Siku Ya Vijana Na Ndoto Za Mchana
بسم الله الرحمن الرحيم
Wakati tarehe 12 Agosti ya kila mwaka imechaguliwa kuwa Siku ya Vijana Kimataifa, hali ya vijana kiulimwengu ni mbaya sana na wengi wao wamekosa matumaini ya kuishi kamwe! Mfumo kandamizi wa kibepari unaowasimamia wanadamu kwa sasa umewatelekeza vijana kiasi cha kufikia wengine kuchukua maamuzi magumu ambayo hayafai kama kujiua, kutumia madawa ya kulevya nk.
Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na Masuala ya Ajira (ILO) ni asilimia 25% tu ya waajiriwa duniani ndio vijana. Hii inamaanisha wengi wa waajiriwa ni watu waliovuka umri wa ujana, ilhali zaidi ya asilimia 43% ya vijana duniani hawana ajira. Katika nchi zinazoendelea ambazo ni makoloni ya mataifa kibepari ya kimagharibi asilimia 31% ya vijana wake hawana elimu ya kujitosheleza kuweza kuajiriwa.
Kutokana na vijana wengi kutokuwa na ajira wamekuwa wanajishughulisha na vitendo vya ajabu kama kucheza kamari kama njia ya kujipatia kipato. Gazeti la “Mtanzania” (Agosti 3 2016) lilitoa makala ya uchambuzi inayoonesha namna gani vijana wengi wanavyojiingiza katika uchezaji kamari. Na serikali za kibepari hazijali kwa kuwa zinapata mapato mengi kupitia kuyatoza kodi makampuni hayo ya kamari.
Aidha, vijana wamekuwa ndio madaraja mwanana ya kudandiwa na wanasiasa wa kidemokrasia kufikia malengo yao. Baada ya hapo wanatemwa na kutupiliwa mbali. Mfano mzuri ni namna vijana wanaojishughulisha na shughuli za kuendesha bodaboda walivyoahidiwa kwa hadaa nyingi katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 nchini, na kisha bada ya uchaguzi hali yao imezidi kuwa mbaya. Kwa ufupi, vijana katika jamii chini ya ubepari wamekuwa wakiambulia masuluhisho hewa kwa matatizo yanayowakabili ambayo hayawafikishi popote.
Uislamu awali unawandaa vijana kubeba fikra thabiti za mfumo wa Kiislamu. Pia huwandaa kuweza kuchukua majukumu ya kuwa walezi wa familia. Kwa mujibu wa nidhamu ya kijamii ya Kiislamu suala la familia ni jambo muhimu sana kwa ustawi wa jamii. Hivyo, huhimiza vijana kuowa haraka na mapema ili kuvunja mianya yote ya kutokea kwa zinaa. Kwa kuzuia zinaa isitokee basi huhamasisha mazingira rahisi na mepesi ya ndoa. Ndio maana hata tukaona katika historia ya Khalifah Umar ibn Abdulaziz aliweza kutoa fungu kwenye hazina ya dola “baytul maal” kuwawezesha vijana wanaotaka kuoa lau hawana mahari.
Aidha, Uislamu unadhamini kila kijana kupata uhakika wa mahitaji yake yote na hauwabagui watu kwa misingi yoyote. Chini ya Uislamu vijana hupewa hadhi maalum na ndio maana ndani ya tarekhe yetu ya Kiislamu kumesheheni mifano ya vijana waliopewa dhamana na kushika nyadhifa mbalimbali za kiutawala na kiutendaji. Kwa mfano, Sahaba Usama bin Zaid ra aliteuliwa na Mtume SAAW kuwa Kamanda wa kikosi katika jihadi huku umri wake ukiwa chini ya miaka 20 na kuwaongoza masahaba wakubwa kiumri kuliko yeye. Aidha, Khalifah Muhammad Al-Fatih alishika ukhalifah akiwa na umri wa miaka 21 tu.
