Tuyakimbilie Mafunzo ya Mtume (saaw) Yenye Nuru kwa Wanadamu Wote
Katika mwezi wa Rabi ul Awwal (mfunguo sita) Mwaka wa Ndovu (miaka 53 kabla ya Hijra) kipenzi chetu, mtukufu na mwisho wa Mitume, Bwana Muhammad bin Abdullah SAAW alizaliwa.
Kwa munasaba wa uzawa huo Waislamu katika kila pembe ya ulimwengu hukumbuka uzawa wake kwa namna mbali mbali.
Katika kuukumbuka uzawa huo ni muhimu kutilia maanani kwa kina kwamba haiba au dhati ya kila mwanaadamu akiwemo Mtume (SAAW) hupatikana kwa uwepo mambo mawili makubwa:
Kwanza,hujengwa juu ya aqlia ya mtu husika. Aqlia humaanisha aina ya ufahamu anaoubeba mtu, mtazamo jumla na msimamo fulani anaoutoa juu ya qadhia mbali mbali zilizomzunguuka.
Kwa mfano, kama mtu anatembea barabarani na akamuona mwanamke akiwa bila ya nguo za stara ya kisharia, mtu mwenye aqlia ya Kiislamu huhuzunishwa na hatofurahishwa na jambo lile kutokana na aqlia aliyonayo kwamba mwanamke kutembea bila ya stara ni jambo la haramu. Hapo mtu huyo huwa katika jambo hilo kaongozwa na kusukumwa na uoni sahihi wa Kiislamu (aqlia ya Kiislamu) katika kuliona suala lile stara. Amma akija na hukmu kinyume na hiyo, hapo huwa si aqlia ya Kiislamu.
Kitu cha pili kinachotengeneza haiba (personality) ya mtu ni nafsiya yake. Nayo ni ile namna anavyotenda matendo yake ya kila siku kufuatana na aqlia (ufahamu) aliyoibeba. Kwa sababu mtu hutarajiwa kutenda matendo kwa mujibu wa aqlia anayoibeba. Kwa hivyo, kwa ufupi aqlia mahala pake ni kichwani kwa kuwa ni ufahamu tu unaobebwa na mtu, na nafsiya ni matendo yanayotendwa ambayo ni dhihirisho la ufahamu alionao mtu (aqlia)
Katika kuadhimisha uzawa wa Mtume (SAAW) ni lazima tukumbuke kwamba yeye Mtume SAAW ni nuru iliyokuja kubadilisha ulimwengu uliokuwa umesheheni kila aina ya viza vya ujahiliyya kwa kulingania watu kushikamana na ufahamu (aqlia) maalum wa Kiislamu, na kuzitegemeza aina zote za ufahamu, juu ya fahamu hii msingi ya ‘La ilaha illa Allah, Muhammad Rasulullah’ na kuifasiri aqlia hiyo kivitendo kwa nafsia ya Kiislamu.
Mtume SAAW nae akatutaka sisi tujifunge na aqlia sahihi ya Kiislamu kwa kumfuata yeye pekee aliposema:
“ Hajaamini mmoja wenu mpaka matamanio ya nafsi yake yafuate yale niliokuja nayo (yaani Sheria za Kiislamu).”
Watu hutofautika kwa mujibu wa aqlia na nafsia zao, wala hawawezi kattu kuwa sawa wale wenye aqlia ya ‘La ilaha illa Allah, Muhammad Rasulullah’ na wale wenye aqlia na nafsia kinyume na hiyo.
Kwa hivyo, kumkumbuka na kumtukuza Mtume (SAAW) kusidhihirike tu katika kusherehekea mazazi yake kwa kutamka ki-ulimi tu, bali kudhihirike katika kujifunga kiudhati na aqlia na nafsia sahihi iliyosheheni nuru na ambayo haithiriwi na zama wala watu.
Hakuna wakati ambao aqlia na nafsia aliyokuja nayo Mtume SAAW inahitajika zaidi kama wakati huu ambapo dunia imerudi katika viza hata kuliko zama za waarabu, licha ya uwepo wa yanayoitwa maendeleo ya sayansi na teknologia.
Leo takriban ulimwenguni kote kuna vurugu katika siasa za kibepari ambazo zimejengwa juu ya ‘umaslahi maslahi’. Dhulma za kiuchumi ambazo kila siku zinaongeza umaskini na kukuza mwanya baina ya walionacho na wasionacho, upande wa kijamii ambapo fikra duni na batil za ‘uhuru’ zimewafanya wanadamu kutenda na kutetea mambo machafu ambayo hata wanyama hawadiriki kuyatenda, kama ushoga, usagaji nk. Bila ya kutaja kuvurugika kwa amani na kusheheni vita kila mahali kwa maslahi madogo ya vibaraka na makubwa ya madola ya kibepari ya kikoloni.
Kwa Waislamu jukumu kubwa tulilonalo ni kuhuisha maisha ya Kiislamu kwa kujifunga na aqlia na nafsia yenye nuru aliyokuja nayo Mtume (SAAW) na kuisimamisha na kuisambaza ulimwenguni kote. Kwa kuwa Mtume SAAW katumwa kuwa Rehma kwa walimwengu wote.
Amma wasiokuwa Waislamu wao ni hii fursa adhimu kutafiti kwa kina na kwa uadilifu mafunzo ya Mtume SAAW yaliyojaa nuru kwa wanadamu wote bila ya kuzingatia rangi, kabila au asili. Basi tunawanasihi wapatilize fursa hii ili wauone ukombozi wa kweli kinyume na mfumo thaqili na wa dhulma wa klibepari
Risala ya Wiki No. 19
Rabiul Awwal 1440 Hijri / Novemba 2018 Miladi
Afisi ya Habari – Hizb ut- Tahrir Tanzania
https://hizb.or.tz/
https://www.facebook.com/Hizb-ut-Tahrir-Tanzania
Maoni hayajaruhusiwa.