Nasaha kwa Wanafunzi wa Kidato cha Nne.

Awali ya yote hatuna budi kumshukuru Allah Taala ambae ndie Muumba wa Kila kitu kwa kutuneemesha neema mbali mbali kubwa na ndogo ambazo leo hii tunazitumia kwa aina ya matumizi ya kimaisha ili kuendeleza uhai aliotupatia.
Miongoni mwa neema kubwa ya Allah Taala kwetu sisi viumbe Ni neema ya Elimu kwani ndio kitu pekee kilichokuja kuleta usahali kwa mwanadam Ni kwa namna gani atakabili maisha ya duniani kwa namna ilio njema ili kuweza kufanikisha malengo alioletewa hapa ulimwenguni.

Njia pekee ambayo mwanadam amaweza kuitumia ili kupata
Elimu Ni kusoma tu ima katika mifumo rasmi au isio rasmi au uzoefu kupitia matendo na shughuli mbali mbali anazozifanya Kama mwanadamu.
Hivyo tunaona suala zima la kuwa na Elimu Ni muhimu kwa mwanadamu yoyote Yule ili aweze kuishi vizuri kulingana na maisha ya ulimwenguni leo yalivyo.

Kwa munasaba wa mitihani ya kidato Cha Nne itakayofanyika kote nchini kuanzia 05/11/2018 sisi Hizb ut-Tahrir Tanzania tunapenda kuwanasihi wanafunzi Mambo yafuatayo -:

1. Kufanya maandalizi ya kutosha ya kupitia na kusoma masomo yao vizuri kwa huu muda mchache uliobaki kufika siku za mitihani na kuachana na kasumba za mitaani kuwa Ngombe hanenepi mnadani msemo ambao huvunja moyo jitihada za mwisho kwa wanafunzi haswa waliokua hawajafanya mwanzo maandalizi ya kutosha.

2. Kufika mapema kwenye vituo vya kufanyia mitihani ili kupata muda wa kutosha wa kujiandaa na kujua kwa usahihi eneo analo fanyia mtihani.

3. Kuchukua vifaa vyote vinavyohitajika katika kufanyia mitihani Kama vile peni na vyenginevyo ili kuepusha usumbufu kwa wanafunzi wengine ndani ya chumba Cha mitihani kwa kuazima azima vitu ambavyo vilikua kihakika viko ndani ya uwezo wake kuchukua mapema siku ile ya mitihani Kama vile penseli na raba.

4. Kujiepusha na udanganyifu wa aina yoyote ile ili kuepusha kufutiwa mitihani yao na kuharibu kabisa jitihada zao za takribani miaka zaidi ya kumi ya uanafunzi na kusoma kwa tabu kabisa, jitihada za wazazi za kumsomesha kwa gharama kubwa lakini mwisho kuishia mikono mitupu. Na ikumbukwe kuwa hili pia Ni kosa kubwa mbele ya Allah Taala Kama vile alivyosema Mtume (s.a.w) :
” Mwenye kughushi si katika sisi”.

5. Adabu na heshima kwa wasimamizi wa mitihani na wote waliomzunguka katika eneo la kufanyia mitihani yao ili kujiepusha na matatizo yasio na ulazima.
Mwisho tunawatakia wanafunzi wote wa kidato Cha Nne mafanikio mema katika mitihani yao na maisha yao kwa ujumla na watumie vizuri fursa hii ili waweze kujiendeleza ziadi kielimu na kupata ustawi ulio Bora kwa mafanikio yao na umma mzima kwa ujumla lakini wasisahau kumtegemea Allah (s.w) na kumuomba kwa muongozo na kupata utulivu wa nafsi wakati wa mitihani na kujikurubisha kwake khaswa kipindi hiki ambacho wamekabiliwa na changamoto hio bali kuishi nae Allah (s.w) katika maisha yao yote.

Allah akufanyieni wepesi mujibu vizuri mitihani yenu na mufaulu vizuri.
Amiin

Maoni hayajaruhusiwa.