Uadilifu wa Uislamu Zama za Khilafah

Leo ulimwengu unapita katika hali ya aibu na fedheha. Baada ya kumakinika mizizi ya utawala wa mfumo wa kibepari wa kimagharibi hakuna kunachotarajiwa isipokuwa ni dhiki na dhulma kwa wanadamu hususan wanyonge. Mfumo huu umekuwa ndio chanzo cha husuma katika ulimwengu, umasikini uliokithiri hasa katika ulimwengu wa tatu na kuwafanya wasionacho hawana haki pindi wanapokuwa na utesi na wenye nacho.

Mfumo huu wa ulafi umesababisha maafa makubwa katika kuwatumikisha wanadamu kama wanyama kuanzia zama za utumwa, ukoloni mkongwe na ukoloni mambo leo ulioshika hatamu leo.

Aidha, ni mfumo ulioleta uporaji wa ardhi na kuzikalia nyengine kimabavu, hali inayoendelea hasa katika maeneo yanayokaliwa zaidi na Waislamu kama vile Kashmir, Palestina nk. Hali hii ni sehemu ya natija/ matokeo ya mfumo huu ulioshindwa kutoa na kusimamia haki hata katika mambo ambayo yako wazi.

Leo wanadamu wanapaswa kujifunza na kuchukua mazingatio kutokana na uadilifu wa Uislamu ulivyokuwa ukisimamiwa na makhalifa wake katika zama zilizotangulia.
Viongozi wa dola ya Kiislamu (Makhalifa) walisimama kidete kusimamia na kutoa haki kwa watu wote bila ya kuzingatia rangi, kabila wala dini.

Kuna tukio kubwa na adhimu la uadilifu wa Uislamu lilitokea katika zama za Khalifa wa Pili wa Kiislamu Umar bin Khatwab ra. ndani ya Misri. Imepokelewa kuwa pindi Waislamu walipofungua Masri, gavana wa eneo hilo Amru Ibnul Ass aliamua kuupanua msikiti mkubwa jamia kwa ajili ya kutosheleza na kuchukuwa watu wengi kuswali kwa wakati mmoja kutokana na idadi kubwa ya jamii ya maqibty kusilimu.
Gavana akataka kununua kipande cha ardhi kilichopo jirani na msikiti kilichokuwa kikimilikiwa na mama mmoja wa kikristo. Mama huyo baada ya kuombwa kuuza ardhi yake kwa Waislamu akakataa kwa madai kuwa ni ardhi ya mayatima, na yeye ni msimamizi tu wa mali yao. Hakika hoja ya mama huyu ilikuwa na nguvu, licha ya kuwa Waislamu wakati huo walikuwa na haja ya kuupanua msikiti wao.

Gavana wa Kiislamu nchini Misri akatumia hila na `akachukua kipande kile cha ardhi na kupanua msikiti bila ridhaa ya msimamizi wa kiwanja kile cha mayatima.
Mama yule wa kinaswara akaamua kulipeleka jambo hilo kwa mapadri na baadhi ya makasisi wa kanisa. Baada ya mashauriano baina ya yule mama na makasisi wakakata shauri kuwa mama yule aende Madina, makao makuu ya serikali ya Kiislamu akamuone na kushtaki kwa kiongozi mkuu, yaani Khalifah.

Ndipo mama yule wa kinaswara alipofunga safari ndefu mpaka Madina, alipofika huko akiwa ameongozana na mtumishi wake, akakutana na kiongozi wa Kiislamu ambaye ni Umar ra. Mama yule alipomwona Umar ra. alishangaa kuona kiongozi yule mtu wa kawaida na amevalia mavazi ya kikawaida kabisa. Mama kutoka Misri akamuuliza, Umar, wewe ndio Umar, Umar ra. akamjibu ndio ni mimi Amiri wa Waumini.

