Tutupie Jicho Furaha za Muislamu

Mazingatio ya Ramadhani – 6

Mtukufu wa darja Mtume SAAW kwa munasaba wa Swaumu katueleza kuwa mfungaji hupata furaha mbili kubwa, kwa kauli yake aliposema katika hadithi :

للصائم فرحتان : فرحة عند فطره وفرحة عند لقاء ربه
“Kwa mfungaji kuna furaha mbili, furaha wakati wa kufuturu, na furaha wakati atapokutana na Mola wake”(Muslim)

Katika mwezi huu wa Ramadhani ni vyema InshaAllah kuziangazia furaha hizo kwa kina ili tupate mwanga na ufahamu utakaotusaidia ndani ya Ramadhani na hata baada ya kumalizika.

Ni muhimu awali kuziangazia furaha za Muislamu kwa ujumla wake kwa sura ifuatayo:

Furaha ya kwanza ambayo kila Muislamu huwa nayo ni katika upande wa kiimani, kwa kule kukiri kwake na kuikubali neema kubwa ya Uislamu na yaliyo ndani yake katika aqida kama uwepo wa Allah SW, kutumilizwa Mtume SAAW na kuletwa muongozo wa Quran ambao ni muongozo kwa wanadamu wote, kama Ramadhani inavyotukumbusha. Hayo ni mambo makubwa na matukufu yaliyomletea mwanadamu majibu msingi na thabiti ambayo kamwe kwa akili yake asingeweza kuyapata. Hivyo, hufungua kifua cha Muislamu kwa furaha: Allah Taala anasema:

قُلْ بِفَضْلِ اللَّهِ وَبِرَحْمَتِهِ فَبِذَلِكَ فَلْيَفْرَحُوا هُوَ خَيْرٌ مِمَّا يَجْمَعُونَ (يونس:
“Sema kwa fadhila za Allah na Rehma zake! Basi kwa hayo na wafurahi. Haya ni bora kuliko hayo wanayoyakusanya” (Yunus : 58)

Katika maelezo ya aya hii, Sheikh Ali Muhsin Barwan (Allah Amrehemu) katika Tafsiri yake ya Kiswahili (Al-Muntakhab) kaandika haya :

“Ewe Mtume! waambie : Furahieni fadhila ya Mwenyezi Mungu na Rehma Yake juu yenu kwa kuiteremsha Quran, kubainisha Sharia ya uislamu. Na hili ni bora kuliko starehe zote anazozikusanya mtu duniani..”

Amma furaha ya pili kwa Muislamu ni ile hali ya kuridhika na qadhaa ya Mola wake katika hali yoyote iwayo, hilo pia huwa ni furaha kwake. Kwa kuwa hutuliza moyo wake, akiwa katika neema humshukuru Mola wake, na akiwa katika dhiki, mashaka na mitihani huridhika kwa subra na kubakia na dhana njema kwa Mola wake. Hili ni kama alivyogusia Mtume SAAW, kwamba Muumini huwa katika hali ya kheri katika hali yoyote akipata neema hushukuru, akikosa husubiri.

Furaha nyengine ya tatu ni Muislamu anapotumia neema aliyoruzukiwa. Jambo hili ni furaha kubwa kwa Muislamu, na asili hili huwa ni furaha kwa kila mwanadamu kutokana na uwepo ndani ya nafsi ya kila mwanadamu hisia ya ndani/ ghariza ya kutaka kubakia maishani (survival instinct) inayomsukuma kujitakia na kujitafutia mazuri mazuri katika maisha yake, na hapana shaka akiyapata huwa na furaha, na Uislamu haujalipinga hilo. Kama Mtume SAAW alipotaja kwamba “miongoni mwa mambo yanayoleta furaha ni mtu kupata rizki yake katika mji wake, kuwa na mke mwema, kudiriki nyumba ya wasaa na kuwa na kipando kizuri”.

Hata hivyo, kwa kuwa matumizi ya neema hizi kwa Muislamu huwa yana fungamano ( roho) na Mola wake, yaani kila anachokifanya Muislamu iwe ni katika matumizi ya neema ile au mengine ni kwa ajili ya kutaraji malipo kwa Mola wake. Hapo huwa kwake Muislamu ni furaha ya kikweli, kwa kuwa katika kutasaruf/ kutumia neema hizo kumepatikana ‘uroho’ (fungamano na Mola wao) ndani yake. Ndio maana japo na makafiri nao kiudhahiri wanapokuwa na neema hujihisi na kudhani wana furaha, lakini kwa kukosa kwao huo ‘uroho’ (fungamano la kweli na Mola wao) kwao huwa sio furaha, kwa kuwa katika matumizi ya neema ile hawakuweka fungamano hilo na Muumba wao. Allah SW anawadhihaki kwa furaha yao ya kiuwongo kwa kusema:

وَفَرِحُوا بِالْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَمَا الْحَيَاةُ الدُّنْيَا فِي الآخِرَةِ إِلاَّ مَتَاعٌ (الرعد: 26
“Na wanafurahia maisha ya dunia. Na hayakuwa maisha ya dunia kwa kulinganisha na akhera ila ni starehe (ndogo).” (Ar-Raad :26)

