Uadilifu Wa Uislamu
بسم الله الرحمن الرحيم
Tukiwa ndani ya mwezi mtukufu wa Ramadhani, hatuna budi kuangazia tukio kubwa lilitokea ndani ya mwezi huu ambalo ndilo lenye fadhila kubwa zaidi, nalo ni tukio la kuteremshwa Quran.
Amesema Mola SW:
“Mwezi wa Ramadhani ambao iliteremshwa Quran kuwa mwongozo kwa watu”
Hakika katika aya hii tunapata lengo hasa la kuteremshwa kitabu kitukufu cha Quran, nalo ni kuwa mwongozo kwa watu wote pasina kuangalia dini zao, rangi wala makabila yao.
Sifa hii kubwa ya mwongozo huu ndio imeufanya kuwa na hadhi ya kipeee kiasi kwamba licha ya kuwa unasimamiwa na Waislamu, lakini haiwazuilii kuwafanyia uadilifu wasiokuwa Waislamu pale wanapohukumu baina yao au baina ya Muislamu na asiyekuwa Muislamu, kwani mwongozo huu huwaamrisha kuwahukumu watu kwa uadilifu na kusimamia mambo kwa insafu ya hali ya juu.
Historia ya utawala wa Kiislamu wakati Waislamu walipokuwa wameshika hatamu katika dunia hii hawakusita kusimamia watu kwa uadilifu. Moja kati ya tukio kubwa linalodhihirisha uadilifu mkubwa wa Uislamu lilitendwa na mausisi wa Khilafah Uthmaniya kwa jina Uthman bin Artoghar ambaye moja kati ya kesi mashhuri aliyohukumu ilikuwa ni baina ya Muislamu na mkristo wa Benzatania (mabaki ya dola ya Roma), mkristo huyu awali aliuliza kwa Khalifah: vipi utaweza kunihukumu kwa uadilfu, hali ya kuwa mimi sio katika dini yako? Khalifah Uthman akamjibu, vipi nisikuhukumu kwa uadilifu, na Mola tunayemwabudu anatuamrisha kufanya uadilifu ndani ya Quran tukufu. Kisha akasoma aya isemayo :
“Hakika Allah SW anawaamrisha (Waislamu) mrudishe amana kwa wenyewe, na mnapohukumu baina ya watu basi muhukumu kwa uadilifu”
Basi ikawa hukmu hii ni sababu ya kusilimu kwa mkristo huyu wa kiroma, kwa jinsi kiongozi alipompatia haki yake, tena kwenye nchi ambayo yeye alikuwa mgeni. Mkiristo huyu alishuhudia uadilifu wa Uislamu kivitendo na sio maneno pekee ambao haukuzingatia misingi ya udini, ukabila wala rangi ya mtu.
Watawala wa Kiislamu daima walikuwa wakisimama juu ya misingi ya uadilifu bila ya kuzingatia haiba, cheo wala hadhi ya mtu. Itakumbukwa kwamba Khalifah wa kwanza Abu Bakar (ra.) baada ya kufariki Mtume SAAW alitamka maneno ya kihistoria aliposema katika sehemu ya khutba yake mara baada ya kuchaguliwa kuwa Khalifah:
“Dhaifu kwenu ni mwenye nguvu kwangu mpaka nimpatie haki, na mwenye nguvu kwenu ni dhaifu kwangu mpaka nichukue haki ya yule aliyemdhulumu”
Aidha, Sheikh ul-Islam Ahmad bin Taymiya aliwahi kusema:
“Hakika Mola ananusuru dola ya watu waadilifu hata kama ni makafiri, na wala hanusuru dola ya watu madhalimu hata kama ni Waislamu”.
Mwezi wa Ramadhani uwe na msukumo wa ziada kwetu katika kuhakikisha tunafanya kazi ya ulinganizi ili uadilifu wa Uislamu uweze kuhisika na kuonekana kivitendo mpaka wasiokuwa Waislamu waone uhalisia na usafi wake kinyume na propaganda za kiuadui zinazoenezwa leo na mataifa ya magharibi chini ya kinara wao Marekani.
Issa Nasibu
#RamadhanNaMuongozoWaQuran
Maoni hayajaruhusiwa.