Pasaka Ndani Ya Ramadhani Waislamu Na Wakiristo Zingatieni Haya:
بسم الله الرحمن الرحيم
Ijumaa Kuu na Pasaka imo ndani ya Ramadhani, ni vyema Waislamu kukosoa upotofu wa Pasaka kwa kufungamanisha na Ramadhani katika khutba au mazungumzo yetu. Muongozo huu unaweza kusaidia.
Siku ya Ijumaa Kuu kama leo Ukristo huitakidi kuwa Nabii Issa As. alisulubiwa, na Jumatatu akafufuka. Hivyo, sikukuu hii ya kikiristo ya Pasaka ni kwa munasaba wa kuyakumbuka na kuyaadhimisha matukio mawili hayo. Pia tukumbuke kuwa Itikadi ya Ukiristo ya Issa As. kufa msalabani, hukusudiwa na ukiristo kuwa kifo chake kimefidia dhambi zao, kwa kuwa ukiristo unaitakidi kwamba mwanadamu ana dhambi ya asili tangu Adam as.
1. Quran Tukufu kitabu kilichoteremshwa katika mwezi huu Ramadhani ambacho ni muongozo kwa watu (Huda linasi) katika jambo hili kimeweka muongozo wazi na bayana kwamba Issa as. hakusulubiwa wala hakufa. Lazima muongozo huo uwekwe bayana na wazi. 4.157
2. Ikiwa Uislamu umesema Imani hiyo ya Ukiristo ya kusulubiwa na kufa Issa as. ni uongo, ina maana pia vyanzo unavyotumia Ukiristo kupata taarifa hizo navyo sio vya kweli. Na hii maana yake Biblia sio kitabu cha Mungu.
3. Quran ni muongozo na Injiil pia ilitumwa kuwa muongozo (5:47). Vitabu vyote hivi viwili kutoka kwa Muumba vilitumwa kwa Mitume wake As. maana yake ni kuwa miongozo hii miwili ni ndugu, na kamwe haiwezikani kutofautiana wala kugongana katika mambo ya kiimani. Hivyo, ni wajibu kuitakasa Injiili kutokana na uongo inayonasibishwa nao kwa kutumia Quran. Kwamba kitabu hicho mbali na uongo wa Ukiristo. Lakini kimsingi, Waislamu tunaamini n ani lazima tuamine hivyo kwamba kiliwahi kuwepo kitabu kinachoitwa Injiil ambacho alipewa Issa As. kuwa muongozo, lakini leo kitabu hicho hakipo, bali kilichopo ni vitabu vilivyoandikwa na watu baada ya kuondoka Issa As.
4. Kuwataka manaswara waje katika Uislamu kwa kuwa Quran ndio kitabu pekee chenye taarifa sahihi za Mitume wote As. waliotangulia na kina kila sifa kuwa ni kitabu cha Mungu tofauti na vitabu vyengine. 3: 64, 4:171
5. Ikiwa wakiristo hawajawa tayari kuwa Waislamu, basi walau wafanye utafiti kwa ikhlasi juu ya Uislamu na wafahamu haya:
6. Japo Uislamu unaitakidi kwamba Ukiristo ni dini isiyo ya haki lakini haulazimishi wakiristo kuwa Waislamu. Wala haikatazi Muislamu kuamiliana kwa wema na insafu na wakirsto katika mambo mengine yasiokuwa ya kidini kama biashara nk. Aidha, Uislamu unawapa heshima wakiristo juu ya dini yao kama Khalifah Umar ra. ndani ya mwezi wa Ramadhani kama huu mwaka 15 Hijria alipokataa rai ya Sophronius, Askofu na kiongozi mkuu kuswali katika kanisa ndani ya Jerusalem baada ya Waislamu kuufungua mji huo, akisema Umar ra. lau ataswali hapo, basi Waislamu watakuja kuufanya msikiti na kuwanyima wakiristo kanisa lao.
7. Pia Umar ra. sambamba na ufunguzi huu wa Jerusalem aliandika waraka wa kihistoria kudhamini usalama wa wakiristo, mali zao, misalaba yao na makanisa yao katika eneo hilo.
8. Hivyo, wakiristo leo wasiingie katika mtego wa madola ya kimagharibi ambao huchochea ugomvi wa kidini baina yetu kwa maslahi ya mfumo wao wa kibepari. Tukumbuke Waislamu na wakiristo wameishi pamoja salama usalimini kwa makarne. Na mifano mingi mpaka leo katika biladi za Waislamu kama Misri, Syria, Lebanon nk. bado kumebakia makanisa na jamii za wakiristo, licha ya kuwa maeneo hayo yalikuwa chini ya Khilafah kwa makarne.
Masoud Msellem
Maoni hayajaruhusiwa.