Kisha, mama akaanza kueleza na kushtakia kesi yake iliyomtoa Misri mpaka Madina, baada ya Umar ra. kumsikiliza kwa makini, akaomba kipande cha karatasi na kuandika sentensi moja yenye ujumbe mfupi unaosomeka: ‘iweje Mfalme Kisra awe mwadilifu kuliko sisi (Waislamu). Na amani ni kwa atakayefuata uongofu’

Kisha akampatie barua ile mama yule na kumwomba ampelekee Gavana wa Misri. Baada ya mama yule kupatiwa ujumbe ule akaondoka na mtumishi wake kurejea Misri, njiani akaamua kufungua na kuisoma ile barua, akashangaa na kuanza kusema huyu mtu (Umar) ni timamu kweli ? Hivi nimekuja huku mwisho wa dunia kweli nitapata haki yangu? uko wapi uadilifu wa Umar unaosemwa? basi mama huyu akaitupilia mbali ile barua yenye ule ujumbe, na kurudi zake Misri. Kwa bahati nzuri baada ya yule mama kuitupa ile barua, yule mtumishi wake kwa busara kubwa akaiokota na kuihifadhi pasina kuonekana na yule mama, ili wakifika Misri awaonyeshe makasisi waone jinsi gani Umar alivyowadharau kwa majibu yake mabaya.

Mama na mtumishi wake walipofika Misri, makasisi na mapadre walikuwa na shauku kubwa ya kusikiliza maamuzi ya Umar juu ya kesi ile ili wapate fursa ya kuusakama Uislamu uliosifika zama hizo kwa uadilifu na kutoa haki hata kwa wasiokuwa Waislamu.

Viongozi wa kikiristo wakasimuliwa yote aliyojibiwa yule mama na Umar, na barua yenye ujumbe aliyopewa, lakini kwa bahati mbaya yule mama hakuwa na ushahidi wa kuthibitisha madai yake kutokana na kuwa aliitupa ile barua yenye ujumbe uliokuwa fumbo kwake. Ndipo makasisi wakaanza kumlaumu huyu mama kwa hatua yake ya kuutupa ujumbe ule huku wakisema, kwa nini hukuuhifadhi ili wapate ithibati ya ouvu na unyama wa Waislamu?

Katika hali hiyo ndipo yule mtumishi wa mama alipoutoa ule ujumbe na kuwapa makasisi. Makasisi wakafurahi na kuuchukua ujumbe ule na kwenda nao moja kwa moja mpaka kwa Gavana Amru Ibnul Aas, wakamkuta akiwa kazunguukwa na walinzi akiwa anateremka juu ya kipando chake, hapo Kasisi Mkuu akamkabili na kumsimulia kile kilichotokea huko Madina katika safari ya yule mama, mmliki wa kile kipande cha ardhi. Basi Amru Ibnul Aas alipofungua ile barua na kusoma ujumbe uliosomeka : ‘Iweje Mfalme Kisra awe mwadilifu kuliko sisi (Waislamu). Na amani ni kwa atakayefuata uongofu”.

Tahamaki makasisi wakaanza kumsakama Amr Ibnul Aas kwa maneno ya fedheha kutokana na ujumbe ambao wao hawafahamu maudhui yake.

Amru Ibnul Aas baada ya kuusoma ujumbe ule, anasimulia yule mama wa Kiqibty, alionekana uso wake umebadilika, akaanza kutetemeka na kuishiwa nguvu mpaka kushindwa kusimama vyema, hadi kuegemea ukuta wa msikiti ambao sehemu yake umejengwa ndani ya kiwanja cha yule mama bila idhini yake.

Hapo gavana Amru Ibnul Ass akasema kwa upole kumwambia yule mama pamoja na ujumbe mkubwa wa makasisi wa Misri, nimekuja hapa msikitini kwa ajili ya kuswali, mkipenda niruhusuni kuswali, kisha nibomoe sehemu iliyoingia kwenye kiwanja chako, au kama hamtoniruhusu kuswali, basi nitavunja sehemu tuliyojenga katika ardhi yako sasa hivi kabla sijaswali.
Ndipo mama wa Qibti na jopo la makasisi wakamaruhusu Gavana aswali kwanza, lakini akimaliza ahakikishe anawafafanulia kuhusu ujumbe ule.

Baada ya swala ndipo gavana wa Kiislamu Amru Ibnul Aas akaanza kuelezea maaana ya ujumbe ule. Akawasimulia kuwa Umar bin Khataab kabla ya kusilimu kwake alikwenda safari ya kibiashara huko katika nchi ya Fursi, ikaswadifu siku moja akiwa huko Mfalme Kisra alikuwa na sherehe katika masiku ya mwaka mpya mbele ya kasri lake, jirani ya kasri hiyo kulikuwa na bibi kizee ambaye alikuwa akipitisha mifugo yake mbele ya kasri lake.

