Miezi Mitukufu Itusukume Zaidi Kwa Ulinganizi
بسم الله الرحمن الرحيم
Maisha yetu Waislamu kwa kila jambo yapasa yawe kwa kutaka radhi za Allah SWT, nako ndiko kufaulu. Hakuna kufaulu duniani na hasa akhera bila kuridhiwa na Allah SWT. Kufaulu ni kuepushwa na adhabu zake na kukirimiwa pepo yake SWT, yaani watakaoingizwa peponi watakuwa wamepata faida, na watakaongia motoni watakuwa wamepata hasara. Anasema Allah SWT kuhusu wasiopata hasara.
إِلاَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ فَلَهُمْ أَجْرٌ غَيْرُ مَمْنُونٍ (التين: 6
“Lakini wale walio amini na wakatenda mema, hao watapata ujira usio kwisha”. (At-Tin:6)
Allah SWT ni Mwenye Rehma kwetu, kamwe hakutuacha bila ya kutuonesha yapi tufanye ili aturidhie na akaweka mazingira ya kuyatenda hayo. Miongoni mwa mazingira mwanana ya kuweza kupata radhi na ujira mkubwa ni Kutenda amali katika miezi mitukufu ambayo matendo ndani yake hupata fadhila, darja na ujira mkubwa. Miongoni mwa miezi hiyo huu mwezi tulionao wa Dhul-Hijja ambao hupatikana kila mwaka
Allah Taala Anasema:
إِنَّ عِدَّةَ الشُّهُورِ عِنْدَ اللَّهِ اثْنَا عَشَرَ شَهْرًا فِي كِتَابِ اللَّهِ يَوْمَ خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضَ مِنْهَا أَرْبَعَةٌ حُرُمٌ
‘Hakika idadi ya miezi mbele ya Allah ni kumi na mbili katika kitabu cha Mwenyezi Mungu tangu siku alipoumba mbingu na ardhi. Ndani ya miezi hiyo kuna miezi minne mitukufu…” (Tawba: 36)
Miongoni mwa matendo mema tunayopaswa kuyafanya ni kuusiana haki na subra. Anasema Allah SWT katika kuonesha ambao matendo yao yatawafaidisha na kuwatoa katika kundi la wenye hasara;
إِلاَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ وَتَوَاصَوْا بِالْحَقِّ وَتَوَاصَوْا بِالصَّبْرِ (العصر: 3
“Ila wale walio amini, na wakatenda mema, na wakausiana kwa haki, na wakausiana kusubiri” (Al-Asr: 3).
Yaani wanaolingania haki (Uislamu) na kulingania/kuusia subra kuvumilia mitihani mbali mbali ya misiba na majanga ikiwemo mitihani katika ulinganiaji haki na kumtegemea Allah swt katika kutafuta nusra/ ushindi.
Hitajio la ulinganizi ni kubwa leo hii kutokana na kiwango kikubwa cha kupuuzwa na kupotea haki kwa Waislamu na wasiokuwa Waislamu. Leo ni zile zama ambazo alizisema Mtume SAAW, kwamba kushikamana na Uislamu ni kana kwamba umeshika kaa la moto.
Fikra za wengi katika Waislamu ni fikra mseto. Kwa Waislamu walio wengi hudhihirika zaidi fikra za kibepari na demokrasia mahala pa Uislamu. Allah Taala Anasema:
وَلْتَكُنْ مِنْكُمْ أُمَّةٌ يَدْعُونَ إِلَى الْخَيْرِ وَيَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَوْنَ عَنْ الْمُنْكَرِ وَأُوْلَئِكَ هُمْ الْمُفْلِحُونَ
“Na liwepo kutokana na nyinyi kundi, linalolingania kheri, na linaloamrisha mema na kukataza maovu. Na hao ndio walio fanikiwa”. (Al-Imran 3:104).
Ni wajibu kujipinda zaidi kulingania khair (Uislamu) katika miezi mitukufu ili kupata ujira mkubwa sana. Tutafute nyenzo ya kuamrisha na kukataza, nayo ni serikali ya Kiislamu (Khilafah)
Malipo ya ulinganizi ni makubwa kwa kuwa amali yenyewe sio ndogo. Imeambatana na misiba, joto na maumivu kutoka kwa wapinzani, makafiri, na watawala wa kidemokrasia.
a. Kulingania umoja wa Kiislamu.
Watu inapasa walinganiwe umoja wa Ummah wa Kiislamu, kuepuka sintofahamu za bandia zilizotengenezwa na wasio tutakia mema.
