Pasaka : Jukwaa la Kuibua Mjadala wa Kistaarabu kwa Ukristo
بسم الله الرحمن الرحيم
وَقَوْلِهِمْ إِنَّا قَتَلْنَا الْمَسِيحَ عِيسَى ابْنَ مَرْيَمَ رَسُولَ اللَّهِ وَمَا قَتَلُوهُ وَمَا صَلَبُوهُ وَلَكِنْ شُبِّهَ لَهُمْ
“Na kauli yao ya kusema kwao: Sisi tumemuuwa Masihi Issa , mwana wa Maryam, Mtume wa Mungu” hawakumuuwa wala hawakumsulubu bali walibabaishiwa mtu mwengine….”
(TMQ 4: 157)
Sikukuu ya kinaswara/kikiristo ya Pasaka itakayoanza kuadhimishwa tarehe 19 Aprili kwa mwaka huu ipo mlangoni, ambapo katika Ijumaa kuu wakristo huitakidi kuwa Nabii Issa As. alisulubiwa, na Jumatatu akafufuka. Hivyo, sikukuu hiyo ni kwa munasaba wa kuyakumbuka na kuyaadhimisha matukio hayo.
Suala la kuanguka kifikra limepelekea baadhi ya Waislamu kushindwa kutofautisha baina ya fikra ya ‘Madania na Hadhara’ ambayo hufafanua wazi ni mambo gani Waislamu huruhusiwa kuchukua kutoka kwa makafiri na mambo gani haturuhusiwi kuchukua. Hali hiyo imewafanya baadhi ya Waislamu nao kujitumbukiza katika maadhimisho ya siku kuu zisizokuwa za Kiislamu, zikiwemo za kinaswara kama hii inayotukabili ya Pasaka.
Kwa mfano, Tanzania Bara na Visiwani kwa miaka mingi kumekuwa na ziara za kimichezo kwa munasaba wa Pasaka. Ziara ambazo kihukmu kwa Muislamu ni haramu kushiriki au kuchangia. Kwa kuwa ni maadhimisho ya kumbukumbu ya kinaswara inayonasibishwa na kusulubiwa kwa Issa As., kufa na kufufuka.
Ajabu inayodhihirika hapa ni badala ya Waislamu kuitumia fursa ya Pasaka kufedhehi waziwazi na kuugonga udhaifu wa dini ya kikristo katika misingi yake na kuwalingania wakristo kuja ndani ya Uislamu kwa hoja na dalili za kiakili, baadhi ya Waislamu kimakosa au makusudi hujumuika na manasara katika maadhimisho hayo haramu.
Uislamu kwa kuwa ni dini ya haki mapema sana ilianzisha mapambano makali ya kifikra baina ya haki na batil. Na kwa upande wa dhidi ya unaswara unagonga kwa nguvu na makemeo makali misingi yote inayosimamia dini hiyo. Kwa kuonesha waziwazi kwamba ni misingi dhaifu, uwongo na batil. Kamwe Uislamu haukupaka mafuta katika suala hilo, ili manasara wauone waziwazi udhaifu huo waache dini hiyo batil na waingie katika dini ya haki ya Kiislamu.
Wajibu huu wa kuigonga haki juu ya batil ndio msimamo ambao Waislamu daima tuna wajibu kushikamana nao. Amma ikiwa dhidi ya vidini vya kiroho kama ukiristo, uyahudi, uhindu ubudha nk. au dhidi ya mifumo batil isiyo na haja ya dini kama ukomunisti ulioanguka kimataifa au demokrasia/ubepari unaoendelea kumtia mashaka mwanaadamu kila uchao.
Quran inatamka wazi kwa kinywa kipana na bila ya lugha ya mzunguuko wala kupaka mafuta juu ya uwongo na upotofu wa fikra zote msingi zilizojengewa dini ya kikiristo. Kuanzia fikra tata ya utatu, uwongo wao kuhusu uzawa wa Issa As, fikra zao potofu juu ya mwanamke mwema bi Maryam As. pia ikagonga kwa ukali upotofu wa madai yao ya kusulubiwa kwa Issa As. ati kasulubiwa kufidia dhambi zao. Aidha, Quran ikatangaza bayana kwamba msimamo wao huo wa kusulubiwa Issa As.ni uwongo shahir dhahir.
Uislamu unayafanya mapambano yote haya ya kifikra kwa kujitosheleza kwa hoja waziwazi na kunadi hadharani kwamba manasara wamekwenda kombo na dini yao ni ukafiri usio na shaka.
