Miongoni Mwa Fikra Hatari za Kuangamiza Uislamu- 1

بسم الله الرحمن الرحيم

Ukuruba Wa Kiimani Baina ya Dini Tofauti (Dini Mseto)

Ni wajibu kwa Waislamu kuwalingania makafiri kuhusu Uislamu na huu ni ulinganizi wa kuwakinaisha makafiri kuhusu Uislamu na waache ukafiri.
Wamekuwa wakifanya hivi Waislamu katika karne zote mpaka hivi sasa, anasema Allah Taala:
ادْعُ إِلَى سَبِيلِ رَبِّكَ بِالْحِكْمَةِ وَالْمَوْعِظَةِ الْحَسَنَةِ وَجَادِلْهُمْ بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ (النحل: 125).
“Waite (watu) kwenye njia ya Mola kwa hikma na mawaidha mema na ujadiliane nao kwa namna iliyo bora” (Nahl: 125)
Na Mtume(SAW) akamlingania Heraclius Mfalme wa Kirumi:
“Hakika nakulingania kwa ulinganizi wa Kiislamu, silimu nawe utasalimika”
Hiki kinachoendelea leo yaani mazungumzo baina ya dini tofauti (dini mseto) ni jambo lipo mbali na ulinganizi wa Kiislamu. Fikra hii ni fikra ngeni, ovu, na ni fikra ya kimagharibi isiyokuwa na msingi wowote katika Uislamu kwani inazalisha dini mpya ambayo makafiri wanawataka Waislamu waitumikie tofauti na Uislamu.
Fikra hii ovu kimataifa ilianza kukua mwaka 1932 katika Ufaransa ambapo kongamano la mwanzo lilifanyika mwaka 1933 mjini Paris. Katika miaka ya 1960 na 1970 yalifanyika zaidi ya makongamano 13 kuhusu dini mseto,makubwa kati yao ikiwa ni kongamano la mwaka 1979 lililofanyika Tunisia.
Katika miaka ya 1990 fikra hii ilichangamka zaidi likafanyika kongamano la Jordan mwaka 1993, kisha Sudan mwaka 1994, Sweden mwa 1995. Kutokamana na makongamano haya ilipendekezwa kubuni maana mpya ya maneno kama ushirikina, kutoamini, wastani, n.k ili kuhakikisha maneno haya hayatakuwa chanzo cha mgawanyiko baina ya watu wa dini tofauti.
Wakatambulisha istilahi zinazolingana kwa pamoja katika dini kuu tatu na katika aqida na akhlaqi. Pia wakaja na mtizamo pamoja na kuunda ufahamu wa kipamoja (wenye kulingana kimaana) katika istilahi za ‘usawa’, ‘amani’, ‘haki za wanawake’, ‘haki za binadamu’, ‘demokrasia’, ‘uhuru’, ‘kuishi pamoja kwa amani’ nk. Ilhali istilahi hizo kiudhati haziwezi kuwa na mitizamo sawa kwa kuwa kila dini imejengwa juu ya misingi yenye tafsiri yake.
Fikra ya ‘dini mseto’ ni miongoni mwa silaha zkali zenye sumu za kifikra kuletwa kwa Umma wa Kiislamu ambapo malengo yao makuu ni kuzuiya kurudi kwa Uislamu kisiasa. Hii ni kwa sababu Uislamu unatishia uhai wa ustaarbu wa kimagharibi na mfumo wao wa Ubepari kwani utaangamiza maslahi yao na athari yao.
Wamelenga pia Mabepari makafiri wakoloni katika fikra yao hii ya ‘dini mseto’ kubadilisha hadhara/ mtazamo ya Uislamu kuwa ni hadhara ya Kibepari hususan katika biladi za Kiislamu ili waondoe kutoka kwa Waislamu thaqafa ya Kiislamu na kuivua sifa zake ambazo zinatofautisha na dini zingine hasa upande wa kisiasa ambapo ni kuendesha maisha kwa mujibu wa hukmu za Kiislamu na kubeba ulinganizi wa Kiislamu dunia nzima.
Makafiri kupitia mazungumzo ya mjumuiko wa ‘dini mseto’ na majukwaa yake wanataka kugeuza haiba na utambulisho (shakhsiya) ya Muislamu kuwa mpya ambapo hatoona aibu kuwacha halali na kufanya haramu.
Aidha, wamelenga makafiri kwa fikra ya ‘dini mseto’ kuharibu raghba ya Muislamu kiasi cha kumfanya afikie kutochukia ukafiri na awe haamrishi tena mema na wala hakatazi maovu.
Kwahiyo, makafiri wakisaidiwa na watawala vibaraka, maulamaa wao waovu na mufakirina/ wanafikra wao katika biladi za Kiislamu wamelenga kubuni aina mpya ya Uislamu utakaoendana na ukafiri wao uliojengwa juu ya aqida ya kutenganisha dini na maisha ambapo mwanadamu hupewa haki ya kutunga sheria badala ya Allah Al Aziz Al Hakim.
Makafiri wameeneza fikra yao hii ovu ulimwengu mzima leo hii na wameibeba masheikh na wanachuoni waovu katika biladi zetu amma kwa ujinga au kwa kuuza akhera yao kwa pato duni la kidunia.
Makafiri kwa kushirikiana na tawala vibaraka na wanavyuoni waovu wametengeneza na kudhamini mabaraza ya ‘dini mseto’ na ‘maridhiano’ ya ‘kueneza amani’ yakihusisha dini tofauti katika biladi zetu.
Ni jukumu letu Waislamu kufahamu mbinu hizi chafu za makafiri zinazobebwa na na masheikh waovu katika biladi zetu, kuzifedhehi hadharani mbinu hizo, kuutahadharisha Ummah na kuwasihi wajitenge mbali na fitna hiyo ambayo ambayo imapelekea kutoka katika Uislamu yaani kuwa ‘murtad’. Na Allah SWT atuepushe na hilo – Amiin
Said Bitomwa
Risala ya Wiki No. 90
02 Rabi’ al-awwal 1442 Hijri/ 19 Oktoba 2020 Miladi

Maoni hayajaruhusiwa.