Furaha ya nne kwa Muislamu ni kupata ushindi na nusra kutoka kwa Mola wake. Kwa kauli ya Alah Taala :

وَيَوْمَئِذٍ يَفْرَحُ الْمُؤْمِنُونَ (الروم: 4
“Na siku hiyo watafurahi Waumini” (Ar-Rum : 4)

Na bila ya shaka ushindi mkubwa zaidi kwa Waislamu katika ulimwengu huu ni ule utaowapelekea wao kuwa chini ya kivuli cha utawala wao wa Kiislamu (Khilafah). Kwa kuwa ushindi huo ndio dhamana ya furaha nyengine za Muislamu, na ndio mwamvuli wa yote yaliyo muhimu na ya wajibu kwa Muislamu, kuanzia ibada zake, usalama wake, amani yake, utulivu wake, heshima yake nk.

Furaha ya tano kwa Muislamu ni kukutana na Mola wake, yaani kuyakuta malipo makubwa, mema pamoja na radhi za Mola wake Siku ya hesabu kwa kuingizwa katika Jannah. Na hilo ni katika kilele cha furaha kwa Muislamu kuliko chochote kwa kuwa aliishi katika maisha haya mafupi ya dunia kwa kujipinda na kusimama juu ya mipaka ya ‘halali’ na ‘haramu’ kwa kuitarajia furaha hiyo ya milele.
Allah SW anasema:

فَوَقَاهُمْ اللَّهُ شَرَّ ذَلِكَ الْيَوْمِ وَلَقَّاهُمْ نَضْرَةً وَسُرُورًا (الإنسان: 11
“Basi Mwenyezi Mungu Atawalinda na shari ya siku hiyo, na atawakutanisha na raha na furaha” (Al-Insan: 11)

Tunaporudi kuziangalia furaha mbili za mfungaji tutaona Waislamu hawazifikii furaha hizo ipasavyo. Kwa upande furaha ya wakati wa kufutari, hapana shaka Muislamu hujihisi furaha kwa kuwa kakamilisha swaumu yake hadi magharibi kwa kuitikia amri ya Mola wake. Hata hivyo, Muislamu katika kumaliza swaumu yake jioni huhitaji chakula na utulivu, vitu ambavyo Muislamu hanavyo. Umaskini wa Waislamu leo kwa kiasi kikubwa si wa kimaumbile, bali ni unyonge na umasikini wa kutengezwa, kwa kuwa ulimwengu wa Kiislamu umesheheni kila aina ya rasilmali kuweza kuwafanya Waislamu waishi katika hali ya neema na kukidhi mahitajio yao.

Kwa hivyo, furaha ya Muislamu wakati wa futari haikamiliki, hata kama kuna baadhi ya Waislamu kibinafsi watakula vizuri wakati wa futari, bado sehemu ya ndugu zao Waislamu ambao ni Ummah wao wanahangaika usiku na mchana wakisibiwa na unyonge, idhilali, mateso, kuuliwa, kuporwa ardhi zao, bila ya kusahau ukandamizaji wa uchumi wa kibepari kiasi cha baadhi kushindwa hata kudiriki kifungua kinywa baada ya funga ya kutwa. Yote hayo hukwamisha Muislamu kuifikia furaha hiyo vilivyo. Na ili furaha hii ikamilike huhitajika furaha (nambari nne) ya ushindi na kurejesha dola ya Kiislamu ya Khilafah ipatikane, kwa sababu hata kama kwa wakati huo kutakua na maskini na fakiri ambae hajimudu, bado unakuwa ni wajibu wa dola kumtoshelezea mahitajio yake.

Amma furaha ya Muislamu kukutana Mola wake, yaani kuyakuta malipo makubwa ya pepo ya ‘Rayaan’ kwa Swaumu yake, japo hilo linabakia kuwa siri ya Muumba, lakini ukweli unabakia pale pale kwa kuwa Muislamu hatekelezi swaumu yake chini ya kivuli cha utawala wa Kiislamu ambao hudhamini mazingira mwanana wa kila ibada, lazima Swaumu hiyo itakuwa na changamoto nyingi kutokana na kuzingirwa na mazingira yasiokuwa ya Kiislamu ambayo kimaumbile sio rafiki kwa ibada hiyo na nyenginezo. Hivyo, ni wazi jambo hilo humkosesha Muislamu utulivu wa nafsi juu ya kuipata furaha yake ya pili.

Tunamuomba Allah SW katika mwezi huu wa Ramadhani Aupe tawfiq ya kuzinduka zaidi Ummah wetu utambue uwajibu wa kufanya kazi ya ulinganizi ili kurejesha tena utawala wa Khilafah Rashidah ambayo ndio mdhamini wa kweli wa furaha za Waislamu

Amiin

Masoud Msellem
10 Ramadhan 1440 Hijri / 15 Mei 2019
#RamadhanNaMuongozoWaQuran

Maoni hayajaruhusiwa.