Kwa hivyo, ikiwa misingi ya dini na imani ya kikristo yote imejengwa juu ya msingi mbovu wa uwongo na batil ina maana pia kwamba vyanzo inavyovitegemea dini hiyo kuvua na kupata mafunzo yake pia ni batil na si vya kutegemea. Katika hali kama hiyo wakristo watakuwa na chaguo moja katika mawili. Amma waache dini hiyo mara moja waingie dini nyengine ya haki. Au watafute vyanzo vya kuaminika kuhusiana na imani waliyonayo. Lolote watakaloshika katika mawili hayo watalazimika waingie katika Uislamu.
Tunapoangalia tareekh ya Kiislamu kwa makini tutaona ya ndani mwaka wa nne wa Utume baadhi ya viongozi wa kiutawala na wakinaswara ndani ya Ethiopia/Uhabeshi walikinai kwamba Quran ni chanzo cha kutegemea, wakati iliposomwa mbele yao na sahaba Jaafar bin Abu Talib Ra. ndani ya kasri yao kufafanua baadhi ya fikra ambazo manaswara wamezipotosha.
Watawala hao na viongozi wa kinaswara walifanya unyenyekevu mkubwa kiasi cha kutiririkwa na machozi na baadhi yao kusilimu. Pia msafara wa wakiristo wa Najran uliokuja kwa Mtume SAAW ndani ya mwaka wa tisa ulikataa kusimama kufanya kiapo cha laana na maapizano (mubahala) baina yao na Mtume SAAW. Hizi zote ni dalili za manaswara kukinai vyanzo vya kweli vya Uislamu.
Changamoto ya Waislamu leo hususan kwa minasaba ya siku kama hizi za maadhimisho ya kinaswara ni kuwakabili wakristo hususan ‘wakiristo makini’ kuwaonesha udhaifu katika misingi ya imani yao na udhaifu wa vyanzo vya mafunzo ya imani hiyo ambavyo kamwe haviwezi kuinusuru imani hiyo. Kwa kuwa kitabu chao hakitokani na Muumba. Na ukweli kuwa kitabu chao si cha Mungu hata wao wanaukiri. Kwa kuwa kitabu cha Mungu, lazima kibakie katika lugha yake ya asili kilivyoteremshwa, kisiwe na mabadiliko kwa kuingizwa mikono ya binaadamu na asiweze mwanaadamu kutoa mithili yake kwa lugha wala maudhui.
Sifa hizo kamwe haziwezi kupatikana katika kitabu chochote duniani isipokuwa Quran. Katika hali hiyo wakristo wangepaswa kutegemea kupata taarifa sahihi za kidini na mengineyo kwa ukweli, uaminifu na ukamilifu kutoka ndani ya Quran. Wakristo wakilikubali hilo ambalo halina budi kila mkristo makini kulikubali, maana yake pia hawatokuwa na sababu ya kukikataaa kila kilichomo ndani ya kitabu hicho. Kwa kuwa wameshakinai kwamba ni kitabu cha haki. Basi wakati huo hawatokua wakristo tena, bali watakuwa Waislamu. Kwa kuwa wamekinai ukweli wa kitabu cha Quran.
قُلْ يَا أَهْلَ الْكِتَابِ تَعَالَوْا إِلَى كَلِمَةٍ سَوَاءٍ بَيْنَنَا وَبَيْنَكُمْ أَلاَّ نَعْبُدَ إِلاَّ اللَّهَ وَلاَ نُشْرِكَ بِهِ شَيْئًا وَلاَ يَتَّخِذَ بَعْضُنَا بَعْضًا أَرْبَابًا مِنْ دُونِ اللَّهِ فَإِنْ تَوَلَّوْا فَقُولُوا اشْهَدُوا بِأَنَّا مُسْلِمُونَ
(آل عمران: 64).
“Sema: Enyi watu mliopewa kitabu (mayahudi na maswara)! Njooni katika neno lililo sawa baina yetu na baina yenu: ya kwamba tusimwabudu yoyote ila Mwenyezi Mungu, wala tusimshirikishe na chochote, wala baadhi yetu tusiwafanye wengine kuwa waungu badala ya Mwenyezi Mungu. Wakikengeuka , semeni shuhudieni ya kwamba sisi ni Waislamu” (TMQ 3:64)
Masoud Msellem
29 Machi 2024
Maoni hayajaruhusiwa.