Ilikuwa ada ya hapo, pindi alipokuwa akipita bibi huyo na mifugo yake wakati wa sherehe, basi sherehe zilisimama kwa muda, baada ya kupita yule bibi sherehe ziliendelea mbele ya ikulu hiyo ya Kisra. Siku moja wakati sherehe zikiendelea ng’ombe mmoja wa yule bibi alipita kwenye majlis ya Mfalme Kisra na kujisaidia juu ya zulia lake. Mmoja wa walinzi wa Kisra alichukuwa silaha yake na kumkata ng’ombe wa yule bibi na kumuua. Baada ya tukio lile Mfalme Kisra alitoa amri ya kuuwawa mlinzi wake yule kutokana na tukio alilolifanya la kumuua ng’ombe wa yule bibi kizee. Kutokana na tukio lile Umar ra. wakati ule alitaka kujua huyu bibi kizee ni nani, iwapo ana mahusiona na mfalme? wenyeji wakamueleza kwa kumsimulia Umar kuwa, yule bibi kizee alikuwa na ardhi kubwa, akiishi nyuma ya kasri la Mfalme, pindi Mfalme alipotaka kupanua kasri lake alimwomba ajuza huyu amuuzie kipande chake cha ardhi sehemu ya nyuma, lakini bibi kizee akakataa, baada ya Mfalme kumshawishi kwa muda mrefu bibi yule bado akakataa, ndipo Mfalme Kisra akaamua kumpa sehemu yake ya ardhi nzuri yenye rutba iliyo mbele ya kasri lake. Bibi yule akamkubalia Mfalme lakini akamwambia Mfalme ‘nachelea nikiwa napita mbele ya kasri lako walinzi wako watakuwa wananisumbua na kunizuiya, ndipo Mfalme Kisra alipoandika mkataba kati yake na ajuza yule, kuwa asikhofu, na yeyote atakayemsumbua bibi huyo hukmu yake ni kuuwawa.

Amru ibnul Aas alikuwa akisimulia kisa hiki huku akitokwa na machozi. Umar ra. alikuwa anamuonesha gavana huyo kwamba sisi Waislamu ndio tuna haki zaidi ya kuwafanyia raia na watu jumla uadilifu hata kuliko Mafursi ambao ni makafiri. Basi jee kwa nini anafanya hivyo kumdhulumu yule mama wa qibtiy ardhi yake?
Ardhi ya mama yule alirejeshewa mwenyewe, na eneo hilo limebaki kuwa ni eneo la kanisa mpaka leo hii nchini Misri. ( Bidaya wa nihayya)

Enyi makasisi, wakristo na wasiokuwa waislamu jumla: Hivi ndivyo walivyokuwa makhalifa wa Kiislamu katika kusimamia uadilifu hata pale magavana walipojaribu kuwadhulumu wakristo walisimama kidete kuwatetea. Basi vipi leo mnawakumbatia na kushirikiana na viongozi wa mfumo wa kibepari kuwadhulumu Waislamu, viongozi hao kwa ujanja wakiwasahaulisha uadilifu na insafu ya Waislamu na Uislamu juu yenu katika tareekh, zama ulipokuwa Uislamu umeshika hatamu katika ulimwengu huu?

Ni wakati muwafaka sasa kwa wasio kuwa Waislamu kuutafiti Uislamu kwa jicho huru pasina kuburuzwa na propaganda, kisha kuungana na Umma wa Kiislamu kuubadilisha ulimwengu huu uliojaa dhulma za makucha ya ukoloni wa kibepari uliootesha matawi ya miti mibaya katika mgongo huu wa ardhi.

وَمَثَلُ كَلِمَةٍ خَبِيثَةٍ كَشَجَرَةٍ خَبِيثَةٍ اجْتُثَّتْ مِنْ فَوْقِ الأَرْضِ مَا لَهَا مِنْ قَرَارٍ (إبراهيم: 26).

‘Na mfano wa neno baya, ni kama wa mti mbaya ambao umeng’olewa katika
ardhi, hauwezi kubakia (TMQ 14: 26)

Issa Nasibu

Risala ya Wiki No. 59

24 Swafar 1441 hijri 23/10/2019 Miladi

Afisi ya Habari – Hizb ut- Tahrir Tanzania

https://hizb.or.tz/

https://www.facebook.com/Hizb-ut-Tahrir-Tanzania

Maoni hayajaruhusiwa.