zeitung la mwezi Machi 2018 linathibitisha kuarifiwa kuwa wadukuzi walikuwa wanaingilia mifumo ya mawasiliano ya serikali kuu ya Ujerumani kwa mujibu wa vyanzo vya usalama vilivyozungumza na gazeti hilo.

Mashambulizi hayo ya udukuzi yalikuwa yakichunguzwa na maafisa wa usalama wa Ujerumani, ambao walikuwa wakijaribu kutambua malengo na utambulisho wa wadukuzi hao.

Katika ulimwengu wa sasa suala la udukuzi wa taarifa za watu limekuwa la kawaida sana kutokana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia. Udukuzi wa taarifa umekuwa kama ni mbinu kubwa ya masuala ya kijasusi ulimwenguni. Mataifa hutumia gharama nyingi sana katika kudukua taarifa. Kwa kupitia mbinu hii hupata taarifa nyingi sana. Halkadhalika, mitandao ya kijamii hupata fedha nyingi sana kwa kuuza taarifa za wateja wake kwa makampuni ya kibiashara na mashirika ya kijasusi.

Udukuzi unafedhehi wazi wazi fikra ya kiuongo ya kidemokrasia kwamba ni mfumo unaochunga faragha na ‘uhuru binafsi’. Ilhali kaulimbiu hiyo ni bango tupu bila ya uhalisia.

Hapana shaka yoyote kwamba Uislamu unapinga wazi wazi fikra za ‘uhuru binafsi’ kwa kuwa mwanadamu hayuko huru katika ulimwengu huu kwa kuwa ni kiumbe cha Mwenyezi Mungu ambae kaleta maagizo maalumu nayotaka mwanadamu ayatekeleze bila ya khiyari.

Lakini haina maana kwamba Uislamu hauchungi mipaka ya faragha ya mtu. Dola ya Kiislamu ya Khilafah inasimamia raia katika maisha ya kiinje na kamwe haifuatilii maisha yao ya faragha, na ikitokea kuna mtawala kawafanyia ujasusi raia bila ya haki iwe kwa udukuzi au namna nyengine, hapo raia ana haki kufungua mashtaka kupitia kwa Afisi maalumu inayodhibiti kusiwe na dhulma za mtawala kwa raia, yaani Kadhi Madhalimu. Aidha, Afisi hiyo endapo tu itapata fununu juu ya tabia hii au dhulma yoyote ya mtawala au mmoja katika watumishi wa Umma, hata kabla ya mdhulumiwa hajaleta malalamiko kwa mahakama hiyo, huwa ni wajibu kwa Mahkama hiyo kutafanya uchunguzi wa jambo hilo kuona kama mtawala hawadhulumu raia.

Kaema Juma

Risala ya Wiki No. 55

12 Muharram 1441 hijri 11/09/2019 Miladi

Afisi ya Habari – Hizb ut- Tahrir Tanzania

https://hizb.or.tz/

https://www.facebook.com/Hizb-ut-Tahrir-Tanzania

Maoni hayajaruhusiwa.