Tuviangazie Vita Vya Siffin Kimfumo Zaidi

Mwezi kama huu wa Dhulhijja mwaka wa 36 Hijria ndipo vilipoanza Vita vya Siffin, vilivyopiganwa baina ya Waislamu, wao kwa wao. Upande mmoja wa vita ukiongozwa na Khalifah wa Waislamu Imamu Ali Abi Twalib ra.

Kwa bahati mbaya baadhi ya Waislamu huichukulia historia kama chanzo cha mateso na migogoro baina yetu badala ya kujifunza na kuzikabili changamoto kwa lengo la kusonga mbele.

Tukumbuke kuwa dola ya Marekani ilikabiliwa na Vita vya wao kwa wao vinavyoitwa The American Civil War (1861- 1865). Upande wa Kusini ukipigana dhidi ya upande wa Kaskazini.
Upande wa Kusini ambao ulitaka kujitenga ulihusuisha majimbo / states kadhaa kama : Carolina, Mississippi, Florida, Alabama, Georgia, Louisiana, Texas, Upper South—Virginia, Arkansas, Tennessee, North Carolina nk.

Vita hivi vilipiganwa kwa miaka minne na kuleta madhara makubwa kwa jamii ya Wamarekani ikiwemo kuathiri uchumi, miundombinu, mahusiano baina yao na kubwa zaidi kuuwawa watu karibu laki nne.

Hata hivyo, kisha wamarekani wakasema sasa imetosha, wakazika husuma na uadui baina yao katika kaburi la historia na kujenga upya nchi yao kwa bidii, muhanga na maarifa ya hali ya juu, hatimae nchi yao imeibuka kuwa dola kubwa katika ulimwengu hususan kuanzia mara baada ya Vita ya Pili baada ya kuzishinda changamoto mbali mbali.

Waislamu lazima tuvichukulie Vita vya Siffin na Vita vya Jamal (Ngamia) walivyopigana Waislamu dhidi ya Waislamu wengine kwa namna hiyo. Japo kweli kuna makosa yaliyotendwa na baadhi ya Waislamu, lakini watendaji wake leo hawapo.

Sisi kama Ummah bora tusiteswe na kutesana na historia au kuanza kusononeka, bali tubebe jukumu kubwa tulilopewa, nalo ni kuibeba ajenda ya kurejesha tena maisha ya Kiislamu kwa kupitia kuutawalisha Uislamu wote kwa ukamilifu kwa kurejesha tena dola yake ya Khilafah inayostahiki kuanzia ndani ya nchi kubwa za Waislamu zenye vigezo vya kisharia kisha kuenea ulimwenguni kote.

#UislamuMfumoMbadala

4 Septemba 2018

Masoud Msellem

Maoni hayajaruhusiwa.