Pia tukimuangalia Kiongozi wetu Mtume SAAW aliitumia vyema rasilmali watu ya vijana kwa awali kuwabadilisha fikra na uoni wao. Kwa kuwa fikra ndio ukombozi msingi kwa kila mwanadamu. Hivyo SAAW aliwalingania Uislamu vijana wadogo ambao wengi wao awali walikuwa ni wahuni, wasio na ajira uhakika na waliokosa muelekeo. Aliwafanya wasilimu na kubeba ujumbe wa haki ambao ulikuja kuleta mabadiliko ya kimfumo katika ulimwengu. Na kwa kuwa vijana ndio waliokuwa wanadhulumiwa kwa kiwango kikubwa katika mujtamaa wa Makka wa wakati huo basi walijikuta wanasilimu kwa wingi: Kwa mfano waliweza kusilimu mas-haba kama Ali bin Abi Talib umri wake ni miaka 8, Zubeir bin Al-Awwam umri wake ulikuwa ni miaka 8, Twalha bin Ubeid Allah miaka 11, Al-Arqam bin Abi Al-Arqam miaka 12, Abdalla bin Masoud miaka 14, Said bin Zeid chini ya miaka 20, Saad bin Abi Waqqas alikuwa na miaka 17, Masoud bin Rabiah alikuwa na miaka 10, Jaafar bin Abi Twalib alikuwa chini ya miaka 18, Zeid bin Harith akiwa na miaka 20, Athman bin Affan takriban miaka 20, Tuleib bin Umeir takriban miaka 20,Khabbab bin Al-Arat takriban miaka 20, Amir bin Fuheirah akiwa ni mtoto wa miaka 20, Musa’ab bin Umeir akiwa na miaka 23, Musaab bin Umeir akiwa na miaka 24, Miqdad bin Al-Aswad akiwa na miaka 24,Abdallah bin Jahash akiwa na miaka 25, Umar bin Al- khatab akiwa na miaka 26, Abu Ubeida bin al-jarrah akiwa na miaka 27, Utbah bin Ghazwan akiwa na miaka 27, Abu Hudhaifa bin Utbah akiwa takriban miaka 30, Bilal bin Rabah takriban miaka 30, Ayyash bin Rabiah takriban miaka 30, Amir bin Rabiah takriban miaka 30, Naim bin Abdallah katika miaka ya 30, Athman takriban miaka 30, Abdallah takriban miaka 17, Qudama takriban miaka 19, As-saib mtoto wa Madhuun bin Habib miaka 20, Abu salama Abdallah bin Abdul Asad al Makhzumiy katika miaka ya 30, Abdurrahman bin Auf takriban miaka 30, Ammar binYassir takriban miaka 30 nk.
Pia tunaona Mtume Muhammad (SAAW) aliweza kuleta mabadiliko ya kimsingi katia maisha ya vijana kwa kuwakomboa kifikra na kimatendo. Kwa mfano, sahaba mkubwa Abu Dharr bin Ghiffar alikuwa anatokamana na kabila la majambazi, alisilimu na kuwa mbeba ujumbe wa haki kila mahala kiasi cha kulifanya kabila lake lote kusilimu na kuweza kuacha tabia yao ya ujambazi ambayo ndiyo iliyokuwa nguzo ya uchumi wao.
Tofauti na hali ilivyo ndani ya mfumo wa kibepari unaotawala dunia leo, kutokana na kuwafanya vijana kukosa muelekeo, wengi wao hujiunga katika vikundi vya kihuni na kihalifu kama vile “mbwa mwitu”, “panya road” nk. Ndani ya Marekani ambayo ndio kinara wa mfumo wa kibepari kuna makundi mengi ya vijana wahuni na kihalifu ambayo humiliki silaha na kuwadhuru raia. Makundi hayo yamekuwa yanahusishwa na vurugu za mara kwa mara. Takwimu za kitaifa nchini humo zinaonesha kuwa: kuna makundi zaidi ya 24,500 ya wahuni na ya kihalifu ambayo humiliki silaha, yakiwa na wanachama zaidi ya 772, 500 wengi wao ni vijana.
Enyi vijana!
Hakika mnajionea ni namna gani mfumo wa kibepari ulivyowadhulumu na kuwafanya ngazi kwa malengo yao. Kwa hakika mfumo huu umefeli si tu kuwasimamia na kuwapa hadhi stahiki vijana bali kuwasimamia wanadamu wote. Mfumo mbadala wenye uadilifu katika kuwasimamia wanadamu ni Uislamu peke. Basi tunawainganieni kuja kwenye Uislamu na kufanya kazi ili umtawale mwanadamu katika kila kipengee cha maisha yake. Huu ndio mfumo pekee ambao unaendana na maumbile ya wanadamu na ambao unaweza kutatua ipasavyo matatizo ya vijana na wanadamu jumla.
Maoni hayajaruhusiwa.