Tuukumbuke Usiku Wa Aqaba

Kwa wanaofahamu sira ya bwana Mtume SAAW usiku wa kuamkia leo yaani 13 Dhul hijjah ndio usiku ambao Mtume Muhammad SAAW alipata nusra kutoka kwa makabila mawili makubwa ya Madina, yaani makabila ya Aus na Khazraj(Answar).

Nusra hiyo ilikuwa ndio chimbuko la mabadiliko ya kimfumo ndani ya Bara Arabu na ulimwengu kwa ujumla, na pia ilibadili hali waliyokuwa nayo wanadamu wakati huo kuanzia hali mbaya ya kijamii, kiuchumi na kisiasa.

Kikao cha Aqaba ya Pili (Kiapo cha Damu) kilichofanyika usiku huo ambacho kama walivyosimulia wanatareekh wakubwa wa Kiislamu kama Ibn Ishaqa na Ibn Hisham usiku wake kilihudhiriwa na majemadari wakubwa na watu wenye ushawishi wa kisiasa (Ahlu alhal wal aqd) kutoka Madina wakiwemo wanawake wawili, Bi Asmaa na Bi Nusayba(ra).
Mara baada ya kiapo hicho Ibilis alipiga kelele kubwa kuashiria kushindwa kwake kuizuiya nuru ya Allah SW.

Hivyo, usiku wa leo ni usiku wa kuenziwa na Waislamu kwa heshima na hadhi kubwa kwani usiku huu ndio uliopelekea tukio kubwa la Hijra ya Bwana Mtume Muhammad SAAW iliyopelekea kuasisi dola ya mwanzo ya Kiislamu na kuandikwa upya historia ya Waislamu na wanadamu kwa jumla.

#UislamNiHadharaMbadala

Na Ust. Issa Nasibu

Maoni hayajaruhusiwa.