Tuviangazie Vita Vya Swiffin Kimfumo Zaidi (Swafar 37 Hijria)

بسم الله الرحمن الرحيم

Mwezi kama huu Swafar 37 AH ndipo vilipotokea Vita vya Swiffin, vilivyopiganwa baina ya Waislamu wao kwa wao. Upande mmoja wa vita ukiongozwa na Khalifah wa nne wa Waislamu Imamu Ali Abi Twalib na upande wa pili wa waasi dhidi ya dola ukiongozwa na Muawiyah bin Abu Sufyan.
Hapana shaka yoyote mgogoro wa vita hivi uliacha fitna na athari kubwa kwa Waislamu ambao ni Umma mmoja.
Hata hivyo, kwa bahati mbaya baadhi ya Waislamu huichukulia historia kama chanzo cha kuendeleza migogoro baina yetu badala ya kujifunza na kuzikabili changamoto kwa lengo la kusonga mbele.
Tukumbuke kuwa dola ya Marekani ilikabiliwa na vita vya wao kwa wao vinavyoitwa American Civil War (1861- 1865) tena kwa muda mrefu. Upande wa Kusini ukipigana dhidi ya upande wa Kaskazini.
Upande wa Kusini ambao ulitaka kujitenga na dola hiyo ulihusIsha majimbo (states) kadhaa kama Carolina, Mississipi, Florida, Alabama, Georgia, Lousiana, Texas, Upper South—Virginia, Arkansas, Tennessee, North Carolina nk.
Vita hivi vilipiganwa kwa miaka minne na kuleta madhara makubwa kwa jamii ya Wamarekani ikiwemo kuathiri uchumi, miundombinu, mahusiano baina yao na kubwa zaidi kuuwawa watu karibu laki nne.
Hata hivyo, kisha wamarekani wakasema sasa imetosha, wakazika husuma na uadui baina yao katika kaburi la historia na kujenga upya nchi yao kwa bidii, muhanga na maarifa ya hali ya juu, hatimae nchi yao imeibuka kuwa dola kubwa katika ulimwengu hususan kuanzia mara baada ya Vita ya Pili baada ya kuzishinda changamoto mbali mbali.
Waislamu lazima tuvichukulie Vita vya Swiffin, Vita vya Jamal (Ngamia) nk. walivyopigana Waislamu dhidi ya Waislamu wengine kwa namna hiyo. Japo kweli kuna makosa yaliyotendwa na baadhi ya Waislamu, lakini watendaji wake leo hawapo.
Sisi kama Ummah bora, tusiteswe na kutesana na historia au kuanza kusononeka na kunyoosheana vidole, bali tubebe jukumu kubwa tulilopewa, nalo ni kuibeba ajenda ya kurejesha tena maisha ya Kiislamu kwa kupitia kuutawalisha Uislamu wote kwa ukamilifu kwa kurejesha tena dola yake ya Khilafah inayostahiki kuanzia ndani ya nchi kubwa za Waislamu zenye vigezo vya kisharia kisha kuenea ulimwenguni, kuunganisha Waislamu na kuwakomboa wanadamu kwa jumla.
Risala ya Wiki No. 190
25 Safar 1446 Hijri / 28 Agosti 2024 Miladi
Afisi ya Habari – Hizb ut Tahrir Tanzania

Maoni hayajaruhusiwa.