وَاعْتَصِمُوا بِحَبْلِ اللَّهِ جَمِيعًا وَلاَ تَفَرَّقُوا (آل عمران: 103).
“Na shikamaneni kwa kamba ya Mwenyezi Mungu nyote pamoja, wala msifarikiane” (Al-Imran 3:103).
Msisitizo huu wa Mwenyezi Mungu SWT katutaka sisi Waislamu tuwe pamoja katika mambo ya misingi ya dini na kiusimamizi wa kisiasa. Katika ulinganizi wa jambo hili tupinge na kufafanua mbinu mbalimbali za kudhoofisha umoja wetu wa kimaumbile kama uzalendo, utaifa, umajimbo, umadhehebu nk. zinazotumika kutugawa na kupunguza nguvu yetu kama Ummah mmoja. Mpaka baadhi ya Waislamu kuzithamini na kuzibeba fikra hizo ngeni zinazopigiwa debe na wamagharibi kuleta mifarakano na kusambaratisha umoja wa Ummah wa Kiislamu.
Pia tuoneshe kwa ushahidi kuwa kwa umoja wetu kama Ummah hatujawahi kushindwa. Kwamba kiungo chetu thabiti ni aqidah ya Kiislamu na kila kinachochipuka kutokana na aqidah hii. Tuwe wamoja zaidi katika mambo msingi ya dini yetu ikiwemo hukmu za Kiislamu.
Aidha, tuoneshe kwa Ummah sababu ya leo hii kuwa na mivutano na mijadala isio ya msingi baina yetu, kama mivutano ya muandamo wa mwezi, siku ya Arafa, na maulidi, khitma nk. ni kututoa katika jukumu la msingi la ulinganizi wa kutabikishwa kwa sharia za Mwenyezi Mungu SWT katika ardhi.
b. Kurejesha kujiamini kwa Waislamu
Ni wajibu kuwalingania Waislamu warejeshe thika yao ya asili, yaani kujiamini kwa Uislamu wao kuwa ni dini ya haki na ushindi. Katika hilo lazima iwe samba mba na kusafisha kila fikra mbovu zilizojengwa kwa waislam kwamba ni wadhaifu, hawawezi kujitawala na kutawala ulimwengu. Eti wamagharibi wana nguvu sana. Tuoneshe uimara wetu.
c. Kuonesha vipimo sahihi vya vitendo.
Katika ulinganizi wetu hatuna badi kufafanua kwa kina vipimo vya vitendo vya Muislamu, ambavyo ni halali na haramu. Yaani halali aitende na haramu ajiepushe nayo. Katika hali kama hiyo vipimo visivyokuwa hivyo kama maslahi kamwe sio vipimo vyetu, bali ni vipimo vya hatari kwa Uislamu bali kwa wanadamu kwa jumla. Kwa kuwa mtenda kitendo anaweza kutenda lolote hata kutesa, kuuwa na kudhuru mwengine kwa suala la maslahi kama tuonavyo leo chini ya mfumo thakili a kibepari na nidhamu yake ya kisiasa ya demokrasia.
d. Kubainisha uadui dhidi yetu
Kuwabainishia Ummah chanzo cha fitna na uadui wa makafiri dhidi yetu, kwa kuufahamisha hatari ya mpambano mkali wa kifikra baina ya Uislamu na ukafiri wa kidemokrasia wa kimagharibi. Kwamba fikra ya Kiislamu inapingwa kwa juhudi na mikakati kabambe na wamagharibi wakiongozwa na Marekani kutumia medani mbalimbali kuanzia thaqafa, siasa, sheria pamoja na uvamizi wa kinguvu katika biladi za Kiislamu.
e. Kuonesha suluhisho la kudumu
Tulinganiane kwa kuwaonesha Waislamu na wanadamu kwa jumla kuwa suluhisho muafaka la kudumu la Kiislamu katika kuiweka dunia kuwa mahala salama pa kuishi Waislamu na wanadamu kwa jumla ni uwepo wa sharia za Mwenyezi Mungu SWT katika maisha ya watu zikiwa chini ya usimamizi wa Khalifah wa Kiislamu. Kutokana na hilo kutapatikana uadilifu, haki na ustawi wa kweli kwa wanadamu wote bila ya kuzingatia dini zao, kabila wala rangi.
Abu Nuthtaq Hamza
Risala ya Wiki No. 109
21 Dhu al-Hijjah 1442 Hijri / 31 Julai 2021 Miladi
Maoni hayajaruhusiwa.